“WAWATA HIMIZENI MIITO”
WITO umetolewa kwa
wanawake wakatoliki nchini kuhimiza miito mitakatifu kuanzia
ngazi za familia, jumuiya ndogo ndogo,vigango, parokia hadi majimboni ili
Kanisa liweze kupata hazina kubwa ya mapadri na masista watakaolitumikia kimwili
na kiroho pamoja na watu wake.
Aidha imeelezwa kuwa mapadri na masista
waliopo umri unazidi kuongezeka na hivyo Kanisa linahitaji vijana wa kike
na kiume watakaoandaliwa katika malezi na kusomeshwa
katika Seminari mbalimbali ili waweze kushika majukumu ya
kichungaji na kitume katika Kanisa mahalia.
Hayo yamesemwa na Katibu wa Wanawake
Wakatoliki Taifa(WAWATA) ambaye pia ni Mwenyekiti wa WAWATA Jimbo Kuu Dar
es Salaam, Bi.Desderia Mahita wakati wa hitimisho la Kongamano la
siku tatu la Kanda ya Nyanda za Juu Kusini lililofanyika jimboni Mbeya
na kuwashirikisha wanawake wa majimbo 8 ya Jimbo Kuu Katoliki Songea.
Majimbo ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini katika
Jimbo Kuu Songea yaliyoshiriki katika Kongamano hilo tangu Juni
23 hadi 25 ni pamoja na Jimbo Katoliki Mbeya, Lindi, Mtwara, Tunduru Masasi, Njombe,
Iringa, Mbinga na Songea lenyewe ambapo zaidi ya wanawake 1000
walishiriki.
Katibu huyo ambaye ni mlezi wa
WAWATA Kanda ya Nyanda za Juu Kusini amewaalika
wanawake wote kuwa wanapohitimisha Kongamano hilo wabebe
jukumu la kwenda kuhimiza miito mitakatifu katika familia zao na jumuiya
ndogo ndogo.
“Akina Mama ni jukumu letu kwenda kuhimiza
miito mitakatifu, chukueni hiyo kazi na mjiulize je Jumuiya, Kigango,
Parokia na Jimbo lina mapadri na masista wangapi na mkawahimize
watoto waende seminari isiwe kwa fasheni bali mkaguswe mioyoni mwetu na
tuombe baraka za Mwenyezi Mungu tuishi maisha ya familia takatifu
kama ya Yesu, Maria na Yosefu, tuhimizane na tukahimizane kufunga na
kubariki ndoa,”amesisitiza.
“Wanawake Wakatoliki tuwe wakamilifu
yaani tusiwe eti misa ya kwanza tunasali kanisani na misa ya pili
tunaenda kwenye maombi katika madhehebu ambako tunakatazwa kuvaa
rozari na tunakatiwa na rozari…lakini tuwe watu wa msamaha, sisi
wanandoa enzi zetu wakati tunafanyiwa mafundisho ya ndoa tulikuwa tunafundishwa
na mababa kuwa tukigombana ndani ya nyumba tuhakikishe tunapatana
kabla ya jua halijazama,” amefafanua Bi.Mahita.
Ameongeza,”Tuweke jitihada katika kuwalea
mapadri wetu kwani wamewaacha Baba, Mama na ndugu zao wanalitumikia
Kanisa, hivyo padri akifiwa, kuuguliwa, akihitaji msaada wowote uwe
wa usafiri... wewe kama WAWATA toa msaada haraka.”
Kwa upande wao, Katibu wa WAWATA Jimbo
Kuu Songea na Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Bi.Imelda Mbawala amesema
katika Kongamano wanajifunza na kubadilishana uzoefu, mada
mbalimbali huku wakiongozwa na kauli mbiu MWANAMKE MKATOLIKI
MWENEZAJI WA HURUMA YA MUNGU, ambapo wamechagua viongozi
wapya wa WAWATA Kanda ya Nyanda za Juu Kusini ambapo Mwenyekiti ni, Bi.
Rita Materu kutoka Jimbo Katoliki Iringa, Makamu Bi. Teresia Chilumba(Lindi),
Katibu Bi.Imelda Mbawala(Songea), Katibu Msaidizi, Bi.Agness Hyera(Tunduru
Masasi) na Mtunza hazina ni Bi.Rebeka Kapinga(Mbinga).
Naye, mlezi wa WAWATA, Sista Verena Kwimba amewaagiza
masista kuwasaidia wanawake kufahamu kuwa kufunga siyo sala
na sadaka tu bali pia na kusamehe yote,”tuwasaidie wanawake kama wanatoa
sadaka na kusali wakati wa mfungo lakini wakitoka na manung’uniko mfungo
wao unakuwa ni bure unafutwa.”
Mwenyekiti wa WAWATA Jimbo la Mbeya,Bi.
Everada Mangwala amesema katika kongamano hilo wamefanya matendo ya
huruma ya kuwatembelea watoto yatima katika kituo cha Igogwe na
kuwapelekea mahitaji mbalimbali ikiwemo chakula,seminari ndogo ya Mbalizi kituo
cha Yatima Iyunga,walitembelea kituo cha malezi cha watawa wa kike.
Bi.Mangwala ametoa wito kwa
wanawake kuanza kujiwekea akiba kidogo kidogo ili wapate
kuwatolea wahitaji katika Kongamano la Kanda ya Kusini, mwezi Juni mwaka
2018 linalotarajiwa kufanyika jimboni Mbinga kwani kuhitimishwa kwa Kongamano
la Mbeya ndiyo mwanzo wa maandalizi ya lile la Mbinga.
Katika ibada hiyo viongozi wastaafu
wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini akiwemo aliyekuwa Mwenyekiti wa WAWATA
wa awamu iliyopita ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jimbo Katoliki Mtwara, Bi. Verena Mahundi na Mweka hazina Bi.
Agness Ng’owo wa Parokia ya Makambako, Jimbo Njombe kwa niaba ya viongozi
wenzao wastaafu wameomba mshikamano uendelee kudumu
huku wakifafanua zaidi kuwa WAWATA siyo kuvaa
sare za vitenge tu bali ni mwanamke yeyote mkatoliki mbatizwa
aliyefikisha umri wa miaka 18 kuusimamia na kuutekeleza kwa
uadilifu utume wake kwa Kanisa.
Comments
Post a Comment