Buriani Naibu Askofu Mdai
WAKRISTO wakatoliki
Jimbo Katoliki Mahenge wamepata pigo baada ya kuondokewa na Naibu Askofu wa
Jimbo hilo Padri Kalistus Mdai
ambaye pia alifanya kazi ya
ukufunzi katika Seminari ya Kasita, pia Mshauri Mkuu wa Askofu wa Jimbo
Katoliki Mahenge.
Kifo cha Naibu
Askofu huyo kimetokea Mei 20, Jumamosi akiwa safarini kuelekea katika hospitali
ya rufaa ya Mt. Francis Ifakara kwa ajili ya kupatiwa matibabu
Akizungumza kwa
niaba ya Askofu wa Jimbo Katoliki Mahenge na Jimbo Katoliki Ifakara, Naibu Askofu wa Jimbo Katoliki Ifakara Padri
Boniventura Mchalange amesema kuwa Mapadri wa majimbo hayo mawili wameupokea
kwa masikitiko makubwa msiba huo kwani wamempoteza mtu muhimu hususani katika
suala la usuluhishi.
“Tumeumia kwa kweli
na tumepata pigo kwani msuluhishi wetu mkubwa ametutoka, nafikiri itatuchukua
muda mrefu sana kuweza kumsahau,” amesema Padri Mchalange, Naibu wa Askofu
Jimbo Katoliki Ifakara.
Aidha Naibu Askofu
huyo amesema mapadri kwa ujumla wametoa pole kwa wote waliopokea msiba huo na
wale wote waliotoa ushirikiano mpaka kufikia hatua ya kuuaga mwili pamoja na
kushiriki mazishi.
Marehemu Padri
Kalistus Mdai alifariki akiwa jimboni Mahenge na mwili wake ukasafirishwa mpaka
jimboni Ifakara ambapo Mei 24 ilifanyika ibada ya kuuaga mwili huo katika
Kanisa la Mt. Andrea ambalo ni Kanisa Kuu la Jimbo Ifakara, kabla ya kurudishwa
jimboni Mahenge na kufanyiwa ibada ya kuuaga Mei 25 katika Kanisa Kuu la Jimbo.
Wasifu wa Marehemu
Padri Kalistus Mdai
alizaliwa tarehe 18 Januari 1939 na alisoma katika shule ya seminari Kasita
iliyopo jimboni Mahenge na alipata Daraja takatifu la upadri tarehe 15 August
1966 katika Kanisa la Kwiro ambalo ni Kanisa Kuu la Jimbo Mahenge.
Mnamo Mwaka 1967 alianza
kazi ya utumishi kama Paroko Msaidizi katika Kanisa la Mt. Andrea Ifakara mpaka
mwaka wa 1970 alipoteuliwa kuwa Leacture wa Kwanza Mwafrika katika Seminari ya
Kasita, akiwa seminarini hapo alipewa
Cheo cha Umonsinyori (MSGR).
Mwaka 1979 Aliyekuwa
Askofu wa Jimbo Katoliki Mahenge Askofu
Iteka alimtoa Msgr Mdai katika Seminari ya Kasita na kumsogeza Kwiro
katika Kanisa Kuu la Jimbo, ambapo alikuwa Naibu Askofu pia Mshauri Mkuu wa
Askofu kwa kipindi chote.
Msgr Mdai amefariki
akiwa na umri wa miaka 78, atakumbukwa na wakristo wengi kwani ni miongoni mwa
wakristo wachache wanaofahamu juu ya Historia ya Jimbo Katoliki Mahenge na lile
la Ifakara.
Atakumbukwa pia
wakati akiwa Mkufunzi katika Seminari ya Kasita kwa kusaidia mapadri wengi
kufanikisha azma yao ya kuwa mapadri.
Mwenyezi Mungu
ailaze roho yake mahali pema, Amina.
Comments
Post a Comment