MARA WATAKIWA KUSHIRIKI KWA WINGI WIKI YA MAZINGIRA KITAIFA
MKUU wa Mkoa wa Mara Dk Charles
Mlingwa amewataka wananchi wa Mkoa huo kujitokeza kwa wingi katika maadhimisho
ya siku ya mazingira yanayofanyika Kitaifa Mkoani humo katika uwanja
wa Mwenge wilayani Butiama kuanzia Juni 1-4 mwaka huu.
Akizungumza na wandishi wa habari
katika ukumbi wa uwekezaji uliopo katika ofisi ya mkuu wa Mkoa, mkuu huyo wa
Mkoa amesema kuwa maadhimisho ya siku ya mazingira kitaifa yalitarajiwa yatazinduliwa
rasmi na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mh.January
Makamba Juni mosi mwaka huu wilayani Butiama.
Mlingwa amefafanua kuwa baada ya
uzinduzi huo kutakuwepo na Kongamano na tafrija mbalimbali kuhusiana na
masuala ya mazingira kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali kutoka nje na ndani ya
Mkoa watakaowasilisha mada mbalimbali kuhusu umuhimu wa kuhifadhi mazingira na athari za uharibifu wa mazingira, ambapo
jumla ya miche 1500 itapandwa wakati wa maadhimisho hayo katika maeneo
mbalimbali ya wilaya ya Butiama.
Amezitaja baadhi ya mada
zitakazotolewa kuwa ni pamoja na kuelimisha wananchi kupanda miti ili kuhifadhi
mazingira na kukidhi mahitaji ya dunia katika kupambana na ongezeko la
hewa ukaa, kuijengea jamii uwezo juu ya uelewa wa masuala ya mazingira na
changamoto za kijamii zinazijitokeza katika kutunza mazingira, kwa kuwa Mkoa wa
Mara ni miongoni mwa mikoa ambayo ina uharibifu mkubwa wa mazingira .
Amesema lengo kubwa la kufanya maadhimisho hayo ya Kitaifa wilayani Butiama ni kuenzi kazi zote za uhifadhi wa mazingira zilizofanywa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius K. Nyerere katika kuhifadhi mazingira enzi za uhai wake .
Neema Chausiku, mkazi wa mjini Musoma amesema kuwa mkoa wa Mara ni moja kati ya mikoa inayotumia nishati ya mkaa na kuni kwa wingi, hivyo maadhimisho hayo yatawasaidia wananchi kupata elimu kuhusiana na upandaji wa miti na uhifadhi wa mazingira kwa ujumla, ili kuepukana na ukame ambao wamekuwa wakikabiliana nao.
Maadhimisho hayo yanatarajiwa kufungwa
rasmi Juni 4 mwaka huu na makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan.
Comments
Post a Comment