Liganga yanufaika na Mradi wa Maji Mtiririko
JUMLA ya shilingi milioni 270 zimetumika kukamilisha
mradi wa maji ya mtiririko katika Kata ya Liganga mkoani Ruvuma.
Akihubiri katika Misa Takatifu wakati wa sherehe za
uzinduzi wa mradi huo wa maji, Padri Dominikus Nyoni ambaye ni Paroko wa
Parokia ya Liganga Jimbo Kuu Katoliki Songea amesema kuwa jamii nzima ya Kata
ya Liganga haina budi kumshukuru Br. Dr Ansigar OSB kwa kufadhili mradi huo wa
maji.
Amesema Br. Dr Ansigar OSB kwa muda wa miaka 30
amekuwa akifanya kazi kubwa ikiwemo ya kuiongoza hospitali ya Peramiho kama
Mkurugenzi wa hospitali hiyo. Amefafanua kuwa, Br.Dr Ansigar OSB
amejishughulisha kuongeza majengo ya hospitali na kuongeza idadi ya madaktari
katika hospitali hiyo.
Ameongeza kuwa licha ya kazi yake ya udaktari Br.Dr
Ansigar OSB amejitahidi kuwaletea wananchi wa Tarafa ya Ruvuma maendeleo
ikiwemo upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama.
Aidha katika sherehe hizo za uzinduzi wa maji ya
mtiririko Br.Dr Ansigar OSB ametoa baiskeli kumi na tatu {13} kwa wahudumu wa
afya msingi majumbani ili ziwasaidie katika kutoa huduma za afya katika vijiji vya Tarafa ya Ruvuma na amegawa vyeti kwa
wahudumu wapya 25 wa afya msingi majumbani.
Kwa upande wake Br. Dr Ansigar OSB amesema kuwa kwa
kiasi kikubwa magonjwa mengi yamepungua kama vile magonjwa ya ngozi, malaria,
kuhara, Ukimwi na kifua kikuu. Katika sherehe hizo ametoa wito kwa wananchi
kujiunga na mpango wa Bima ya Afya, na ameahidi mwaka huu kuendelea kuchimba
pampu nyingine nane {8} katika kata zote zilizopo katika Tarafa ya Ruvuma.
Akizungumza kwa niaba ya serikali, Kaimu Mkurugenzi
wa Halmashauri ya wilaya ya Songea Bwana Venance Komba amesema serikali
inatambua mchango wa Br. Dr Ansigar OSB kwa wananchi wa Tarafa ya Ruvuma.
Amesema serikali itahakikisha inasimamia na kuvitunza vyanzo vyote vya maji ili
huduma hiyo ya maji ya mtiririko iweze kuwa endelevu.
Comments
Post a Comment