ASKOFU LEBULU ASHAURI MAPADRI WAPEWE USHIRIKIANO KULIIMARISHA KANISA
ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu
Katoliki Arusha Mhashamu Josaphat Lebulu amewataka waamini nchini
kuonyesha umoja na mshikamano kwa mapadri ili kuleta maendeleo ya parokia na jamii
kwa ujumla.
Askofu Lebulu ameyasema hayo kwenye
Misa Takatifu ya uzinduzi wa parokia mpya ya Mtakatifu Yuda Thadei Ilboru Jimbo
Kuu Katoliki Arusha ambayo imezaliwa kutoka Parokia ya Loruvani zamani ikiwa kigango
cha Ilboru.
Katika misa hiyo mapadri wawili wamesimikwa
ambao watakabidhiwa parokia hiyo mpya, padri Simon Amsi ambaye atakuwa paroko
na padri Euzeb Mapua ambaye atakuwa msaidizi wa paroko, wote wametoka katika
Shirika la Wanakanuni wa kawaida wa Mtakatifu Victor wa Kanuai ya Mtakatifu Augustino
(CRSV) Jimbo Katoliki Mbulu ambayo makao yake makuu yapo nchini Ufaransa.
Akizindua Parokia hiyo Askofu Lebulu
amesema kuwa waamini wote bila kujali umri wanapaswa kuwapa ushirikiano mzuri
mapadri kwa kushauriana nao changamoto mbalimbali zinazojitokeza jambo ambalo
litaleta manufaa kwa parokia na kuwepo kwa maendeleo.
“Parokia nyingi ambazo zimekuwa na
maendeleo ni kutokana na mshikamano wa wakristo baina yao na mapadri bila
kuwepo na chuki wala ubaguzi huku wakihitaji manufaaa ambayo yametokana na
nguvu zao, lakini kama waamini hawatakuwa na upendo kwa viongozi wao, maendeleo
wanatayasikilizia kwenye vyombo vya habari.” Amesema.
Aidha amewasihi waamini kuiendeleza
parokia hiyo kwa kujenga miundombinu ya kutosha huku wakiwatia moyo mapadri
wapya jambo ambalo litasababisha nao kuwa na vigango ambavyo vitazaliwa na parokia
hiyo.
Naye Abate Mkuu wa Shirika la
Wanakanuni wa kawaida wa Mtakatifu Victor wa Kanuai ya Mtakatifu Augustino
(CRSV) kutoka nchini Ufaransa, Hugues Paulze d'Ivory ambaye amekuja kwa ajili ya
tukio hilo amemshukuru Askofu Josaphat Lebulu kwa kuwapokea mapadri katika
Jimbo lake.
Amesema Shirika hilo ambalo lilianza
miaka 30 iliyopita nchini Ufaransa litahakikisha linaonyesha mshikamano
wa kutosha kwa utii na unyenyekevu huku akiwasihi wakristo kuwa na umoja ili
kazi ya Mungu isonge mbele.
Kwa upande wake paroko mpya padri Simon
Amsi akitoa shukrani zake, amesema kwamba atahakikisha anafanya kazi ya Mungu
kadri awezavyo pamoja na msaidizi wake padri Euzeb Mapua .
Amewataka wakristo kuwapa ushirikiano
wa kutosha ili kazi ya Mungu isonge mbele na kwamba wawe wakristo wa kusali.
Katika tukio hio, pia Askofu Mkuu Josaphat
Lebulu amewapa wanafunzi 44 Sakramenti ya Komunyo.
Comments
Post a Comment