Benki ya Mkombozi kutoa gawio Julai
Benki ya
Biashara ya Mkombozi inatarajia kutoa gawio kwa wanahisa wake kuanzia mwezi
Julai mwaka huu.
Mwenyekiti wa Bodi ya Benki hiyo, Bw.
Method Kashonda amesema wametoa ratiba ya utoaji wa gawio kama ilivyoelekezwa na
Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), hivyo wanatoa gawio kuanzia tarehe 6 Julai
mwaka huu.
Kutokana na ratiba hiyo amesema tarehe
ya kutangaza gawio ni Mei 27 mwaka huu ambayo itafuatiwa na ununuaji wa hisa
pamoja na gawio kuanzia Mei 27 hadi Juni 15.
Mwenyekiti huyo ambaye alikuwa
akizungumza katika mkutano mkuu wa benki hiyo ambao uliwaleta pamoja mamia ya
wanahisa Jijini Dar es Salaam, amesema ununuzi wa hisa bila gawio utaanza
tarehe 16 Juni mwaka huu.
“Kufungwa kwa kitabu cha orodha ya
wanahisa ni Juni 20 mwaka huu na kufungua tena kitabu cha orodha ya wanahisa ni
Juni 21 mwaka huu,” amefafanua Mwenyekiti huyo.
Amesema pia baada ya hatua zote hizo
kukamilika, wanahisa wanatarajiwa kupokea gawio lao kuanzia Julai 6 mwaka huu.
“Gawio litalipwa moja kwa moja kwenye
akaunti ya mwanahisa au kwa kupitia M-Pesa, Airtel Money au Tigopesa,” amesema
Mwenyekiti na kuongeza kuwa benki hiyo imetangaza gawio la shilingi 20 kwa kila
hisa.
Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo Bi.
Edwina Lupembe akielezea utendaji wa benki kwa kipindi kilichoishia tarehe 31
Disemba 2016, amebainisha kuwa benki hiyo ilifanikiwa kukusanya amana za jumla
ya shilingi bilioni 102.55 na kutoa mikopo na karadha ya jumla ya shilingi
bilioni 73.80. Jumla ya Rasilimali za benki zilifikia shilingi bilioni 128.17
ikilinganishwa na shilingi bilioni 111.31 iliyokuwepo mwaka 2015.
“Hadi kufikia mwaka 2016, miaka minane
baada ya kuanzishwa benki hiyo ilikua na matawi 6 na vituo vya kutoa huduma za
kifedha viwili katika mikoa mitano ya Tanzania. Benki hii ilipata faida baada
ya kodi ya shs. Bilioni 1.04 mwaka 2016,” amesema.
Benki ya Biashara ya Mkombozi
ilianzishwa mwaka 2009 na Kanisa Katoliki Tanzania na taasisi zake kwa
madhumuni ya kusaidia wafanyabiashara wadogo, wa kati na wakubwa kupata huduma
za kifedha.
Ili kutanua wigo zaidi, waanzilishi wa
benki hiyo walitoa nafasi kwa watanzania wengine wakiwemo wafanyabiashara na
wawekezaji kununua hisa zake ili kuongeza nguvu.
Benki ya Mkombozi
ina matawi matano na vituo viwili vya huduma za kifedha katika mikoa ya Dar es
Salaam, Bukoba, Moshi, Mwanza na Morogoro.
Comments
Post a Comment