Kanisa kuadhimisha siku ya maskini duniani
BABA
Mtakatifu Fransisko ametoa ujumbe wake kwa Siku ya Kwanza ya Maskini
Duniani inayoadhimishwa Jumapili ya 33 ya Kipindi cha Mwaka wa Kanisa Novemba
19, 2017 na kusema kuwa ‘Watoto wadogo, tusipende kwa neno, wala kwa ulimi,
bali kwa tendo na kweli’.
Kauli mbiu ya
maadhimisho ni “Tusipende kwa neno bali kwa tendo”. Baba Mtakatifu anasema,
upendo wa namna hii unahitaji jibu makini, kwani umemiminwa bila madai yoyote
na uko tayari kuwasha moyo kwa mwamini yoyote licha ya dhambi na mapungufu ya
kibinadamu. Hili linawezekana ikiwa kama neema ya Mungu na upendo wenye huruma
unapokelewa moyoni na kusaidia kuongoza utashi na vionjo vya upendo kwa Mungu
na jirani!
Baba Mtakatifu anaendelea
kusema, Kanisa daima limekuwa likisikiliza na kujibu kilio cha maskini na
wahitaji kama inavyoshuhudiwa kwenye Kitabu cha Matendo ya Mitume, kwa
kuwachagua Mashemasi saba walioshuhudiwa kuwa wema, wenye kujawa na Roho na
hekima, ili waweze kutoa huduma kwa maskini, hii ni alama ya kwanza ya huduma
kwa maskini kutokana na utambuzi kwamba, maisha ya Kikristo yanafumbatwa katika
udugu na mshikamano.
Mwinjili Luka anatoa kipaumbele
cha kwanza katika Injili yake matendo ya huruma, changamoto kwa waamini hata
katika nyakati hizi kuwa ni mashuhuda wa huruma ya Mungu. Mtume Yakobo
anaonya tabia ya kuwapendelea matajiri kwa kuwavunjia heshima na kuwabeza
maskini, lakini hawa ndio matajiri wa imani na warithi wa ufalme wa Mungu.
Anakumbusha kwamba, imani bila matendo imekufa.
Baba Mtakatifu anakiri kwamba,
kuna wakati katika historia ya Kanisa, waamini walimezwa na malimwengu, lakini
Roho Mtakatifu akawasaidia kukumbatia mambo msingi, kiasi cha kuibua waamini
ambao walijisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa maskini.
Wakaandika historia ya Ukristo kwa unyenyekevu na kiasi; kwa ukarimu na upendo;
wakawahudumia ndugu zao maskini kwa ari na moyo mkuu.
Amesema Siku ya Maskini Duniani
iwe fursa ya kushikamana kwa kujenga na kudumisha utamaduni wa watu kukutana na
kusaidiana, kama alama ya urafiki, umoja na udugu unaovunjilia mbali kuta za
utengano kwa sababu mbali mbali. Maadhimisho haya yakamilishwe kwa namna ya
pekee Kanisa linapoadhimisha Siku kuu ya Yesu Kristo Mfalme wa Ulimwengu.
Comments
Post a Comment