Kasi ya uharibifu wa mazingira inatisha!


θ Ask Msonganzila awaonya viongozi wabinafsi
θ Makamba: Ekari 2500 zinateketea kila siku

n Na Pascal Mwanache, Dar
Taifa linapoadhimisha wiki ya mazingira inayofikia kilele chake Juni 4 imeelezwa kuwa kukithiri kwa ubinafsi wa viongozi wanaojali ajenda binafsi kuliko manufaa ya umma, kukosekana kwa usimamizi mzuri wa sera na sheria za mazingira, na mamlaka za mazingira kufanya kazi kwa matukio, ni kati ya mambo yanayochangia kukithiri kwa uharibifu wa mazingira nchini.
Hayo yameelezwa na Askofu wa Jimbo Katoliki Musoma Mhashamu Michael Msonganzila katika mahojiano maalum na gazeti hili, ambaye amebainisha kuwa mamlaka husika za mazingira hazijaweka mkazo mkubwa kwenye utunzaji wa mazingira hali inayochangia uharibifu mkubwa wa mazingira.
Aidha amebainisha kuwa sera na sheria za mazingira zinaishia kwenye karatasi huku watu wenye tamaa ya fedha wakiendelea kuharibu mazingira kwa manufaa yao binafsi. Ameiasa jamii ijikite katika matumizi ya nishati mbadala ili kupunguza uharibifu unaotokana na matumizi ya kuni na mkaa na kuisihi serikali iweke mazingira yatakayowezesha upatikanaji wa nishati hizo kwa urahisi.
“Sera za mazingira zisiishie kwenye makaratasi tu, tunahitaji kuonyesha usomi wetu kwa kuwaelimisha watu wa chini kwamba uharibifu wa mazingira unawaathiri hata wao pia. Pia kila mtu kwenye familia yake apande miti walau kumi na kuisimamia” amesema.
Pia amezitaka mamlaka za mazingira kuwezesha na kuhamasisha taasisi na mashirika binafsi na ya kidini ili zishiriki kikamilifu katika utunzaji wa mazingira badala ya kuweka kipaumbele kwenye taasisi za serikali pekee. Amesema kuwa Kanisa Katoliki limekuwa mstari wa mbele katika upandaji wa miti ambapo parokia nyingi zimezugukwa na miti mikubwa, jambo linaloashiria uwezo wa taasisi za kanisa katika kutunza mazingira.
“Taasisi zote zinazohudumia jamii kama makanisa, zipewe nafasi katika mipango na mikakati ya utunzaji wa mazingira kwa kuwa taasisi hizo zina uwezo na zinawafikia watu wa maeneo yote.  Asasi nyingi zinazoshughulikia uhifadhi wa mazingira zimejikita zaidi mjini huku uharibifu mkubwa ukifanyika maeneo ya vijijini” amesema Askofu Msonganzila.

Padri Dkt Msafiri: Tuzingatie Teolojia na maadili ya uumbaji
Kwa upande wake Balozi wa Mazingira nchini Padri Dkt. Aidan Msafiri amesema kuwa namna bora ya kukabiliana na kukithiri kwa uharibifu wa mazingira ni kurejea kwenye teolojia na maadili ya uumbaji, inayomtaka mwanadamu kuutunza ulimwengu na kuuacha ukiwa bora zaidi ya alivyoukuta. Amesema kuwa binadamu amepewa dunia siyo kwa ajili ya kutumia rasilimali tu bali awajibike katika kutunza na kuhifadhi vyote vilivyomo na kutoa haki kwa vizazi vijavyo.
“Binadamu ndiye chanzo kikuu cha uharibifu wa mazingira kwa kudhani kwamba yeye pekee ndiye mwenye haki na maamuzi ya kuyatumia mazingira anavyopenda. Dunia siyo mali ya mwanadamu wala siyo mali ya serikali, tumeshirikishwa uumbaji tukiwa kama waumbaji wenza. Ni lazima tukiri ukuu wa Mungu katika uumbaji, tutumie tunu za busara na haki katika kutumia rasilimali” amesema Padri Msafiri.
Ameongeza kuwa waraka wa Baba Mtakatifu Fransisko wa ‘Laudato Si’ ndiyo kanuni kuu katika utunzaji wa mazingira ulimwenguni, unaotoa dira kwa kanisa na ulimwengu na kwamba kanisa linapaswa kuendelea kuwa mfano katika kutunza mazingira.
“Kanisa kupitia taasisi zake kama shule linapaswa kuendelea kuwa mfano wa utunzaji wa mazingira. Na inafaa ifike mahali ambapo Sakramenti zote za kanisa zitolewe kwa watu baada ya kuwa wameotesha miti. Kwa mfano, mtoto akitaka kubatizwa basi wazazi au wasimamizi wapande miti kwanza, wanaopewa nadhiri, wanaofunga ndoa waoteshe miti ndipo wapewe hizo sakramenti” ameongeza.

Waziri Makamba atoa hali halisi
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia muungano na mazingira, January Makamba amesema kuwa kuna uharibifu mkubwa wa mazingira nchini ambapo takribani ekari 2500 za misitu zinateketea kwa siku, huku zaidi ya miti laki tisa ikipotea kwa mwaka.
Aidha amebainisha kuwa vyanzo vya maji ambavyo vingi vipo katika misitu vinakauka kwa kasi kubwa huku sumu ya viwandani inayomwagwa kwenye mfumo wa ekolojia ikiendelea kuleta madhara katika mazingira.
“Inawezekana uchumi wetu ungekua kwa kasi zaidi kama tusingeharibu mazingira. Tunaandika sera mpya ya mzingira kwa kuwa sera tuliyokuwa nayo sasa, ya mwaka 1997, ni butu na mambo mengi sasa yamebadilika” ameeleza.

Tathmini ya Kanisa juu ya mazingira na uchumi wa nchi
Katika kongamano la kitaaluma lililojadili juu ya uchumi na mazingira, wadau wa uchumi walibainisha kuwa ukuaji wa uchumi usiojali uhifadhi wa mazingira, maliasili na utu wa kila mwananchi ni pigo ambalo haliakisi uhalisia wa ukuaji huo.
Kongamano hilo lilijikita katika dhima ‘Mchango wa mafundisho jamii ya Kanisa Katoliki katika kukua kwa uchumi na maendeleo ya jamii’ na lilifanyika katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Stella Maris Mtwara.
“Ili kuwa na uchumi wenye tija na maendeleo endelevu, ni lazima tutoke kwenye dhana ya kusema ‘nini ninataka’ na kujikita katika dhana ya ‘nini Mungu anataka’. Vinginevyo tujiandae kulipa deni la kuharibu Ekolojia, na kusababisha utu wa mwanadamu ukose maana” alieleza Askofu Nyaisonga wa Jimbo Katoliki Mpanda, ambaye kitaaluma ni mwana Jiografia.


Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI