KONGAMANO LA WAWATA LAWANUFAISHA WASIOJIWEZA
Wanawake Wakatoliki
Tanzania, (WAWATA) Kanda ya Mashariki wametoa zawadi ya vitu mbalimbali kwa
kituo cha watoto yatima cha Mtakatifu
Elizabeth kilichopo Parokia ya Mbingu jimboni Ifakara vyenye thamani ya zaidi ya shilingi Laki tano
ili kuwasaidia watoto hao kuzikabili changamoto mbalimbali kituoni hapo.
Msaada huo umetolewa mwishoni mwa mwezi
Juni, wakati WAWATA wakihitimisha kongamano la Wanawake wakatoliki ikiwa ni
sehemu ya Hija katika kituo hicho kinachomilikiwa na shirika la masista wa upendo wa Mtakatifu Fransisko.
Msaada uliotolewa ni
pamoja na; Sukari mifuko miwili, mafuta ya kula ndoo 2, sabuni ya unga mifuko
2, Sabuni za mche box 4, Magodoro madogo 20, Vitenge pande 24 na Juisi dazani
12 .
Akikabidhi msaada huo kwa
niaba ya wanawake hao Mwl. Faith Peter
kutoka Jimbo Katoliki Ifakara ameupongeza uongozi wa kituo hicho kwa
kazi wanayoifanya na kuongeza kuwa kimsingi hilo ni jukumu la jamii hasa akina mama.
Akipokea msaada
huo msimamizi wa kituo hicho, Sista
Maria Anatolia Mgubike, amewashukuru wanawake hao kwa upendo wao, na kuonesha
kujali huduma hiyo, na kuongeza kuwa
kituo hicho hadi sasa kina miaka 14 tangu kuanzishwa , na kimepokea watoto 168
mpaka sasa, ambapo kati yao 20 wamefariki.
Akizungumza na Kiongozi,
Katibu wa WAWATA Jimbo Katoliki Ifakara, Mwl. Longina Mbano amesema kuwa pia wamepeleka misaada mingine katika vituo
viwili, kimoja ni Gereza la Kiberege, ambapo walipeleka vitu vyenye thamani ya
shilingi 227,000/-, na kituo cha pili ni Kituo cha kulelea watoto wenye ulemavu
wa akili cha Bethlehemu, kilichopo Parokia ya Kibaoni, Jimbo Katoliki Ifakara,
ambacho kilipata vitu vyenye thamani ya shilingi 194,000/-
Kwa upande wake
Mwenyekiti wa WAWATA Kanda ya Mashariki mama Rose Mpembe, amemshukuru Askofu wa
Jimbo Katoliki Ifakara, Mhashamu Salutaris Libena kwa kushirikiana na kina mama
hao tangu walipofika mpaka siku ya mwisho na kuongeza kuwa Kongamano hilo
limefana sana huku wakipendekeza Kongamano lijalo lifanyike jimboni Zanzibar.
Baadhi ya Mada
zilizowasilishwa katika Hija hiyo ni pamoja na Mwanamke mkatoliki mwenezaji wa
huruma ya Mungu, iliyowasilishwa na padri Thadei Memba, katika mada hiyo
kulikuwa na hoja kama; Dhana ya huruma ya Mungu, Dhana
ya wanawake kutoka katika katiba ya WAWATA, Sifa za mwanamke, Matendo
ya huruma, Namna ya kueneza huruma ya Mungu, na mwisho Padri Memba alitaja
kumbukumbu
mbalimbali za Mama Bikira Maria ambazo Kanisa linazienzi katika
kumkumbuka mama Maria.
Aidha kina mama hao
walipata fursa pia ya kujifunza mada ya kumkomboa mwanamke kiuchumi, mada
iliyowasilishwa na padri Sirili Njau, mada aliyoigawa katika sehemu tatu, Mama
ni nani? Ni mambo gani amekosa mpaka akombolewe na Namna ya kujikomboa.
Kongamano la WAWATA Kanda
ya Mashariki linajumuisha majimbo Katoliki
6, Dar es salaam, Tanga, Zanzibar, Morogoro, Mahenge na Ifakara, ambalo
limefanyika Jimbo Katoliki Ifakara.
Kongamano hilo lilianza Juni 23, kwa Ibada ya Misa takatifu iliyoongozwa na
Askofu wa Jimbo hilo, Mhashamu Salutaris Libena iliyofanyika katika Parokia ya
Ifakara.
Comments
Post a Comment