Makinikia: Askofu Msonganzila ampongeza Rais Magufuli
Askofu wa Jimbo Katoliki Musoma
Mhashamu Michael Msonganzila amesema kuwa kilichojitokeza kwenye ripoti ya pili
ya mchanga wa dhahabu ni kwa sababu wahusika wa pande zote mbili hawakuwa
makini katika kuona umuhimu wa kumwendeleza mwanadamu kutoka pale alipo.
Askofu Msonganzila ameyasema hayo
hivi karibuni alipokuwa akitoa maoni yake juu ya ripoti ya pili ya mchanga wa
dhahabu iliyowasilishwa hivi karibuni na kamati iliyoundwa na Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na kuwasilishwa Juni 12 mwaka
huu.
Amesema wahusika hao wangemakinika
katika kuangalia namna ya kumsaidia mwanadamu kiuchumi badala ya kipaumbele
chao kikubwa kuwa ni kuchuma pesa bila kumwangalia mwanadamu atanufaikaje na
uwepo wa rasilimali hiyo tuliyopewa zawadi na Mwenyezi Mungu katika nchi yetu.
“Binafsi nampongeza Rais Magufuli na
ninamuunga mkono kwa hili alilolifanya, amekuwa makini katika kuibua sakata la
makanikia, mzalendo wa nchi yake na mtetezi wa wanyonge na nawaomba watanzania
tuungane kwa pamoja katika kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Rais wetu,”
amesema Askofu Msonganzila.
Askofu amesema kuwa
kinachowaangusha wananchi ni kukosa uzalendo kwa nchi yao na ubinafsi
umekuwa mkubwa, na mbaya zaidi asilimia 10 tu ndiyo ambayo imekuwa ikiliangamiza
Taifa, kutokana na kusaini mikataba bila kuisoma, na kwamba sakata hili
litumike kumfundisha kila mwananchi kuwa makini wanapotaka kufanya jambo lolote
hasa lenye maslahi kwa Taifa.
Comments
Post a Comment