Miaka 100 ya Upadri: Maelfu Geita kushuhudia maajabu Nyamatongo
Maelfu ya wakazi wa mkoa wa Geita, wakiwemo wakristo na waamini wa
dini mbalimbali zikiwemo dini za asili wanatarajiwa kushuhudia maajabu ya kituo
cha Hija cha msalabani Nyamatongo katika Parokia ya Nyantakubwa Jimboni Geita,
ambapo ndani yake wataadhimisha misa Takatifu itakayoongozwa na Askofu wa Jimbo
Katoliki Geita Mhashamu Flavian Kassala.
Wakristo wakatoliki wanafanya Hija hiyo kuanzia Jumamosi hii wakiadhimisha
miaka 100 tangu kuwapata mapadri wa kwanza waafrika kutoka Kanda ya Ziwa, na
pia miaka 150 tangu ukristo uingie Tanzania Bara. Eneo la Nyamatongo limesifika
siku nyingi kutokana na msalaba ulioachwa na wamisionari tangu mwaka 1880-81
wakijaribu kuanzisha misheni hapo japokuwa haikufanikiwa.
Miongoni mwa masimulizi yaliyoenea hapo na kuwavuta watu wengi
kutamani kufika hapo ni kifo cha ajabu cha Padri Andreas Combarieu, aliyefia
hapo kwa homa ya ini, na kwa amri ya Mtemi Rwoma wa Karumo, alitupwa ziwani
katika kisiwa cha Juma, usiku, lakini asubuhi yake wakamkuta anaelea ufukweni.
Wakazi hao, wakiwemo waamini wa dini zingine wamepanga kwenda
kuona hicho kinachowavuta wakristo wengi kumiminika kila siku eneo hilo na
kushinda huko kuanzia asubuhi hadi joni wakipanga mawe na kutengeneza barabara
kwa ajili ya kuandaa tukio kubwa la misa Takatifu itakayofanyika jumamosi hii.
Akizungumza na Gazeti hili, Paroko wa Parokia ya Nyantakubwa
jimboni Geita Padri George Nkombolwa amesema tukio hili ni fursa ya kuwajenga
kiimani waamini wa Geita, lakini hata wafuasi wa dini nyingine wana hamu kubwa
ya kuona jinsi wakatoliki wanavyoheshimu msalaba wa Yesu na hivyo kuamua
kulitunza eneo la msalabani.
Padri George Nkombolwa ambaye pia ni Mkurugenzi wa Uchungaji jimboni
amesema kuwa Nyamatongo ni Mlango wa imani kwa kanda ya ziwa, kwani hapo
walikaa mapadri watatu, Augustine Levesque, Ludovick Girault na Andreas
Combarieu wa shirika la wamisionari wa Afrika (White Fathers) waliokuja na msafara wa kwanza mwezi Desemba mwaka 1878
wakaenda Uganda, na baada ya kukataliwa Uganda, walikuja Karumo wilayani
Sengrema na wakakaa hapo Nyamatongo msalabani.
Miongoni mwa mambo wanayofanya wakristo wa Parokia ya Nyantakubwa
katika maadhimisho hayo ni pamoja na kujenga makumbusho (MUSEUM) itakayotoa
masimulizi juu ya Padri huyo Andreas Combarieu na mapadri walioishi hapo
Ama hakika ni chanzo Bora kuenea kwa Imani kwa Kanda ya ziwa na tunamshukuru sana fr.George kwa kujitoa kwake kuhakikisha eneo hilo linaendelea kimiundombinu ambayo itakidhi mahitaji ya mahujaji wote kwa Jimbo la Geita .Ee Mungu uibariki Imani katoliki
ReplyDelete