Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)
Na
Charles Rwehumbiza
UINJILISHAJI
BAGAMOYO NA TANZANIA KWA UJUMLA
Kutokea Bagamoyo,
wamisionari wa Shirika la Roho Mtakatifu waliweza kuendelea kuinjilisha sehemu
mbalimbali za Tanzania kama vile Mhonda (Morogoro), Mandera (Morogoro), Kilema
Kibosho (Moshi) na Kondoa, n.k. Kutokana na ugumu wa watu wa Bagamoyo kukubali
Injili na uamuzi wa wamisionari wenye asili ya Uholanzi kuhamia Morogoro mjini.
Bagamoyo iliachwa
kwa kipindi kirefu bila huduma za mapadri au wakiwa wanapata huduma ya
Misa Takatifu mara moja kwa mwezi. Jambo hili lilisababisha ukuaji wa
Kanisa la Bagamoyo kuwa duni sana hadi mwaka 1992 padri mwafrika wa kwanza
alipoingia na kuweka makazi ya kudumu Bagamoyo.
Padri huyu wa kwanza
mwafrika kuinjilisha Bagamoyo sio mwingine ila Padrei Valentine Bayo wa Shirika
la Roho Mtakatifu. Tangu aingie Bagamoyo, Padri Bayo chini ya usimamizi wa
shirika lake, ameweza kuipa Bagamoyo hadhi iliyo nayo leo hii. Hakika haitakuwa
vibaya kumwita Padri Bayo “Baba wa Uinjilishaji Mpya Bagamoyo”.
Anastahili jina hilo
kwani ameitoa Bagamoyo kutoka parokia na jengo moja la Kanisa hadi kuwa na
parokia tatu, yaani Moyo Safi, Epifania na Kristo Mfalme pamoja na vigango vyao
vingi Bagamoyo mjini na vijijini.
Utume wa Padri Bayo na
Shirika lake haukubakia tu kwenye usimamizi wa sakramenti bali ulijikita kwenye
maeneo yote yanayohusiana na ukombozi wa mwanadamu, yaani elimu, afya na huduma
nyingine za kijamii.
Hadi leo hii, shule za
Marian ni mojawapo ya shule zinazoongoza kwa ufaulu Tanzania. Vijana wengi wa
Bagamoyo na mikoa mingine waliopitia kwenye shule za ufundi Marian wameweza
kujipatia taaluma za ufundi na ajira katika fani mbalimbali zikiwemo useremala,
ushonaji, uashi, ufundi vyuma, rangi, upishi na huduma za hoteli. Hakika elimu
imekuwa njia kuu ya uijilishaji mpya Bagamoyo, kwani leo hii tunashuhudia uwepo
wa Chuo kikuu kishiriki cha Marian Bagamoyo kinachojikita kwenye Elimu ya
Sayansi.
CHANGAMOTO ZA UNJILISHAJI BAGAMOYO
Kanisa linapojiandaa kwa
sherehe za miaka 150 ya uinjilishaji Bagamoyo na Tanzania kwa ujumla, linakiri
kuwa changamoto bado ni nyingi. Kanisa la Bagamoyo linaonekana bado kama changa
kwani sehemu zake nyingi hasa za vijijini bado ziko kwenye hadhi ya uinjilishaji
wa kwanza.
Hata hivyo, Bagamoyo ni
wilaya inayokua kwa kasi, ukuaji unaochochea wahamiaji na wawekezaji wengi
kuingia Bagamoyo. Ukuaji huu umeongoza hata Kanisa Katoliki la Tanzania
kufikiria kuanzisha jimbo la Bagamoyo ifikapo mwaka 2018. Ukuaji huu
unaashiria, bila shaka, mahitaji zaidi ya wachungaji na miundombinu ya Kanisa.
Miongoni mwa miundombinu
itakayohitajika kwa jimbo jipya ni nyumba za malezi ikiwemo seminari. Hata
hivyo itakumbukwa kuwa iliyokuwa seminari ndogo ya jimbo la Morogoro, St.
Peters, na kuhamishiwa Morogoro mjini mwaka 1969, sasa inatumiwa na Wakala wa
serikali wa Maendeleo na Uongozi wa Elimu ya Msingi Tanzania (Chuo cha ADEM).
Inasemekana kuwa Kanisa
lilikubaliana na Serikali kuwa seminari hiyo itumiwe na serikali kwa muda
lakini kinachoonekana sasa ni kuwa, sio seminari tuu, ila hata eneo la Kanisa
linaloizunguka linadaiwa kumilikiwa na ADEM. Jambo hili bado liko mahakamani
likisubiri maamuzi licha ya ukweli kwamba linategemea zaidi msukumo kutoka
jimboni Morogoro.
KUINGIA KWA WAMISIONARI WA AFRIKA TANZANIA
Miaka kumi baada ya
wamisionari wa Shirika la Roho Mtakatifu kuingia Bagamoyo, walikuja wamisionari
wengine wakiwemo Wabenediktini na Wamisionari wa Afrika (White Fathers). Hawa
wote walikaa na wamisionari wa Shirika la Roho Mtakatifu kwa kipindi cha miezi
mitatu wakijifunza juu ya mila na desturi za waafrika pamoja na kuzoea hali ya
hewa ya Afrika Mashariki.
Miongoni mwa hao
wamisionari walikuwa Wamisionari wa Afrika (White Fathers) walioingia Bagamoyo
mwaka 1878 wakitokea Algeria. Kulingana na mikakati ya uinjilishaji kipindi
kile Wamisionari wa Afrika walitumwa kuelekea mikoa ya kati na kanda ya ziwa,
jambo lililowapeleka hadi Tabora, Uganda na Bukoba.
Baadhi ya Wamisionari wa
Afrika wa kwanza wamezikwa kwenye makaburi ya Kanisa Katoliki Bagamoyo na mwaka
2000 kundi la wamisionari hawa walirudi Bagamoyo na kusimika mnara wa
kumbukumbu kwenye mlango wa makaburi hayo. Mnara huu ulikuwa ishara ya shukrani
kwa Shirika la Roho Mtakatifu kwa ukarimu wao uliowawezesha kuzoea mazingira ya
Tanzania Bara.
Tarehe 18 Novemba, 2017
Askofu Msaidizi wa jimbo la Bukoba, Mhashamu Methodius Kilaini, kama mwana
historia alialikwa na Wamisionari wa Afrika kule Bagamoyo ili kuwapatia semina
juu ya utume wao hapa Tanzania na Afrika kwa ujumla.
Kwa siku nzima Askofu
Kilaini alikuwa nao katika ukumbi wa mikutano wa hoteli ya Stella Maris,
Msalabani, Bagamoyo. Semina hiyo ni mojawapo ya matukio ya Shirika la White
Fathers kuadhimisha miaka 150 tangu kuanzishwa kwake huko Algeria mnamo mwaka 1868
kwa lengo la kuinjilisha bara la Afrika.
Katika maadhisho ya
Jubilei ya miaka 150 ya Uinjilishaji, tumeshuhudia maadhimisho mbalimbali
ambayo ni matunda ya Uinjilishaji huo.Hapo tarehe 27 Desemba, 2017 Jimbo
la Bukoba limefanya sherehe kubwa parokiani Kashozi likisherehekea miaka 125
tangu kuhubiriwa Injili kwa mara ya kwanza hapo mwaka 1892. Tunawashukuru
wamisionari wa Afrika kwani ndio walioleta Habari Njema ya Kristu jimboni
Bukoba wakiwa wanatokea Uganda. Wamisionari hawa walijenga kanisa la kwanza
huko Kashozi mwaka 1892 ambalo sehemu yake kubwa ilibomolewa na tetemeko la
ardhi la Septemba 10, 2016.
Tunda lingine la
Uinjilishaji ni maadhimisho ya miaka 100 ya upadre Tanzania. Maadhimisho haya
yalizinduliwa Rubya huko Bukoba tarehe 1 Oktoba 2016 na kufungwa kitaifa tarehe
15 Agosti 2017. Maadhimisho hayo hayo yamefanyika pia huko Rwanda na Jimboni
Bunda huko Ukerewe.
Ningependa kumalizia kwa
kuonesha kumbukumbu moja muhimu ya wamisionari wa kwanza Bagamoyo inayofanana
sana na makanisa ya kwanza huko Bukoba: “Miembe Misafa.”
Miembe hii yenye
umri ilioteshwa miaka ya 1870 pande zote mbili za barabara ya karibu
urefu wa kilomita moja kuelekea Kanisa la Moyo Safi wa Bikira Maria. Miembe hii
inatengeneza “nyarulembo” inayokutwa kwenye makanisa ya zamani
huko Bukoba.
Kwa wasiojua, “Nyarulembo”
ni uwanja mkubwa mrefu wenye miti mikubwa kila upande huku na huku iliyooteshwa
au kusimikwa kuelekea ikulu ya mfalme. Karibuni wote tuingie ikulu ya Mfalme wa
milele kwa kuadhimisha jubilee hii ya miaka 150 ya uwepo wa “Mfalme”
wetu huko Bagamoyo. Kristu Mfalme wetu aendelee kututawala na kutuongoza
daima.
Comments
Post a Comment