Askofu Msonganzila akemea ukatili kwa watoto
Askofu wa
Jimbo Katoliki Musoma Mhashamu Michael Msonganzila amekemea ukatili unaoendelea
kwa watoto katika jamii akisema kuwa ni unyama kwa watoto ambao hawawezi
kujitetea.
Askofu
Msonganzila ameyasema hayo hivi karibu katika Misa Takatifu ya kumshukuru Mungu
kwa kumaliza mwaka 2017 salama na kuvuka mwaka mpya salama, iliyofanyika
katika Kanisa Kuu la Maria Mtakatifu Mama wa Mungu.
Amesema
kuwa, kumekuwepo na ongezeko kubwa la vitendo vya ukatili kwa watoto wadogo
ambavyo vinahusishwa na chuki na hasira ambavyo vyote ni kinyume na
mapenzi ya Mungu na uumbaji.
“Matendo
ya kikatili kwa watoto yanazidi kuongezeka kwa kasi, tunamtesa mtoto kwa
kumchoma moto kwa kupoteza shilingi 100 au kwa kulamba sukari.
Nani
asiyefahamu maumivu ya moto? Ni mateso makali sana. Mtoto wa miaka miwili ama
mitatu unamchoma kwa nini usimuonye kwa kumkemea au kumpa adhabu inayoendana na
umri wake?
Wakristo
wenzangu watoto ni zawadi kutoka kwa Mungu, wadogo hawa hawana pa kukimbilia,”
amesema.
Amesema
hakubali wala hatambui kauli inayosema ‘Watoto wa mitaani’ kwani hakuna mtoto
wa mitaani, wanaokuwepo mtaani wamekimbia mateso nyumbani.
“Naombeni
sana kila mmoja atumie siku hii kuomba toba, kujitakasa na kama mtu amethubutu
kushiriki kutoa mimba hata awe mume naombeni sana mtubu dhambi ili kuanza mwaka
kwa amani na utulivu “alisema Askofu Msonganzila.
Aliwaomba
waamini wa Jimbo hilo kuhakikisha wanapunguza mizigo mingi ya hasira ambayo
ndio inayosababisha matendo ya kinyama yakiwemo mauaji yasiyo na hatia,
ukatili kwa watoto wadogo na wanawake pamoja na ugomvi ndani ya jumuiya na
familia zao.
“Ugomvi,
chuki na na hasira ndiyo chanzo cha uvunjifu wa amani, ndugu zangu tusikubali
kubeba kilo 100 za hasira maana ukiwa na hasira na usijue kuizuia hasira yako
unaweza kusababisha mambo mabaya yasiyompendeza Mungu.
Tujitahidi
mwaka huu uwe mwaka wa baraka na mafanikio kwa kila mmoja wetu, kwa kuanza
kuweka mipango mizuri ndani ya familia zetu na kukemea vitendo vya ukatili
katika jamii yetu,” amesema Askofu Msonganzila.
Comments
Post a Comment