WAZAZI WAASWA KUTOA MAFUNZO YA DINI KWA WATOTO
Na waandishi wetu Musoma.
WAZAZI
na walezi nchini wametakiwa kuwa mfano kwa kuwahamasisha watoto kusali kwenye
familia, jumuiya, kanisani pamoja na kuonesha matendo ya huruma katika
kuwajenga kiimani na upendo ili kukabiliana na magumu yanayotoka katika
familia.
Wito huo umetolewa na Paroko
wa parokia ya Maria Mtakatifu Mama wa Mungu Jimbo Katoliki Musoma padri
Benedict Luzangi katika Misa ya sikukuu ya familia Takatifu ya Yesu, Maria na
Joseph ambayo imeambatana na utoaji wa sakramenti ya ubatizo kwa watoto 28.
Padri Luzangi amesema kuwa
familia ni kitovu cha maisha ya fadhila ambayo huleta umoja, upendo,
uwajibikaji, imani na malezi bora ya kiimani.
Hata hivyo padri Luzangi
amekemea tabia ya baadhi ya wazazi wasioona uchungu wa familia za watu wengine
hasa wanapokuwa na shida pia wasiotunza na kuwajali wazee kwani kwa kufanya
hivyo ni sawa na kupungukiwa na imani kama mkristo na kwamba mali na
utajiri bila furaha ni sawa na bure.
Kwa upande wao wazazi na
walezi wa watoto hao kwa nyakati tofauti wameahidi kuwalea watoto katika misingi
bora ya kidini na kuwaandalia maisha bora ya kiroho na kimwili yenye kumpendeza
Mwenyezi Mungu.
Kwa upande wake, paroko
msaidizi wa parokia ya Mugango, Padri Cleophas Sabure amewataka wazazi na
walezi kuwalea watoto kulingana na maisha yao pasipo kutamani vitu wasivyokuwa
na uwezo navyo kwa kuwa jamii na Kanisa wanategemeana katika masuala mbalimbali
ya kiimani, kiuchumi na kimaendeleo na kuwakumbusha kujitathimini ili kuona
walichokifanya katika mwaka 2017.
Wakati huo huo, jumla ya
ndoa 14 zimefungwa katika maadhimisho ya sikukuu ya familia Takatifu katika
Parokia ya Kiabakari jimboni Musoma.
Maadhimisho hayo ya
Misa Takatifu iliyoongozwa na Askofu wa Jimbo Katoliki Musoma Mhashamu Michael
Msonganzila na paroko wa parokia ya Kiabakari padri Wojciech Adam na
kuhudhuriwa na waamini zaidi ya 600 katika Kanisa hilo la Huruma ya Mungu
Kiabakari.
Askofu Msonganzila amewaasa
wanandao hao kuiga familia Takatifu ya Yosefu, Maria na mtoto Yesu kwa kuishi
katika nguzo tatu ambazo ni ndoa, kufanya kazi kwa pamoja kama ilivyokuwa kwa
mtoto Yesu na wazazi wake na kuishi katika sala na kuwafundisha watoto
wao sala na kuwa na moyo wa shukrani katika maisha yao.
Amesema sala ni kiungo
kishikamanishi katika familia na hatimaye hujenga familia iliyo bora na ya
kumpendeza Mungu, hivyo familia ijikite zaidi katika kusali hasa kuwapeleka
watoto wao kanisani na kula nao pamoja na siyo kuwaacha wakishinda katika
mitandao ya kijamii ambayo itawapoteza kimaadili.
Amewausia wanandoa hao kuwa
na upendo wa kweli katika ndoa hasa kuvumilia, kunyenyekea, kushirikiana na
kusameheana pindi wanapokosana au kukwaruzana na palipo na shida wasisite
kutafuta ushauri.
Comments
Post a Comment