Bweni lateketea, Biblia na Rozari pekee vyasalia
Baadhi ya vifaa vilivyoteketea kwa moto lakini Biblia na Rozali zilikutwa salama
|
Hata baada ya moto kuteketeza vifaa hivi, Biblia na Rozari vimekutwa salama
|
θ Ni Seminari ndogo ya St. Mary Mbeya
JANUARI
21 mwaka huu zaidi ya wanafunzi 52 wa Shule ya Seminari ndogo ya
St.Mary’s ya Mbalizi Jimbo Katoliki Mbeya wamenusurika kifo
kutokana na ajali ya moto ulioteketeza bweni lote na vifaa vilivyokuwemo.
Aidha tukio jingine la ajabu ni kutoungua kwa Biblia
na Rozali Takatifu zilizokuwa zimehifadhiwa katika masanduku ya bati ya
wanafunzi licha ya vingine vyote na jengo kuteketea kwa moto.
Akizungumza na Gazeti Kiongozi, Gombera wa Seminari
hiyo Padri Edwin Mwimba amesema kuwa, tukio hilo limetokea siku ya jumapili
mara baada wanafunzi kutoka kanisani majira ya saa 5 asubuhi na kuendelea
na masomo darasani.
Ghafla wakashtuka kuona moshi ukitokea katika bweni
hilo na bahati nzuri hapakuwa na mwanafunzi yeyote aliyekuwepo ndani ya bweni
hilo hivyo wote wapo salama.
Padri Mwimba amesema bado haijafamika kiwango cha
athari zilizojitokeza kutokana na ajali hiyo ambayo pia haijafahamika
chanzo licha ya kila kitu kilichokuwepo ndani kuteketea isipokuwa Biblia za
wanafunzi pamoja na Rozari Takatifu ambavyo havikuungua.
“Kwa kweli tumekumbana na changamoto hiyo katika bweni
la St. James baada ya wanafunzi kupiga kelele na baadhi ya majirani na wazazi
waliokuwepo jirani walifika tukasaidiana kuuzima moto.
Wakati huohuo tukijaribu kupiga nambari za simu za kikosi
cha zimamoto ambazo hazikuwa na majibu hadi tulipowasiliana na Padri
aliyekuwepo jimboni ambaye alienda kutoa taarifa kwenye ofisi za zimamomoto
na hatimaye walifika kuuzima ingawa hakuna kitu tulichookoa, isipokuwa
Biblia na Rozari Takatifu,
“amesema.
Gombera huyo ameeleza kuwa bweni hilo lilikuwa
linahifadhi wanafunzi wa kidato cha kwanza. Baada ya kuteketea lote
wamewahamishia katika majengo mengine yaliyokuwepo wazi na wanaendelea na
masomo kama kawaida.
“Kwa ujumla kutakuwepo na uhitaji wa mavazi, magodoro,
vitanda, vitabu nk. kwani wamebakiwa na mavazi waliyokuwa wamevaa na
hiyo ndiyo changamoto kubwa,” amesema Gombera huyo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Naibu Kamishna wa Polisi,
Mohamed Mpinga amethibitisha kutokea kwa tukio hilo Januari 21
mwaka huu majira ya saa 6.30 mchana katika shule ya seminari ya St.Mary’s
iliyopo Kijiji cha Mapinduzi, Kata ya Nsalala,Tarafa ya Usongwe,Wilaya ya Mbeya
Vijijini mkoani Mbeya.
Kamanda Mpinga amefafanua kuwa bweni moja la St.James
liliwaka moto na kuteketea lote pamoja na mali zote za wanafunzi na
shule zilizopo ndani ya bweni hilo, hakuna madhara yeyote yaliyojitokeza
kwa binadamu.
Aidha tathmini halisi ya thamani ya uharibifu bado
haijafahamika na chanzo cha moto huo bado hakijajulikana na uchunguzi
unaendelea.
Comments
Post a Comment