Kanisa lafungua kitengo cha Magonjwa ya Mfumo wa Chakula Dodoma
Minja-DODOMA.
Kanisa
Katoliki hivi karibuni limefungua kitengo cha Magonjwa ya Mfumo wa Chakula
(ENDOSCOPY) katika Hospitali ya Mtakatifu Gemma iliyoko Miyuji Dodoma.
Wakati wa ufunguzi wa jengo hilo, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu
Katoliki Dodoma Mhashamu Beatus Kinyaiya ameiasa jamii kuwa na mwamko wa haraka
kuchangia huduma za afya pale zinapohitajika ili kunusuru maisha ya watanzania.
Pia iwe na mipango ya kudumu ya huduma za afya kwa
maendeleo.
Pamoja na hayo Askofu Mkuu Kinyaiya amesema ufunguzi wa
kitengo hicho ni muhimu kwa wananchi wa Dodoma kwani wamekuwa wakisumbuka kwa
muda mrefu na kuwataka madaktari katika Hospitali hiyo kuwa na moyo wa huruma
katika kuwahudumia wagonjwa.
Aidha amewasisitiza kulinda vifaa tiba katika kitengo hicho.
Kwa upande wake Mganga Mkuu Msaidizi katika Hospitali hiyo
Sista Dkt. Theodora Mwasu amesema kuwa,wazo la kuanzisha Hospitali hiyo
lilikuwa ni kwa ajili ya kuwatibu masista wagonjwa na wazee ambapo kwa sasa
hospitali hiyo inatoa huduma kwa jamii nzima.
Hata hivyo Sista Theodora ametaja baadhi ya changamoto
zinazoikabili Hospitali hiyo ikiwa ni pamoja na uhaba wa wafanyakazi, chumba
cha kuhifadhia maiti, ubovu wa barabara inayoingia hospitalini hapo na uhaba wa
vifaa tiba kutoka bohari kuu ya dawa.
Kutokana na hayo Mgeni Rasmi katika ufunguzi huo kwa niaba
ya Waziri wa Kazi, Ajira na Vijana Anthony Mavunde, Mkuu wa Wilaya ya Kongwa
Deo Ndenjembi amesema kuwa, serikali iko mbioni kumaliza tatizo la uhaba wa
wafanyakazi katika hospitali zote na kuwataka wananchi wa Dodoma kuwa na mwamko
wa kuitumia Hospitali ya Mtakatifu Gemma kwani inajitosheleza katika kutoa
huduma za afya.
Pamoja na hayo amesema kuwa, mwamko mdogo wa wakazi wa mji
wa Dodoma unachangia kudidimiza maendeleo ya hospitali hiyo na kuwataka
wananchi kuwa kichocheo cha maendeleo hospitalini hapo kwa maendeleo ya Taifa
kwa ujumla.
Wazo la kuanzishwa kwa kitengo cha magonjwa ya mfumo wa
chakula hospitalini hapo lilibuniwa na Sista Gemma Mkondoo kutokana na msukumo
alioupata kwa kusafirisha wagonjwa mara kwa mara kwenda kutibiwa Dar Es Salaam
huku wakiwa wadhaifu kiafya.
Hali hiyo ilimlazimu kuomba msaada kwa rafiki zake
waitaliano ambao wamesaidia kufanikisha huduma hiyo kwa karibu zaidi na jamii.
Comments
Post a Comment