Papa Francisko atuma salam na matashi mema kwa wakuu wa nchi

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu mchana tarehe 22 Januari 2018 amewasili mjini Vatican baada ya kuhitimisha hija yake ya kitume huko Amerika ya Kusini. Mara tu baada ya kuwasili, Baba Mtakatifu alikwenda moja kwa moja kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu, lililoko hapa mjini Roma, ili kumshukuru Bikira Maria Afya ya Warumi, kwa ulinzi na tunza yake ya kimama iliyomwezesha kukamilisha hija yake ya kitume, iliyokuwa na changamoto pevu katika maisha na utume wa Kanisa huko Amerika ya Kusini! Lakini, changamoto zote hizi amezikabili kwa: ari, moyo wa amani na umoja wa matumaini kwa watu wa Mungu huko Amerika ya Kusini.

Akiwa njiani kurejea mjini Vatican, Baba Mtakatifu alibahatika kupitia kwenye anga la Perù, Colombia, Venezuela, Ureno, Hispania, Ufaransa na hatimaye, Italia. Akiwa angani, Baba Mtakatifu ametuma salam na matashi mema kwa viongozi wakuu wa nchi hizi zote. Kwa namna ya pekee kabisa, amemshukuru na kumpongeza Rais Pedro Pablo Kuczynski wa Perù kwa ukarimu na mapokezi makubwa waliyomwonesha wakati wa hija yake ya kitume nchini humo. Anapenda kuwahakikishia sala na baraka zake za kitume kwa familia ya Mungu nchini humo!
Baba Mtakatifu amemwambia Rais Juan Manuel Santos wa Colombia katika ujumbe wake kwamba, bado anayo kumbu kumbu hai ya hija yake ya kitume nchini humo na kwamba, anawaombea wananchi wote wa Colombia amani na furaha. Alipowasili kwenye anga la Venezuela, amemwambia Rais Nicolàs Maduro wa Venezuela kwamba, anapenda kuiweka nchi ya Venezuela chini ya tunza ya Mwenyezi Mungu ili hatimaye, aweze kuwajalia amani na nguvu! Baba Mtakatifu Francisko amemwambia Rais Marcelo Rebelo de Sousa wa Ureno kwamba, bado anakumbuka hija yake ya kitume nchini Ureno kama sehemu ya kumbu kumbu ya miaka 100 tangu Bikira Maria alipowatokea Watoto watatu wa Fatima ambao kati ya wao wawili tayari amewatangaza kuwa watakatifu. Hawa ni Francis na Yacinta Marto wakati ambapo mchakato wa kumtangaza Sr. Lucia kuwa Mwenyeheri bado unaendelea katika ngazi ya kijimbo!
Akiwa kwenye anga la Hispania, Baba Mtakatifu amewatakia wananchi wote wa Hispania heri na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu katika ujumbe wa matashi mema aliomwandikia Mfalme Felipe VI wa Hispania. Amewahakikishia wananchi wa Ufaransa sala na baraka zake katika ujumbe aliomwandikia Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa. Baba Mtakatifu Francisko katika salam na matashi mema kwa Rais Sergio Mattarella wa Italia, amemwambia kwamba, katika hija yake ya kichungaji Amerika ya Kusini, amebahatika kukutana na umati mkubwa wa familia ya Mungu katika maeneo haya, ameguswa kwa namna ya pekee kabisa na imani yao na kiu ya kutaka kukua na kukomaa kiroho na kijamii. Baba Mtakatifu anapenda kuihakikishia familia ya Mungu nchini Italia sala kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi pamoja na kuwapatia baraka zake za kitume!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Vatican News!

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI