BENKI YA BIASHARA YA MKOMBOZI YAPATA MKURUGENZI MTENDAJI MPYA

 Januari 27, 2018: Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya Biashara Mkombozi imetangaza uteuzi wa Bw. George Shumbusho kama Mkurugenzi Mtendaji mpya wa benki hiyo kuanzia Disemba 1, 2017.
Uteuzi huu unafuatia kustaafu kwa Mama Edwina Lupembe ambaye ni miongoni mwa viongozi maarufu katika sekta ya kibenki na ameiongoza benki ya Mkombozi kwa miaka tisa.
Akizungumza katika hafla maalumu ya kumuaga Mama Lupembe na kumkaribisha mkurugenzi mpya, katika Baraza la Maaskofu Tanzania, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Bw. Method Kashonda aliwashukuru wote wawili kwa makabidhiano mazuri ya ofisi ambayo yameleta imani kuwa benki inabaki katika mikono salama.

 Mwenyekiti huyo alimpongeza Mama Lupembe kwa umahiri wake katika uongozi. Mama Lupembe alijiunga na benki hiyo Agosti 29, 2009 huku akiwa ameshika nafasi za juu kwa zaidi ya miaka 20 katika sekta ya kibenki, taasisi za umma na kuwa mjumbe katika bodi mbalimbali za mashirika ya umma na binafsi.
Alisema Bodi inampongeza kwa utumishi wake uliotukuka wakati wote wa uongozi wake ambao umeifanya Benki ya Mkombozi kuwa moja ya benki zinazoongoza katika soko la Tanzania. Kwa mujibu wa Bw. Kashonda, Mama Lupembe amekuwa na mafanikio makubwa katika miaka 37 aliyokuwa katika utumishi.

 Alisema Bw. Shumbusho, Mkurugenzi Mtendaji Mpya na mtaalam anayetambuliwa na Masoko ya Kimataifa, ana Shahada ya Uzamili kutoka Maastricht School of Management / Eastern and Southern Management Institute (MsM / ESAMI) anajiunga na Benki ya Mkombozi, huku akiwa na uzoefu mkubwa uliojikita zaidi katika Masoko ya Kimataifa.
 Bw. Kashonda alisema Mkuugenzi Mtendaji mpya aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali katika benki za Exim Bank, Stanbic, Standard Chartered na NMB kwa zaidi ya miaka 15.
“Tuna imani kuwa Bw. Shumbusho atatumia uzoefu wake na kufanya kazi kwa karibu na wafanyakazi wa Mkombozi, wateja, bodi na wadau wengine ili kuhakikisha benki inapata mafanikio zaidi ikiwemo kutoa huduma bora na kuwajibika katika utoaji wa huduma za kijamii.

 Akizungumza katika hafla hiyo, Mama Lupembe aliishukuru bodi, wanahisa na wafanyakazi wote kwa ujumla kwa ushurikiano mkubwa waliompa katika kipindi chote cha uongozi wake. 
“Ni kwa kupitia ushirikiano huu, niliweza kuwaongoza vizuri. Naamini kuwa Bw. Shumbusho ataendeleza mazuri yote tuliyoanzisha na kufanya hata makubwa zaidi kwani benki hii ina nafasi ya kupata mafanikio zaidi ya haya hasa ukizingatia kuwa sasa imeshaorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam. Yote haya yaliwezekana kwa sababu ya uwazi na uadilifu katika kuwahudumia wateja wetu. Nakutakia kila la heri Mkurugenzi mpya na nakuahidi ushirikiano wangu pale ambapo utahitaji ushauri wangu,” alisema.

 Naye Bw. Shumbusho aliishukuru Bodi ya Wakurugenzi kwa kuwa na imani na yeye na pia kumshukuru Mkurugenzi aliyemaliza muda wake kwa kuweka msingi mzuri.
“Nimemfahamu Mama Lupembe kwa muda mrefu sasa katika sekta ya kibenki na sina wasiwasi kuwa ninachukua nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na mmoja wa wakurugenzi watendaji mahiri hapa nchini. Hii ni changamoto kubwa sana kwangu kwani lazima na mimi nihakikishe kuwa naiweka benki hii katika nafasi ya juu kabisa kabla muda wangu wa kuondoka haujafika. Yote haya yatawezekana kupitia ushirikiano kutoka kwetu sote ikiwemo bodi, wanahisa na wafanyakazi kwa ujumla. Nawashukuru wote kwa mapokezi yenu mazuri,” alisema.



 Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na maaskofu kutoka Majimbo mbalimbali, wajumbe wa bodi, wadhibiti, maafisa watendaji wa benki zingine wafanyakazi wa Mkombozi na wadau mbalimbali.
Benki ya Biashara ya Mkombozi ilianzishwa mwaka 2009 na Kanisa Katoliki Tanzania na taasisi zake kwa madhumuni ya kusaidia wafanyabiashara wadogo, wa kati na wakubwa kupata huduma za kifedha. 
Ili kutanua wigo zaidi, waanzilishi wa benki hiyo walitoa nafasi kwa watanzania wengine wakiwemo wafanyabiashara na wawekezaji ili kuongeza nguvu.


Comments

Post a Comment

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI