Iringa wapata mashemasi 10
Askofu
wa Jimbo Katoliki Iringa Mhashamu Tarcisius Ngalalekumtwa, Jimbo la Iringa,
hivi karibuni ametoa Daraja Takatifu la ushemasi kwa waseminari kumi katika
Kanisa Kuu la Kiaskofu la Moyo Mt. wa Yesu Parokia ya Kihesa.
Waliopata
daraja hilo la ushemasi ni Mseminari Alfred Msanzi (Kihesa), Barnabasi Kalinga
(Mafinga), Betram Kigodi (Usokami), Eugen Ngatunga (Migoli), Festo Kitosi
(Consolata –Mshindo),
Florence Mlangwa (Ifunda). Jayfa-Zacharia Kayage
(Madege), Moses Mgimiloko (Tosamaganga), Nelson Mapembe (Ifunda) na mseminari
Polycarp Kindole wa Parokia ya Usokami.
Askofu Ngalalekumtwa amesema kuwa maaskofu na mapadri
wanahitaji wasaidizi ambao ni mashemasi na hatua wanayoindea ina madai makuu ya
wema.
“Maaskofu na mapadri wanahitaji msaada wenu maana
tuna kazi nyingi. Mtawasaidia kutangaza neno la Mungu na kutoa sakramenti
kadhaa ukiwemo ubatizo, komunyo na ndoa,” amesema Mhashamu Ngalalekumtwa na
kuongeza kuwa;
“Ninyi ni watumishi wa Kristo na Kanisa lake,
washiriki na wajenzi wa Kanisa la Mungu, mna vitabu vya sala na muwe na matendo
ya uadilifu na wema wenye kujaa roho Mtakatifu na hekima” amesema.
Amewaambia Mashemasi hao kuwa wamependelewa nafasi
hiyo na Kristo hivyo hawapaswi kumuangusha sababu anabaki kuwa mpole na mwema.
Ameeleza kuwa, Daraja la Takatifu la Ushemasi ni
hatua ya mpito, wapo safarini wanapoelekea kwenye ngazi ya ukuhani na hivyo
waamini wanapaswa kuwa nao katika sala ili wamalize salama.
Aidha,
kwa nyakati tofauti, Mhashamu Askofu Ngalalekumtwa mwanzoni mwa juma amesali na
watoto wa shirika la Utoto Mtakatifu katika Parokia ya Kihesa, huku akiwataka
watoto hao kuwaombea viongozi wa serikali ili wawe na haki na watawale kwa
amani.
Ni utaratibu ambao askofu Ngalalekumtwa amejiwekea
kusali na watoto kila mwanzoni mwa mwaka na kuwabariki katika masomo yao.
Mwaka huu watoto hao wamesali kutoka parokia 9 za
Vikaria ya Consolata ambayo inahusisha parokia 11 za Jimbo la Iringa.
“Salini kwa ajili ya wazazi wenu, walezi na walimu
wenu, muwaombee pia viongozi wawe na haki na watawale kwa amani, tutunze amani
duniani.
Pia mjifunze mambo mazuri kutoka kwa Yesu ambayo ni
wema, upole, ukweli na uaminifu, usafi na matendo mema na unyenyekevu,” amesema
Mhashamu Ngalalekumtwa.
Comments
Post a Comment