SHIRIKA LA WATAWA LA MABINTI WA MARIA LAPATA VIONGOZI

n Na Patrick Mabula, Tabora.
SHIRIKA la watawa la Mabinti wa Maria limepata viongozi wake  wakuu baada ya  kumchagua Sista Theresia Sungi  kuwa Mama Mkuu kuendelea kuliongoza, makamu wake akichaguliwa  Sista Evodia Lupagaro kuendelea na nafasi hiyo huku Halmashauri yao wakiwa ni Sista Sophia Mbihije, Sista Victoria Mamiro na Sista Yohana Kulwa.
Akiwasimika viongozi hao, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Tabora, Mhashamu Paulo Ruzoka hivi karibuni katika misa ya kuwasimika amewataka viongozi hao siku zote wajiweke katika maongozi ya Mwenyezi Mungu na wawe wamoja katika kuliongoza shirika lao. 
Askofu Mkuu Ruzoka amesema watawa hao ambao walikuwa wamefunga Novena ya siku 60 wakisali na kumuomba Mungu na Roho Mtakatifu aweze kuwaongoza kupata uongozi  wao, waendelee kuwa wamoja  na wakiwa na nia moja huku wakidumu katika sala na mashauriano.
Amesema uchaguzi huo uliowaweka madarakani viongozi wa watawa hao wa shirika la Masista wa Mabinti wa Maria kwa mapenzi ya Mungu uwafanye wawe wanyenyekevu kwake  na awalinde na wote wawe na upendo, mshikamano na kuvumiliana.
Askofu Mkuu Ruzoka amesema Kristo sharti atawale  kutokana na kuwa Shirika ni chombo cha ukombozi  wa watawa  wana wajibu wa kuwakomboa watu wengine kwa kuongozwa na Roho Mtakatifu aendelee kuwasaidia  kufanya kazi za shirika.
Amesema  yeye kama mlezi wa shirika anaamini lina watawa  wazuri wenye vipaji mbalimbali  na wacha Mungu   ambao wamekuwa wakijitoa kuwatumikia  watu na Mungu  na  kuwaomba waendelee kuwa na moyo huo wakiongozwa na katiba yao  na nadhiri  zao za usafi wa roho .
Katibu wa Shirika la Watawa wa Mabinti wa Maria na msemaji wao Sista Sophia Shija amesema wakiongozwa na Roho Mtakatifu, wameamua kumrudisha  madarakani  tena Mama Mkuu Sista Theresia Sungu kwani kazi zake alizofanya zimelisaidia shirika na wana imani ataendelea kufanya makuu kwa kushirikiana na Halmashauri yake.
Naye Mama Mkuu wa Shirika, Sista Sungi amesema anamshukuru Mungu na mlezi wao Askofu Mkuu Paulo Ruzoka kwa kuwalea, kuwasimamia vizuri kwa upendo na kuwa wajibu waliopewa wameupokea kwa moyo wote.
Mama Mkuu Sista Sungi amesema watatimiza wajibu wao katika kuliongoza shirika lao kwa mapenzi ya Mungu wakiongozwa na utii na usimamizi wa Mama Bikira Maria kufikia malengo ya shirika na kuomba msaada wa sala na ushirikiano wakiongozwa na Roho Mtakatifu na kuwashukuru watawa wote  kwa  moyo wao wa kujitoa.

Kwa mjibu wa taarifa za shirika la Watawa la Mabinti wa Maria lenye makao yake Kipalapala  Jimbo Kuu Katoliki Tabora, kwa sasa limetimiza miaka 60 toka lianze mwaka 1957, toka uongozi wa utawala  wa wamisionari na sasa limejitanua na kuwa la ulimwengu mzima huku uchaguzi huo uliowaweka madarakani viongozi wake ukiwa uchaguzi wa sita.


Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI