‘Viongozi wa Dini msiogope kuonya mtu!’

·      Sahihisheni makosa ili watu waishi kwa haki
·      Msiendeleze urafiki unaoficha maovu

Na Pascal Mwanache, Dar

WITO umetolewa kwa Wakleri nchini kutoogopa kuonya mtu kwa kuwa watu wanahitaji kuonywa ili waache maisha mabovu na hatarishi kwao wenyewe na wengine.
Hayo yamesemwa na Askofu wa Jimbo Katoliki la Moshi Mhashamu Isaac Amani, wakati akitoa homilia katika adhimisho la Misa Takatifu ya kutoa Daraja Takatifu la Ushemasi kwa mashemasi wapatao 7, katika Kanisa Kuu la Kristo Mfalme Moshi.
Akiwaasa mashemasi hao wapya, Askofu Amani amesema kuwa kamwe hawapaswi kuendekeza urafiki ambao unaficha maovu ili wapendeke, kwani kwa kufanya hivyo watakuwa wanaisaliti Injili.
“Msiogope kuonya mtu. Sahihisheni makosa ili watu waishi kwa haki maana haki inapoharibiwa amani inapotea. Nani atakayepiga kelele haki ikae mahali pake? Ni watumishi wa Mungu. Lakini mkiwa na hofu na woga wa kuhubiri na kusahihisha, maovu yatazaa matunda ya maovu mengine zaidi” ameeleza.
Pia Askofu Amani amesema kuwa Ushemasi, Upadri na Uaskofu ni madaraja yanayovusha huruma ya Mungu iwafikie watu katika mazingira na nyakati mbalimbali. Amesema kuwa anayeotesha ni Mungu na hivyo kazi ya wahudumu hao ni kuvuna ili mavuno yasiharibike shambani, huku akiwaasa wavune kwa uaminifu na uangalifu.
“Kazi yenu siyo kustarehe au kungojea mambo mengine. Siyo kuchumia mifukoni. Ni kufanya mlichoitiwa yaani kufundisha. Kufundisha ndiyo kazi aliyoifanya Yesu kwa muda mrefu, watu wanapokosa mafundisho upotoshaji hutokea. Ndipo wanaanguka kwa kukosa mafundisho sahihi” amesisita.
Aidha amewataka mashemasi hao kwenda kuponya magonjwa ambayo ni mengi hasa magonjwa ya kimahusiano, kifikra, huzuni na udhaifu, kwa kuwa watu wanapokosa maarifa wanaishi maisha duni, kwa hasara, wanatoka jasho lakini hawaendelei. Amewasihi wawaangazie watu kwa mwanga wa Injili ili wapate uhuru wa fikra na wamwabudu Mungu katika kweli na roho.
“Haujaitwa ili uishi maisha ya starehe, kubembelezwa au kuhongwa. Mmeitwa mdumu katika ukweli mliofundishwa tangu mlipopokea komunio ya kwanza, na daima Maandiko Matakatifu yawe chakula chako na kuwalisha wengine. Fundisheni ukweli ili watu waijue njia sahihi ya kumwelekea Mungu na kuwaelekea watu” amesema Askofu Amani.
Vile vile Askofu Amani amewakumbusha viongozi wa dini kutosheka na maisha ya kawaida, kwa kushika na kuishi viapo vyao. Amesema kuwa utajiri wa kupindukia kamwe hawataupata katika wito wa upadri, huku akiwakumbusha kutoyumbishwa na utandawazi na malimwengu.
“Hakuna mseja anayezaa mtoto. Unapofanya mambo ya ajabu kwa makusudi, yaani unavua kanzu na kuvaa tai, siyo shetani wala bahati mbaya bali unakuwa ni ujinga. Ishini viapo vyenu. Malimwengu na utandawazi yanabeza maisha ya sadaka. Maisha ya fadhila ndiyo ya maana. Ushindi haupatikani kwa kutawaliwa na mali wala mwili na ubinafsi” amesema.
Wakati huo huo Askofu Amani amesema kuwa Kanisa Katoliki linaposherehekea Yubilei ya miaka 150 ya Uinjilishaji Tanzania Bara linamshukuru Mungu kwani mwanga wa Injili umedhihirika katika Taifa hasa kwa namna Kanisa linavyojitoa kuhudumia wananchi katika sekta za afya, elimu na huduma nyingine za jamii.
Amewaasa waamini kuwa na fikra za kimisionari kwa kuwa na ari na moyo wa kupeleka Injili pale ambapo bado haijafika, kwa kushiriki katika michango ya uinjilishaji. Pia amewaasa waendelee kuziombea familia zao ili zichipushe miito mitakatifu ya ndoa, upadri na utawa, huku akiwashukuru wazazi wa mashemasi hao kwa kuwatoa watoto wao ili walihudumie kanisa.
Mashemasi waliopewa daraja hilo ni Shemasi Honest Ndeonakazi, Shemasi Novatus Babu, Shemasi Benedikto Kagwa, Shemasi Antony Amani na Shemasi Emaueli Imani. Wengine ni Shemasi Cleofasi Kimaro na Shemasi Dismasi Bahati.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI