Kanisa kujitoa rasmi kuchukua Hospitali ya Rufaa Kwangwa Musoma
Modest
na Bertha Mayayi Musoma.
Imeelezwa
kuwa kukosekana kwa hati miliki, thamani kubwa ya fidia, pamoja na kukosekana
kwa wahisani wa ufadhili zimetajwa kuwa ni miongoni mwa sababu zilizosababisha
Kanisa Jimbo Katoliki Musoma kujitoa rasmi kimaandishi juu ya ombi la kuchukua
na kuendeleza Hospitali ya Rufaa Kwangwa ambayo kwa sasa inasimamiwa na
serikali.
Hayo yamebainishwa na Askofu wa jimbo hilo Mhashamu Michael
Msonganzila hivi karibuni wakati akichangia hoja katika kikao cha kamati ya
ushauri ya Mkoa wa Mara (RCC) ambapo alikieleza kikao kuwa maazimio mengi ya
kikao hicho kuhusu Kanisa kuendelea na ujenzi wa Hospital hiyo,
yameshawasilishwa kwa maandishi katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.
Askofu Msonganzila amesema kuwa, Kanisa lilifuatilia
vielelezo muhimu vya umiliki halali wa hospitali hiyo ya rufaa kwa muda wa
miaka miwili bila mafanikio yeyote ikiwa ni pamoja na kukosekana kwa hati
miliki ya eneo husika kama ilivyoahidiwa na kutolewa January 20 mwaka 2008.
Pia baada ya kufahamika kuwa Kanisa Katoliki linachukua na
kuendeleza hospitali hiyo walijitokeza watu wengi wanaodai fidia yenye thamani
ya shilingi milioni thelathini na nane jambo ambalo Kanisa halikuelewa.
“Tulijiuliza ni kwa nini madai hayo ya fidia yanakuja
tena yenye gharama kubwa hivyo? Je, ni kwa sababu ya Kanisa Katoliki
kuchukua eneo au laa! Nalo halikupata majibu na mbali zaidi Kanisa lilifanya
jitihada za kupata wahisani wa kufadhili upatikanaji wa fedha zilizohitajika
kwa wakati huo lakini lilikwama,”amesema Askofu Msonganzila.
Hata hivyo Kanisa limepokea barua kutoka katika ofisi
ya Mkoa iliyotoa muda wa miezi sita vinginevyo serikali ichukue eneo lake ndipo
Kanisa kupitia kikao hichohicho cha kamati ya ushauri, likaridhia kujitoa rasmi
kimaandishi kati yamwaka 2010 na mwaka 2011.
Akizungumzia mchango wa Kanisa kwa Serikali katika utoaji
huduma za jamii, Askofu Msonganzila amesema jitihada za kanisa Katoliki
zimeonekana tangu mwaka 1911 ambapo limejenga makanisa, vituo vya
afya na shule ambazo baadaye zilitaifishwa na Serikali takribani shule kumi na
sita na hivyo Kanisa kukosa chochote, ingawa halikukata tamaa na kwamba
mpaka sasa jimbo la Musoma lina shule kumi zinazomilikiwa na Kanisa kwa
ajili ya kusaidia jamii si tu kwa kufundisha bali hata kimalezi pamoja na kiimani.
Aidha amesema Kanisa pia linatetea haki za binadamu na
amani ya mtu mmoja mmoja hususani akina mama na watoto wa kike ili
wasinyanyaswena kutendewa ukatili kwa kuwatunza na kuwalea katika vituo vya
Masanga, Rogolo na kituo cha Terminal Female Genital Multilation (TFGM) ambao
wamekimbia mila potofu ya ukeketaji.
Hata hivyo ameeleza chamgamoto kubwa kuwa ni baadhi ya
wazazi kupinga hatua hiyo lakini Kanisa halijakata tamaa na badala yake
litakuwa na uvumilivu wa hali ya juu dhidi ya mapambano hayo.
Kanisa halivumilii ukatili huo hivyo litamkeketa mtoto wa
kike kielimu na kumuandaa kiakili aweze kuwa na nafasi kubwa kwa jamii ya
kutwaa madaraka si ya kimila pekee bali madaraka ya taifa na ulimwengu mzima.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mara ambaye ndiye mwenyekiti
wa kikao hicho Adam Malima amewataka wajumbe wa kikao hicho kujadili namna ya
kukamilisha ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kwangwa ambayo imeshindwa
kukamilika kwa muda wa zaidi ya miaka hamsini sasa.
Comments
Post a Comment