Ujumbe wa Papa Fransisko Siku ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani 2018

BABA Mtakatifu Fransisko katika ujumbe wake kwa Siku ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani kwa Mwaka 2018 inayoadhimishwa Januari 14, 2018 anakazia kwa namna ya pekee umuhimu wa “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayoakirimia. 
Tangu mwanzo wa utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, ameguswa sana na matatizo na changamoto zinazowakabili wakimbizi na wahamiaji sehemu mbali mbali za dunia. Hawa ni watu wanaokimbia vita, dhuluma, manyanyaso, majanga asilia na umasikini. 
Katika mchakato wa kukabiliana na changamoto hizi, Baba Mtakatifu Fransisko ameanzisha kitengo maalum cha wakimbizi na wahamiaji katika Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya binadamu ambacho kinawajibika moja kwa moja kwake kama kielelezo makini cha huduma ya mshikamano wa Kanisa na wakimbizi, wahamiaji, watu wasiokuwa na makazi pamoja na waathirika wa biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo. 
Huduma kwa wakimbizi na wahamiaji wanaobisha hodi kwenye malango ya watu mbali mbali duniani, ni nafasi muhimu sana ya kuweza kukutana na Kristo Yesu, ambaye anajitambulisha kama mkimbizi na mhamiaji anayekataliwa na kubezwa na watu wa nyakati mbali mbali.
Mama Kanisa anapenda kuwaonesha upendo wake wa dhati, wakimbizi na wahamiaji, katika hatua mbali mbali za safari yao, tangu wanapoondoka, wanapofika na hatimaye, kurejea tena makwao hali inaporuhusu. Waamini wakishirikiana na watu wote wenye mapenzi mema, wanaalikwa kuyavalia njuga matatizo na changamoto zinazowakabili wakimbizi na wahamiaji kwa kuwaonesha moyo wa ukarimu, hekima na busara kila mmoja kadiri ya uwezo na nafasi yake. 
Lakini, wote kwa pamoja wanaweza kujibu changamoto hizi kwa kujikita katika mchakato unaofumbatwa katika mambo makuu yafuatayo: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji”.
Baba Mtakatifu anafafanua kwamba, Kuwapokea maana yake ni kutoa fursa kwa wakimbizi na wahamiaji kuingia katika nchi husika kwa njia salama zinazozingatia sheria za nchi; kwa kutoa hati za kusafiria na kuwapatia wakimbizi na wahamiaji nafasi ya kuweza kukutana na kujiunga tena na familia zao. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, Jumuiya na Mashirika mbali mbali yatasaidia kutoa msaada wa kiutu kwa ajili ya wakimbizi na wahamiaji wanaokabiliwa na hali tete zaidi. 
Watu wanaokimbia vita, nyanyaso na uvunjifu wa haki msingi, utu na heshima ya binadamu, waangaliwe kwa jicho la huruma kwa kupewa hati za muda na huduma makini kadiri ya utu na heshima yao kama binadamu, ili kutoa nafasi kwa watu hawa kukutana na wenyeji wao, ili hatimaye, kuboresha huduma, daima usalama na utu wa mtu, ukipewa kipaumbele cha kwanza kabla hata ya kuangalia usalama wa taifa, sanjari na kuvifunda vyema vikosi vya ulinzi na usalama kwenye mipaka ya nchi. 
Wakimbizi, wahamiaji na watu wanaotafuta hifadhi ya kisiasa, hawana budi kuhakikishiwa usalama na huduma msingi, kwa kuheshimu utu wao kama binadamu na kuondokana kabisa na mtindo wa kuwaweka kizuizini wakimbizi na wahamiaji wasiokuwa na nyaraka za kusafiria.
Baba Mtakatifu anasema, Kuwalinda maana yake ni kuhakikisha kwamba haki zao msingi, utu na heshima yao kama binadamu zinalindwa na kudumishwa, kwa kupatiwa huduma ya faraja; kwa kulinda na kutunza nyaraka na utambulisho wao; kwa kupatia fursa za haki, nafasi ya kuweka kufungua akaunti ya fedha benki pamoja na huduma makini ya maisha; kwani kwa hakika, wakimbizi, wahamiaji na watu wanaotafuta hifadhi ya kisiasa ni hazina na amana kwa jamii inayowapokea na kuwapatia hifadhi. 
Kumbe, utu na heshima yao, uhuru wa kutembea, uwezekano wa kupata fursa za ajira na mawasiliano ni mambo ambayo wanapaswa kupewa. Kwa wale wanaotaka kurejea makwao, basi, kuwepo na huduma itakayowawezesha kuingizwa katika mfumo wa kazi na jamii katika ujumla wake. Itifaki za kimataifa kuhusu haki za watoto wakimbizi na wahamiaji hazina budi kufuatwa na kuzingatiwa kikamilifu, kwa kupewa elimu ya msingi na sekondari na kamwe wasiwekwe vizuizini. 
Watoto wasioongozana na wazazi na walezi wao, wapewe ulinzi na usalama wa kutosha; wahakikishiwe haki zao msingi kwa kuzingatia sheria za kimataifa. Wakimbizi na wahamiaji wapewe nafasi ya kupata huduma ya afya ya jamii, waingizwe kwenye mfumo wa pensheni na uwezekano wa kuhamisha mafao yao pale wanaporejea makwao!
Baba Mtakatifu anafanua kwama, Kuwaendeleza wakimbizi na wahamiaji maana yake ni kuhakikisha kwamba, Jumuiya inayowapokea na kuwakirimia inawapatia fursa ya kujiendeleza katika utimilifu wao kama binadamu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Wapewe uhuru wa kuabudu na kuungama imani yao; fursa za kazi na ajira; nafasi ya kujifunza lugha na tamaduni za watu mahalia, ili kweli waweze kushiriki kikamilifu katika maisha ya Jamii inayowahifadhi. 
Watoto wadogo walindwe dhidi ya kazi za suluba zinazoweza kuwapoka utu na heshima yao kwa kuwadumaza! Wakimbizi na wahamiaji wapewe fursa ya kuungana tena na wanafamilia wao bila ya kuweka uchumi kuwa kikwazo kikuu kinachowatenganisha. Jumuiya ya Kimataifa ishirikiane katika kuwahudumia na kuwatunza wakimbizi na wahamiaji.
Baba Mtakatifu anasema, Kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji ni kuhakikisha kwamba, hata katika mwingiliano wa tamaduni, mila na desturi, bado wakimbizi na wahamiaji watabakia na utambulisho wao, lakini wajenge madaraja ya kufahamiana na kuheshimiana, ili kujenga watu wa mila na tamaduni mbali mbali, zawadi ya Mwenyezi Mungu kwa binadamu. 
Mchakato huu unaweza kuendelezwa kwa haraka kwa kutoa vibali vya uraia na vibali vya kuishi kwa muda mrefu, daima utamaduni wa watu kukutana, kufahamiana na kusaidiana ukipewa kipaumbele cha kwanza, ili kujenga mchakato wa kuwahusisha na kuwashirikisha wakimbizi na wahamiaji katika uhalisia wa maisha ya jamii inayowahifadhi. 
Kwa wakimbizi na wahamiaji wanaolazimika kuzikimbia nchi zao, wapewe huduma makini wanaporejeshwa makwao, ili waweze kupata tena fursa za kazi nchini mwao. Mama Kanisa kama sehemu ya Mapokeo na Utamaduni wake, yuko tayari kuhakikisha kwamba, mapendekezo yote yaliyotolewa katika Ujumbe huu yanamwilishwa. Ili kuweza kupata mafanikio yanayokusudiwa, kuna haja kwa wanasiasa pamoja na viongozi wa kijamii, kuhakikisha kwamba, kila upande, unatekeleza dhamana na wajibu wake kikamilifu!
Baba Mtakatifu Fransisko katika ujumbe wake kwa Siku ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani kwa Mwaka 2018 anakumbushia kwamba, mwaka 2016, Viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa waliamua kuivalia njuga changamoto ya wakimbizi na wahamiaji duniani, kwa kuokoa maisha yao, kwa kulinda na kudumisha haki zao msingi pamoja na kushirikishana wajibu katika ngazi ya kimataifa. 
Nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa zimeamua kutekeleza kwa dhati ifikapo mwishoni mwa Mwaka 2018 Mikataba ya Kimataifa “Global Compacts” kwa ajili ya wakimbizi na wahamiaji. Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, wanawashirikisha kikamilifu wanasiasa na viongozi wa kijamii ili kuhakikisha kwamba, Mikataba hii ya Kimataifa inapitishwa. 
Mwishoni, Baba Mtakatifu Fransisko anapenda kuwaweka wakimbizi na wahamiaji wote chini ya ulinzi wa Bikira Maria, ili aweze kuyapokea na kusikiliza matumaini ya wakimbizi, wahamiaji pamoja na jumuiya zinazotoa hifadhi kujifunza kumwilisha ndani mwao huduma ya upendo kwa wakimbizi na wahamiaji kama wanavyojipenda wao wenyewe.


Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI