Papa Francisko: Jengeni mshikamano wa upendo dhidi ya ubinafsi
Fumbo la Umwilisho limemwezesha Mwenyezi Mungu kuingia katika historia na maisha ya binadamu, Kristo Yesu, Neno wa Mungu aliyetwaa mwili ni kiini cha Habari Njema ya Wokovu. Mwenyezi Mungu anapenda kukaa pamoja na watu wake, hali inayojionesha katika uhalisia wa maisha ya kila siku. Watu wa Mungu wanapokuwa kazini, wanapojihusisha na malezi na majiundo ya watoto wao na wanapokuwa wakishiriki katika ujenzi mbali mbali wa jamii zao. Lakini hata katika mazingira kama haya, bado Mwenyezi Mungu anawaita waja wake ili kutoka kifua mbele kutangaza na kushuhudia wema na huruma ya Mungu kwa waja wake.
Kama ilivyokuwa awali kwa Yona, aliitwa, akatumwa, lakini alikataa, akajificha na kutoka katika uso wa Mungu. Yona anasema, alikuwa na sababu msingi za kutokubali mwaliko wa kwenda Ninawi ili kutangaza Habari Njema ya Wokovu. Sababu kubwa hapa ni kiwango cha maendeleo, kwani kuna watu ambao wamebahatika kuwa na kiwango cha juu cha maendeleo, lakini pia kuna umati mkubwa watu wanaoogelea katika umaskini na ukosefu wa maendeleo, hawa ndio wale wanaoambulia makombo ya maendeleo ya binadamu!
Ni watu wanaoishi katika mazingira tete, bila hata ya kupata mahitaji msingi katika maisha, hali inayodhalilisha utu na heshima yao kama binadamu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Huko ndiko mahali pa kukutania na watoto pamoja na vijana wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi. Ili kuweza kukabiliana na changamoto kama hizi zinazojionesha katika miji mingi nchini Perù, kuna haja ya kujenga na kudumisha utamaduni wa watu kukutana, kushikamana na kusaidiana ili kuondokana na tabia ya watu kukimbia miji yao na kukosa amani ya ndani. Watu wajenge utamaduni wa kusikilizana ili kuonja shida na magumu ya jirani zao pasi na kuwageuzia kisogo. Jamii isimame kidete kulinda na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo, kwa kuwakubali na kuwapokea wagonjwa kama sehemu ya amana na maisha ya binadamu; badala ya kuwaonjesha ukatili na vitendo ambavyo vinakwenda kinyume cha utu na heshima ya binadamu.
Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili ya tatu ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa, huko Jimbo kuu la Lima, nchini Perù, tarehe 21 Januari 2018, wakati wa hija yake ya kitume nchini humo. Baada ya Yohane Mbatizaji kukamatwa na kutiwa gerezani, Kristo Yesu, alianza maisha na utume wake wa hadhara kwa kutangaza toba, wongofu wa ndani na kuiamini Injili, chemchemi ya matumaini ya uwepo wa Ufalme wa Mungu karibu na kati yao. Huu ukawa ni mwanzo wa furaha ya Injili kwa Mitume wa Yesu na watakatifu wengine wote waliofuatia hapo baadaye, wakajikita katika mchakato wa ujenzi wa utandawazi unaosimikwa katika mshikamano wa upendo, dhidi ya utamaduni usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine, kwani upendo wa Mungu unawawajibisha Wakristo! Huu ni upendo unaopaswa kutolewa kwa Mwenyezi Mungu pamoja na jirani, mwaliko wa kujenga na kudumisha umoja na mafungamano mapya kwa ajili ya maisha ya uzima wa milele.
Yesu akiwa amefuatana na mitume wake aligundua jinsi watu walivyokuwa wametengwa, wakaathirika kwa saratani ya rushwa, iliyokuwa inatishia pia matumaini ya watu wa Mungu. Yesu akawataka watu kutubu, kumwngokea Mungu na kuiamini Injili kama njia ya kukutana na Mwenyezi Mungu katika hija ya maisha yao, kwani hata wao ni sehemu muhimu sana ya historia ya wokovu. Hata leo hii, Yesu anaendelea kutembea katika miji na vijiji vya watu wa Mataifa, ili kuwasha moto wa matumaini, ili kujenga na kudumisha udugu, mshikamano, haki na amani. Anaendelea kuwaita watu na kuwapaka mafuta ili kutangaza na kushuhudia Injili ya amani na matumaini yanayopyaisha mwono wa watu. Yesu anaendelea kuamsha dhamiri ili kuondokana na mahusiano yasiyokuwa na mvuto wala mashiko, ili kuwatangazia watu Injili ya matumaini ili vipofu waweze kuona, waliopooza wapate kupona, wakoma watakaswe na visiwi wapate kusikia tena na kuonja ufufuko wa wafu! Baba Mtakatifu anaitaka familia ya Mungu nchini Perù kuwa ni chombo na wakala matumaini, unabii, matumaini na ushuhuda. Yesu anawaita wananchi wa Perù kuambatana naye katika mitaa yao ili kuwatangazia watu Injili ya furaha kwani Mwenyezi Mungu yu pamoja nao!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Vatican News!
Comments
Post a Comment