Elimu ya mazingira ianzie kwenye elimu ya awali

DHAMIRA ya elimu ya mazingira ni kujenga ulimwengu wa watu ambao wanaelewa na kujali mazingira na matatizo yanayohusiana nayo na wenye maarifa, stadi, ari na msimamo wa kujituma mmojammoja au kwa pamoja katika kutafuta ufumbuzi wa matatizo yaliyopo na katika kuzuia matatizo mengine yasitokee.
Uelewa huo wa kujali mazingira utajengwa na kizazi mahalia wala si mikutano ya kimataifa.
Mtoto anayeanza elimu ya awali akifundishwa namna ya kuthamini mazingira akili yake inakuwa kwa mantiki hiyohiyo.
Akifundishwa umuhimu wa kupanda miti, kupanda maua, kulinda vyanzo vya maji, kusafisha makazi yake nk. akiwa mtu mzima jamii haitatumia nguvu kumuhamasisha juu ya hayo.
Elimu ya mazingira iwepo katika mitaala ya elimu ya awali, msingi, sekondari na vyuo kama tunataka kupambana na janga hili.
Sera ya Taifa juu ya elimu ya mazingira Mwaka 1995 ilitoa utaratibu juu ya sera ya mazingira shuleni na ulianzishwa kama Sera ya Taifa kufuatia kuongezeka kwa uharibifu wa mazingira nchini na pia kutokana na uelewa mdogo katika kukabiliana na hali hiyo. Mwongozo ulitolewa na Wizara ya Elimu na Utamaduni mwaka 2005 kama sehemu ya mkakati wa kuhakikisha walimu kuingiza katika mada zao elimu za mazingira ili kumhamasisha mwanafunzi aweze kuhusisha anachofundishwa darasani na mazingira yake nje ya shule katika jamii. 
Kujenga ufahamu wa mwanafunzi kimazingira; uzuri na ugumu wa mazingira, na madhara ya shughuli za kibinadamu katika mazingira. 
Kuhakikisha mwanafunzi anaelewa mambo mahususi ya kimazingira katika eneo mahalia. 
Serikali iweke mikakati ya kutoa elimu ya mazingira katika vyuo vya ualimu kwa ngazi zote ili wawajengee uwezo na ufahamu wa mazingira katika upana wake.
Jinsi elimu ya sayansi na hisabati vinavyokazaniwa katika elimu ya awali na msingi vivyo hivyo mazingira. Kumbe lazima wawepo walimu wa mazingira walioandaliwa na lazima wajengewe njia bunifu za kufundishia elimu ya mazingira. 
 Ni rahisi sana kufundisha watoto wadogo elimu ya mazingira kwani wanafaa kupewa elimu kwa vitendo.
Wataalamu watunge ngonjera, maigizo, nyimbo, ngoma za utamaduni zinazohusiana na mazingira, hadithi nk.
Wafundishwe kupanda miti kwanza kutengeneza vitalu vya miti shuleni, kuvitunza na kuotesha miti.
Mtoto akuwe na hoja hii kwamba kukata mti ama kuharibu hata tawi la mti ni dhambi na ni kitendo ambacho hakikubaliwi na jamii.
Mtoto anapaswa kujuwa namna ya kutengeneza bustani, kuchimba shimo la taka nyumbani, kufundishwa kuwa kutupa taka hovyo ni kosa. Ajuwe changamoto za mazingira na namna ya kutatua.
Aanze tangu uchanga wake kusoma alama za nyakati kutokana na hali ya hewa ili amudu mazingira yake.
Maisha ya kila mmoja wetu yanategemea mazingira yetu. Ili tuweze kutunza mazingira yetu tunatakiwa kuyaelewa. 
Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania TFCG ni shirika lisilo la kiserikali ambalo ujumbe wake ni kuhifadhi na kurudisha bioanuwai ya misitu muhimu kidunia ya Tanzania kwa faida ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.
Samaki mkunje angali mbichi.


Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI