WITO umetolewa kwa Wakristo wakatoliki
nchini kutobaguana kutokana na vyama vya kitume na badala
yake wamealikwa kumtumia Mama Bikira Maria kama daraja kufikisha
maombi na sala zao
kwa Mwenyezi Mungu.
Akizungumza
katika ibada ya misa takatifu ya hitimisho la Mahujaji wa utume wa
Fatima wa jimbo la Mbeya, Njombe na Tunduru Masasi iliyofanyika katika
Kanisa la Mtakatifu Izidori Mkulima, Parokia ya Izuo, Mkurugenzi wa
Utume wa Walei, jimboni Mbeya, na vyama vya Mashirika na
jumuiya za kitume jimbo, Padri Sirilo Mwalyoyo amewataka wakaristo
kumtumia Mama Bikira Maria kufikisha maombi yao kwa Mungu ili
wapate kusamehewa.
Padri
Mwalyoyo ambaye pia ni Mratibu wa Idara ya Uchungaji Jimbo Katoliki
Mbeya amewaalika mahujaji wasiache kusali rozali kwani kwa imani ya
Kanisa na kupitia mafundisho yake na mapokeo yanawafanya wapate
ufunuo kamili kujuwa Mungu ni nani.
“Kipindi
cha likizo za kufungwa shule ndipo ada za semista zinahitajika
na ndiyo kipindi ambacho baba akimuona mtoto anakunja sura anajuwa
muda wa maombi ya ada umewadia na hivyo watoto wanawatumia mama zao
waweze kufikisha ujumbe kwa baba kwa sababu wanajuwa kabisa mama anajuwa mbinu
za kumuingia baba, atamuandalia chakula na vipande vizuri vya kuku na maneno
mazuri na ndipo Mama anaingizia ombi la ada, na ndivyo ilivyo
hata kwa Mama Maria,” amesema Mkurugenzi huyo huku akishangiliwa na Mahujaji.
Ameongeza,”Na
sisi tunamuogopa Mwenyezi Mungu kwa sababu ya dhambi zetu hivyo, kupitia
kwa Mama Bikira Maria atafikisha maombi yetu ya kusamehewa dhambi, katika
maandiko tunasoma kuwa Yohane mbatizaji alisema anakuja mkubwa kuliko mimi naye
ni Kristo bwana na Malaika waliwaambia wachungaji
tumewaletea habari njema amezaliwa mwokozi ambaye ni Kristo na tunaona
pale msalabani Yesu alimwambia Maria mtazame Yohane huyu ndiye
mwanao na wewe Yohane huyu ndiye Mama yako na Yohane pale pale
alimchukuwa Mama Bikira Maria kwenda nyumbani kwake.”
“Hivyo
nawaombeni sanamu ya Bikira Maria inayotembea na kupitishwa na Radio
Maria muipokee kwa shangwe, muikimbilie na msiikimbie kwa sababu mkiikimbia
mtaikuta huko mnakokimbilia na pendaneni muwe wa utume wa
moyo mtakatifu wa Yesu, utume wa Francisco wasaikulari, wakarismatiki, utume wa
Fatima, Legio Maria,Wanafrancisco, Kwaya au vijana ninyi nyote ni kiungo
kumbukeni Yesu alisema mwili wake una viungo vingi lakini kichwa ni
kimoja ambacho ni yeye mwenyewe, kumbukeni ninyi nyote ni viungo katika mwili
wa Kristo, hakuna anayemzidi mwenzake,”amesisitiza Mkurugenzi na Mratibu huyo.
Akizungumza
wakati wa kumuomba Mkurugenzi Padri Mwalyoyo kutunuku hati maalum kwa
mahujaji, Mwenyekiti wa utume wa Fatima Jimbo la Mbeya,Venance Ntakabile
amemshukuru Mhashamu Askofu Evarist Chengula wa Jimbo Katoliki Mbeya ambaye ni
Rais wa Utume wa Fatima ulimwenguni nchini Tanzania kwa ufunguzi wa ibada
ya misa takatifu ya Hija na yote aliyowaasa watayazingatia na
yataendelea kuwaimarisha.
Mwenyekiti
huyo ametaja masista walioshiriki Hija hiyo kuwa ni watatu na mapadri
sita ambapo amesema Hija ya mwaka huu imetia fora
kutokana na kushiriki mahujaji 485 kutoka Parokia 35 kati ya
Parokia 45 za Jimbo Katoliki Mbeya wakiwemo na mahujaji
watano kutoka majimbo jirani ya Tunduru Masasi na Njombe.
Ntakabile amesema
katika Hija iliyofanyika mwaka 2016 katika Parokia ya Bara, mkoani
Songwe jumla ya mahujaji 344 walishiriki ambapo pia amemshukuru
Mungu kwamba hakuna mahujaji walioumia na wote wamehitimisha salama.
KIONGOZI
imezungumza na Mahujaji kwa nyakati tofauti kupata maoni yao
kuhusu Hija hiyo ambapo Mzee Elia Mwanjale kutoka Kata ya Kisondela,
Parokia ya Kisa,Wilaya ya Rungwe, amesema wamepata semina ambayo
imewaimarisha kiroho na kiimani.
“Tumejifunza
na kukumbushwa kuwa wanyenyekevu,wapole,wenye huruma, upendo kwa watu
wote na tumeamka salama na na tunamshukuru Mungu kwa
kuhitimisha Hija salama na tunaahidi kwenda kuwa chachu
ya matendo mema katika nyumba zetu,” amesema kwa furaha.
Mama
Mangasila, kutoka Parokia ya Mwambani, wilaya ya Songwe, mkoani Songwe amesema
kupitia Hija amekuwa shuhuda mzuri wa kutofikiwa na homa
nyumbani kwake na amekuwa akiyapata mafanikio ya kupata
vyakula na mahitaji muhimu kwake na familia yake anayoishi nayo ambao ni
wajukuu huku mahujaji wengine kutoka parokia hiyo
Teodora Mwatowine na Neema Ndolomi wamesema
wamejifunza mengi kuhusu ukatoliki na wamewaomba vijana wajiunge
katika vyama vya kitume waweze kunufaika.
“Na
kupitia maigizo ya njia ya msalaba imetumkumbusha kuwa
Yesu alikufa msalabani kwa ajili ya mateso yao hivyo tusitende
dhambi na kupitia mahubiri ya Mapadri inaendelea kutujenga katika
kutafuta utakatifu wa Mungu,”wamesema.
Enita
Nyondo kutokea Jumuiya ya MtakatifuTerezia, Kigango cha Isongole Parokia
ya Itumba, na Marietha Kamwela kutoka Jumuiya ya Mtakatifu Paulo Wilaya
ya Ileje, mkoani Songwe wamesema wamejifunza mengi katika Hija ya
mwaka huu.
“Hakika
Hija imezaa matunda, na wengine wafike katika Hija nyingine tukipata
uzima na tunawaomba waume zetu kushiriki katika Hija nyingine
panapo majaliwa na tunakwenda kuwahamasisha na pia
tumejifunza mahusiano ya Mama Bikira Maria na mwanae Yesu,”wamefafanua.
Wamesema kuwa kuwa katika hija
hiyo mahujaji waliofika na waume zao wamejifunza mengi hivyo
wamemuomba mungu na Mama Bikira Maria ili aweze kuwasaidia katika hija
nyingine wakawashawishi waume zao kushiriki na kuweza
kuimarisha kupitia salama,mafungo,maungamo na mafundisho.
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa Utume wa Fatima Parokia ya Mbeya, Josephine Kamunga
kutoka Jumuiya kuu ya Mtakatifu Yuda Tadhei,Sisimba jijini Mbeya amesema
Mama Bikira ameendelea kumtendea miujiza mingi ya mafanikio katika maisha
yake na kwamba kwa kasi ya ajabu katika hija hiyo
wamevuna samaki wengi (wanachama) na anaamini kwamba baada ya miaka
mitatu wanaweza kufikia wanautume zaidi ya 1000 huku akiahidi kuendelea
kumtangaza Mama Bikira Maria ndani na nje ya jimbo na nchi kwa
ujumla.
Kutoka
Jimbo la Njombe, Parokia ya Matamba, Alubina Mushi ambaye pia ni
mjumbe wa Utume wa Fatima Taifa amesema licha ya kupata neema
nyingi kupitia Hija hiyo lakini wamejifunza kutoka jimboni na kuwa katika
Hija ya Jimbo Mbeya kuna mahujaji na wana utume
wengi wakiwemo vijana na wanaume na hivyo majimbo
mengine wanapaswa kuiga na kusema mkristo asiyeingia
katika vyama vya kitume ni sawa na kuingia katika shamba lisilo na
mbolea.
Kutoka
Jimbo Katoliki Tunduru Masasi, Parokia ya Makulani hujaji Mutali Maria
amemshukuru Paroko wake Mwenisawa kumuhamasisha kufika kujifunza
kuhusu utume wa Fatima na Hija na hakika wamevuna mengi
Katibu
Mtendaji wa Utume wa Fatima Taifa, Sr.Cecilia Ntongoro amewaomba
mahujaji kuwa mbegu waliyoipanda iendelee kustawi ndani ya mioyo yao
na kuwakaribisha katika Hija kitaifa itakayohusisha mahujaji kutoka
nchi za jirani Oktoba,10 hadi 13 mwaka huu itakayofanyika jimboni Mbeya
ili iendelee kustawisha roho zao
Sr.Cecilia
ambaye pia ni Katibu wa Utume wa Fatima kwa Nchi za Kanda ya
Afrika amewaalika wakristo wote kushiriki Hija ya
kiulimwengu itakayohusisha Mahujaji wa Nchi za Bara la Afrika na
Ulaya inayotarajiwa kufanyika mwaka 2018 nchini Tanzania katika jimboni Mbeya.
Aidha akitoa shukrani kwa mahujaji,
Paroko wa Parokia ya Izuo, Padri Jeremiah Majengo amewashukuru viongozi wa
Utume wa Fatima Jimbo kwa kupita vigangoni kuelimisha juu ya
ukatoliki ambapo amesema Baba Askofu Chengula alitoa
Sakramenti ya Kipaimara kwa wakristo 25, sakramenti ya Ekaristi
Takatifu kwa waumini 48,wamebatizwa wakristo 52, pamoja na
kubariki ndoa.
Comments
Post a Comment