“Mkakati wa miaka 100 utanusuru mazingira” TEC
Katibu Mkuu
wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Padri Raymond Saba amewataka viongozi
wa serikali na umma nchini kushirikiana na wadau katika kupanga mikakati ya
miaka 100 ya utunzaji wa mazingira na siyo kuweka mikakati ya miaka mitano au
kumi.
Padri Saba
amesema kuwa kinachochangia kuendelea kuharibika kwa mazingira ni kutokana na serikali kuweka mikakati ya
mazingira ya miaka mitano mitano badala ya kuweka mikakati ya miaka 100, ambayo
inadumu na kutekelezwa kwa muda mrefu.
Katibu
Mkuu huyo ameyasema hayo wakati wa Kongamano la mazingira kwenye maadhimisho ya
Siku ya mazingira kitaifa yaliyofanyika wilayani Butiama mkoani Mara kuanzia
Juni Mosi hadi 4 mwaka huu, alipokuwa akizungumzia nafasi ya imani ya dini
katika kuhifadhi mazingira.
Padri Saba
amebainisha kuwa suala la mikakati ya miaka 100 litaweza kusaidia katika
kuboresha usimamizi mzuri wa uoto wa asili na utunzaji wa mazingira, kwa kuwa
kila kiongozi anayeingia madarakani
anaingia na sera yake, ambayo anaitekeleza kwa muda wa utawala wake yaani
miaka mitano au kumi tu, na akishaondoka sera ile inakuwa haitumiki tena,
lakini mikakati ya muda mrefu ikiwekwa itaboresha hali ya mazingira.
Aidha
padri Saba ameshauri kuwa ili kuweka msisitizo mkali juu ya umuhimu wa utunzaji
wa mazingira na uoto wa asili kwa ujumla ni vyema somo la mazingira liwepo
kwenye mitaala ya elimu kuanzia shule ya awali hadi ngazi za juu, na
kuwashirikisha wadau mbalimbali, ili
hata mwanafunzi awe na ufahamu mzuri juu ya suala zima la utunzaji wa
mazingira, katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi tangu akiwa mdogo.
“Kama
kungekuwepo na mikakati ya mazingira ya
miaka 100 tungeweza kufaulu, lakini sera
ya miaka mitano haitekelezeki na ndio maana tumefika hapa tulipo, na
tusiongelee mabadiliko ya tabia nchi bali tuongelee tabia za watu, na tukiamua
na tukashirikiana kwa pamoja kuanzia
elimu ya awali pamoja na wadau wa mazingira tutafaulu kutunza mazingira, kwani
Kanisa tumekuwa tukijitahidi kushauri
watu wabadilike, na inawezekana kabisa watu kubadilika na mazingira yetu
yakabaki na uoto wake wa asili,” Amesema Padri Saba.
Wakichangia
mjadala huo wa nafasi ya imani ya dini
katika kuhifadhi mazingira, wadau mbalimbali wa mazingira wamesema kuwa
bado viongozi wa dini hawajafanikiwa sana kwa kuwa binadamu amekuwa mharibifu
wa kwanza wa mazingira na wao hawajawashauri waamini kupanda miti ili
kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi .
Wadau hao
wamesema kuwa hata katika uumbaji Mungu aliumba kila kitu na mwanadamu
alikabidhiwa mazingira yakiwa safi bila uharibifu wowote, lakini ndiye amekuwa kwa kwanza kuharibu ambapo
waliwaomba viongozi wa dini kusimama na kukemea uharibifu huo, kwani hata
madhara ya mabadiliko ya tabia nchi yanayotokea sasa ni kutokana na mwanadamu
kuharibu mazingira.
Patrick
Kihoza kutoka Chuo kikuu cha Mzumbe amesema kuwa viongozi wa dini wana nafasi nzuri ya kuonya
juu ya uharibifu wa mazingira kama wataamua kwa pamoja kulisimamia, kwa kuwa
kila jambo linapoonekana kuwa gumu viongozi wa dini wamekuwa wakilifanya kuwa
jepesi kwa kuwaasa waamini wao makanisani na misikitini juu ya madhara ya
uharibifu wa mazingira na matokeo yake yamekuwa yakionekana, hivyo amewaomba
kusimama na kukemea suala la uharibifu wa mazingira ili kukabiliana na
changamoto ya mabadiliko ya tabia nchi.
Comments
Post a Comment