WATAWA WAEPUKE UBINAFSI-ASKOFU CHENGULA
ASKOFU wa Jimbo Katoliki Mbeya Mhashamu Evarist Chengula amewapongeza wajubilanti 6 kwa kutimiza miaka 25 ya nadhiri ya utawa huku akibainisha kwamba hiyo siyo kazi rahisi kwa mapenzi yao bali wanapaswa kumshukuru Mwenyezi Mungu na kuendelea kumuomba awasaidie ili wazidi kusonga mbele kwa kushirikiana katika mashirika yao.
Askofu Chengula ameyasema hayo
wakati wa Homilia ya adhimisho la misa takatifu ya miaka 25 ya
utawa na kuweka nadhiri za daima kwa masista sita wa Shirika
la Bikira Maria Malkia wa Mitume wa Mbeya iliyofanyika katika
Kanisa Kuu la kiaskofu la Mtakatifu Anthony wa Padua Parokia ya Mbeya
Mjini.
Wajubilanti hao walioadhimisha miaka 25
ya utawa na kula kiapo cha nadhiri za daima ni Sr.Astrida Katimbuka, Sr.Asteria
Nyamwela, Sr.Victoria Aswile, Sr.Yosepha Ayobangila, Sr.Adelphina Kipangula na
Mkurugenzi wa Idara ya Mawasiliano Jimbo Katoliki Mbeya, Sr,Joyce Nchalla
wote wa Shirika la Bikira Maria Malkia wa Mitume wa Mbeya
.
Amesema kutimiza miaka 25 ya utawa kwa
kuachana na kila kitu katika ulimwengu na kuamua kumtegemea
Mwenyezi Mungu na kuwaletea watu neema ya kiroho na kimwili si kazi
ndogo, hivyo amewapongeza na kuwaalika kuendelea
kumtegemea na kumuomba Mama Maria kama alivyofanya kwa
Elizabeth awaongoze katika kuendelea kuwatendea mema
wengine.
Amesema nguvu zao hazingetosha
kufikia miaka 25 hiyo bali ni kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu, lakini kadri
miaka inavyozidi kusonga mbele kuna hatari ya baadhi ya watawa kuwa na
roho ya mgando ya uvuguvugu, hivyo amewakumbusha kuwa duniani ni
mahali pa kutafuta ukamilifu.
“Mmetembea na kufanya kazi hiyo kwa
miaka 25 kwa kutembea na Mwenyezi Mungu, hivyo muamshe nguvu hiyo
ndani ya mioyo yenu, ninyi mnayaona kama mambo ya kawaida lakini muelewe
hayo mambo hayazoeleki wala si ya kawaida kwani sisi tulio
nje tunayaona siyo ya kawaida, kumbuka wazazi wenu, ndugu, jamaa na marafiki
wameacha kazi zao wamekuja kuwashuhudia kuwasikia na mnavyojivunia
kwamba mtaendelea tena kwa kumtegemea Mwenyezi Mungu katika
maisha hayo,”
“Nawatakia ujumbe mwema wa Mama Maria daima
kuona mnawajibika kuwaletea watu neema na popote mtakapokuwa lazima iwe sababu ya majirani kupata neema,
neema ya kutambua uwezo wake Mwenyezi Mungu kama Mama Maria alivyofanya kwa
Elizabeth.”
Askofu Chengula amewaasa watawa kuwa
sehemu ya faraja kwa maisha ya wenzao watakao kumbana na magumu
akibainisha kuwa ikitokea basi wasimuache mwenzao anahangaika ili asijisikie
mpweke akakata tamaa lakini kama watamfuata Mama Maria itakuwa ni rahisi
kwao kwenda kuzungumza na mwenzao aliyepo kwenye matatizo na siyo ya kimali
au kimwili bali ni katika mambo ya kiroho.
“Sote tunajuwa kuwa watawa wameingia utawani
kwa ajili ya kuwa wakamilifu kama Mungu Baba na tukiona ndugu yetu
hafuati mfumo huo, huo ni umaskini lazima kwenda kumsaidia na
kumsalimia siyo lazima kumpigia kelele, ila Roho wa Bwana anayekuwa
ndani yetu ndiye atakayemsukuma, atakayemfanya atambue kwamba yeye ameingia
katika Shirika kwa ajili ya kujikamilisha, wengine wanasema
kujitakatifuza, kukamilisha utakatifu,”amesisitiza.
Amewaalika kuwa kielelezo cha
upendo katika utume huo kwa kutembeleana na kuwasihi
endapo itatokea mwenzao katika hali ya kibinadamu
hataki kukutana na Roho Mtakatifu, kwa kuwakwepa wajue kuwa
anakumbana na nguvu ya kiza, wasimtenge bali wawe naye kwa njia ya kumuombea na
kuzungumza naye daima.
Aidha Askofu Chengula amesema
watawa wanaoadhimisha nadhiri ya miaka 25 waepuke
kufanya utume kwa mapenzi yao na kupitia siku hiyo
inawakumbusha wengine kuacha mapenzi yao na kutakiwa
kufuata mapenzi ya Shirika ambalo linaongozwa na Kanisa.
“Chagueni
viongozi kwa manufaa ya shirika na mjue kuwa mbele yenu
pamoja na Mama Maria ni kazi moja kuwachagua watu watakaowasimamia muwe
wakamilifu siyo kufanya katika mapenzi yetu, na siyo kuchagua watu wa
mkoa gani, au vijana, hapana tufurahi, tuwe watu wa kushukiwa na roho,”Amefafanua.
Amebainisha kuwa viongozi
watakaokuwa wanawachagua wajue kuwa wameshukiwa na Roho Mtakatifu ili
awasaidie, huku akiendelea kuwasisitiza kuzingatia na kuziishi kanuni za Kanisa
na Shirika lao katika muongozo wa pamoja hasa katika kukazia juu ya
kusali.
Comments
Post a Comment