Maneno “uchawi” au “mchawi” kwa dhana za kiafrika hayastahili kuwamo kwenye Biblia

KATIKA kutolea maoni kibwagizo changu cha jana cha “WOTE KIMYAA!!”, mwenzetu Deonatus F. N. Mutani ametaka kutuchanganya sote. Mimi nawatafuta “wachawi” au “watu wenye uchawi” wanyeshe mvua siku hizi tupone. Nataka wajitokeze tuone. Nataka wajitokeze hadharani watende kitu cha kutufaa sote.

Nimekataa uwapo wa uchawi na wachawi kati yetu. Tulionao ni wababaishaji na watu tunaowatuhumu kwa kuwasengenyasengenya tu. Wachawi kiukweli hawapo na bado ninawatafuta. Ninataka wajitokeze na nimesema kama kuna anayewajua awataje, atuitie au atuoneshe wenzake. Mwenzetu Deonatus Mutani ametoka huko niliko na kusema eti Biblia inakiri kuwapo kwa uchawi na wachawi.
Ndipo amenishangaa mimi ni padre wa aina gani kukataa uwepo wa uchawi ambao kwa kadiri yake unashuhudiwa na Biblia yake.

Sawa. Lakini leo hii tukimuuliza mwenzetu huyu Biblia gani hiyo, bila shaka atasema ni Biblia ya Kiswahili au ya Kiingereza fulani. Kumbe, hapo ndipo atakapokosea na ndipo panaponipa mimi fursa ya kutoa somo la lugha asilia za Biblia, japo kwa ufupi tu.
Nisikilizeni vijana na wasomaji wangu.

Ni hivi, kwenye Biblia hakuna hata mahali pamoja palipoandikwa kwa Kiswahili neno “mchawi” au “uchawi” kwa mastahili. Biblia za Kiswahili zimetutumbukizia maneno hayo pasipo simile. Maneno hayo yaliyotumbukia humo hayabebi maana na dhana halisi ya kilichosemwa katika lugha asilia za Kiebrania au Kigiriki. Dhana ya Kiafrika juu ya “uchawi” na “wachawi” haiingii kwenye Biblia hata kidogo.

Nina hoja. Nadhani mnaweza kukubaliana nami kwamba katika makabila yetu dhana au fasili ya uchawi si nyepesi. Ni dhana mtambuka. Dhana au fasili yetu ya “wachawi” ni ya watu wenye nguvu za ajabu za kufanyia mambo ya ajabu kama tunavyosema wenyewe, labda kuruka angani kwa nyungo, fisi, mbweha, pembe au mikeka;

kunyesha mvua hata kiangazi; kupiga radi wapendavyo; kuingia majumbani mwa watu kwa kupitia milango na hata madirisha yaliyofungwa, kuroga tokea mbali, kutazama na kudhuru watu kwa macho au kauli, kuwabadili watu wakawa labda mainzi, nyoka au ngedere na kadhalika. Orodha ni ndefu mno. Kwa lugha yenu vijana, “orodha ni ndefu kishenzi!”.

Ndipo kwetu sisi “wachawi” ni watu wenye uwezo wa kuwatoa wafu makaburini na kuwala nyama maiti; wenye uwezo wa kufanya mikutano usiku pasipo watu wengine kuwaona; watu wenye kuwatengeneza na kuwatunza watu kama misukule; watu wenye uwezo wa kuroga wengine kutoka mbali; watu wasioweza kuonekana wanapofanya shughuli zao; watu wenye kutembea usiku uchi wa mnyama; watu wanaoweza wakawatazama watu kwa macho ya aina yake wakadhurika vibaya; watu wanaoweza kuwasemea wenzao maneno ya laana au mikosi wakadhurika na kadhalika.
 
Naomba maweza mengine muyaongezee wenyewe maana, bila mashaka, kwenu dhana hii ipo nanyi, kama humwamini wenyewe, walau mmesikia habari zake. Zaidi sana, imani hiyo mnaijua ilivyotuganda Waafrika wengi kiasi cha Baba Mtakatifu Benedikto XVI kutuonea huruma katika mausia yake Africae Munus namba 93 yaliyoelekezwa kwa Waafrika wote pale mwaka 2009 kufuatia Sinodi ya Pili ya Afrika.

Aghalabu, mnajua jinsi tunavyodhuriana katika jamii zetu, kujichonganisha, kupoteza muda na pesa nyingi, kwa shughuli za jamaa kushikana na kwenda “kunyoana” kwa waganga wa kienyeji; watu kuwaalika “akina Lambalamba” na “kusafisha vijiji” vyao; watoto kuwatuhumu na kuwaua wazazi wao; wanavijiji kubomoleana nyumba au kuchomeana moto wakifukuzana kwa ukatili mkubwa;
Watu kuwaua vikongwe na wazee; watu kuwafukuzia watuhumiwa wao kwenye vijiji vya wachawi; watu kuwapiga na kuwachomea wengine nyumba moto au kuwaharibia mazao na mali zao wakidaiwa kuzuia mvua; timu zetu za michezo kutumia pesa nyingi kulipia “mabenchi ya ufundi” yaani waganga wa kienyeji; wachezaji wetu kupewa masharti magumu au kulazwa makaburini kabla ya mechi; watu kuzindika nyumba zao kwa hirizi;

Watu kuwaua au kuwadhuru albino wakitafuta viungo vyao wapate vyeo na utajiri; watu kutafuta mifupa na mafuvu ya binadamu kwa ajili ya kuboreshea biashara au ajira zao; akina mama kuuawa kwa sababu ya sehemu zao za siri; watu kunyofolewa macho, ndimi na masikio; watu kutafuta, kuchukua na kuvaa hiziri na kadhalika.
 
Sina mashaka, haya yote mnayajua; imani na vitendo vilivyoipa Tanzania nafasi ya kwanza Afrika katika kuamini uchawi, kwa kadiri ya utafiti wa mwaka 2009 wa PEW Research Centre ya Washington D.C., Marekani. Lakini habari ngeni kwenu nyote ni hii kwamba Biblia haina dhana hiyo, hata chembe na hakuna panapostahili kutokea neno “uchawi” au “mchawi” ndani yake. Maneno hayo yanatokea isivyostahili.

Msishtuke. Ndipo hapo hapo ninapojaribu kulitangaza jambo hili pasipo kusadikika. Wengi wananishangaa sana. Lakini si kitu nimeunda jeshi la mtu mmoja! Hata ndugu yetu Deonatus Mutani ananishangaa sana. Kumbe, nguvu ya hoja yangu ni lugha asilia zilizotumika kuandikia Biblia. Nawahakikishieni nyote kwamba dhana yetu ya uchawi na wachawi haimo kwenye Biblia maana maneno yote asilia yaliyotumika humo hayana MAANA ZETU. 

Msinibishe. Nendeni kwenye lugha asilia Kiebrania (Agano la Kale) na Kigiriki (Agano Jipya).
Biblia katika lugha zake asilia hazina maneno yenye maana zetu. Ndiyo maana nakataa kwa nguvu na kwa kujiamini kabisa. Tafsiri za Kiswahili na Kiingereza zinatupotosha. Kwa bahati njema baadhi ya watafsiri wa nakala za Kiingereza wamejitahidi sana ama kuepuka au kutumia kiusahihi maneno: “witchcraft”, “sorcery” na “magic”. Katika Kiswahili tuna maksi ya karibu sefuri.

Tusiandikie mate, wino ungalipo. Hebu tuthubutu kujitengea muda siku fulani tujisomee na kutafakari kwa utulivu sehemu zifuatazo: Mwa 41:8.21, 1Sam 28:7, Kut 7:11.22, 8:7.18.19, 9:11, Law 19:26, Kum 18:10-11, Isa 3:3, 47:9.12, Dan 1:20, 2:2.10.27, Nah 3:4, Mdo 13:6.8, 19:19, Gal 5:20 na Ufu 22:15. Hizi ndizo sehemu maarufu kwa maneno “uchawi”, “mchawi” au “wachawi”.
Zatupasa kuzichambua kwa makini. Maneno yametumika kwa kupwaya mno.
Nawahakikishieni tena kwamba tukizitalii sehemu hizi katika lugha zake asilia, hatutapata maana ya wachawi katika dhana ya Kiafrika isipokuwa mojawapo ya maana hizi:
mabingwa wa kutumia visivyo utaalamu mbalimbali, wachanganya madawa, wacheza mazingaombwe, watu wenye kuwatinga wenzao kwa utaalamu, wataalamu wa nyota, watabiri, wapiga ramili, waona maono, watu wanaotafuta ushauri wa wafu au mapepo, watafsiri ndoto na kadhalika.
 
Maana hizi ndizo zilipaswa kuchaguliwa vyema na waliotutafsiria Biblia katika Kiswahili zamani zile. Kumbe, wote waliotajwa hivyo, kwenye Biblia, kwa Wayahudi, walikuwa wataalamu waliokuwa wanajulikana na watu na utaalamu wao uliwekwa kwenye vitabu vyenye kusomeka bayana (rej. Mdo 19:19).

Swali  halali ni “Kama uchawi unataja zaidi utaalamu fulani, inakuwaje Biblia inasema “wachawi wauawe” au hawataingia mbinguni, kwa mfano Gal 5:19-20 na Ufu 22:15?  Jibu ni rahisi, wataalamu  (“wachawi”), iwe kwa maana ya waona maono, wachanganya dawa, wataalamu wa nyota, wacheza mazingaombe na kadhalika, wakipitiliza maana nzuri ya utaalamu wao na kuanza kubabaisha watu wengine wanaingia katika eneo la dhambi na hapo ndipo wanapostahilisha adhabu kali.

Kwa mfano, mchanganya madawa akichanganya dawa zake kiasi cha kuwalewesha watu kudhuru afya zao na kuwafanya wabwate bwate  na kukiri mambo yasiyojuzu (kwa mfano kwa kupewa ketamini), atenda dhambi kubwa naye anajistahilisha adhabu kubwa. Ndivyo inavyoweza kuwa katika mambo yote. Kuchinja kuku si dhambi, lakini anayetumia ujuzi na wepesi wake wa kuchinja kuku kuchinja watoto wa watu, afanya dhambi naye astahili kutupwa motoni. Udreva si dhambi, lakini dreva anayeendesha gari na kuwaponda watu barabarani afanya kosa kubwa naye anastahili asiingie mbinguni.

Anayepiga dawa ya usingizi ili watu wafanyiwe operesheni (nusu kaputi), anafanya kazi iliyotukuka. Lakini mtu huyo huyo akiwatia watu dawa kwa kuwalipa kisasi ili wafe watakapofanyiwa operesheni afanya dhambi naye astahili kutupwa motoni na kadhalika. Ndipo kumbe ilipostahili, katika tafsiri, kuchagua sana maneno ya kutumia badala ya kutafsiri sehemu zote kwa neno kumbakumba “uchawi”.
Maana yake ilitakiwa kuwa makini sana kwa sababu hata kama vitu vinafanana majina vinaweza kutofautiana. Ndiyo kisa kuna “paa” na “paa” na kuna “kaa” na “kaa”. Kifupi, ilipasa kuainisha na kupembua aya kabla ya kulitumbukiza neno uchawi kila mahali. Unakwazika kwa haya ninayosema? Usikwazike. Nakujulisha.

Huu ndiyo utaalamu wa tafsiri unaosomewa katika vyuo vya kutafsiri Biblia katika Kanisa Katoliki, kwa mfano Biblicum, Roma. Neno la Mungu (Biblia) kwetu sisi Wakatoliki ni uwanja wa utaalamu na si dhambi kuchunguza mambo kiasi cha kitaalamu. Kanisa Katoliki si kanisa la wakariri Biblia tu, ni Kanisa la waelewa Biblia.

Ndipo, basi, tusidanganyike tukachukua dhana yetu ya uchawi ya Kiafrika tukaiingiza kwenye Biblia takatifu. Tutakuwa waongo na wakufi wa weledi. Narudia na kusisitiza kwamba katika Biblia hicho kinachotafsiriwa kama “uchawi” kilikuwa aina ya elimu au utaalamu. Ndiyo maana kulikuwa na vitabu vyake kama nilivyosema sasa hivi (rej. Mdo 19:19) na watu wenye elimu hiyo walikuwa wakijulikana na wengine.


Wataalamu wenyewe hawakumwonea mtu yoyote haya na wala hawakujificha. Ndiyo maana waliwahi kuitwa na Farao wakatokea barazani (Kut 7:11) na waliwahi kuitwa na mfalme Nebukadneza huko Babiloni wakajumuika na wataalamu wengine (rej. Dan 2:2). Hali kadhalika tazama jinsi Simeoni “mcheza mazingaombwe” alivyokuwa anajulikana na watu (rej. Mdo 13:6.8).

Comments

  1. Asante sana uchawi haupo ni matapeli tu na wafanya mazingombwe, eti mtu apae angani kwa ungo?? Never on earth

    ReplyDelete

Post a Comment

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU