‘Utajiri usiwasahaulishe Mungu,’ waamini watahadharishwa

MOROGORO, Askofu Telesphor Mkude wa Jimbo Katoliki Morogoro amesema kuwa mali na utajiri si kigezo au sababu ya kumsahau mwenyezi mungu kama ilivyo desturi ya baadhi ya watu wanaomsahau wanapopata mafanikio.
Amesema hayo wakati wa kutoa Daraja Takatifu la Ushemasi kwa Mashemasi watatu wa shirika la Mtakatifu Vicenti wa Msalaba iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Patris jimboni Morogoro.
Askofu Mkude amesema kuwa ni watu wachache ambao wanamuweka mbele Mwenyezi Mungu wanapopata mafanikio katika nyanja mbalimbali, isipokuwa wengi wao wanamsahau Mungu kabisa na kutawaliwa na utajiri unaowazunguka.
“Watu wachache ambao wamekuwa wakimuweka Mungu mbele wanapopata mafanikio katika nyanja mbalimbali maishani mwao huku wengi wao wakimsahau kabisa na kutawaliwa na utajiri unaowazunguka pia husahau walipokuwa wakitafuta walipiga goti ili wapate, kwa vile wamepata hawana budi waendelee kumshukuru Mungu ili aendelee kuwabariki na kulinda kile walichobarikiwa,” amesema Askofu Mkude.
Aidha amesema kuwa watawa ni mfano bora wa kuigwa katika maisha kutokana na kazi na majitoleo yao katika huduma za jamii bila ya kudai ujira na maslahi bali wanafanya kazi zao kwa utii na unyenyekevu kwakuwa ni wito huku wakiendelea kumshukuru Mungu katika utawa wao.
“Watawa ni mfano wa kuigwa kwakuwa wamejitoa sadaka kwa Mungu ili wahudumie watu kiroho na kufanya shughuli nyingine za kijamii kwa kujitoa pasipokudai ujira wowote, naamini haya yote wanafanikisha kwa kumtanguliza Mungu kwa walichokifanikisha, wanachofanya na wanatakachofanya hawachoki kumshukuru na kumuomba katika kila hatua yao, nami nawatia moyo katika hilo na wasikate tamaa katika kuitenda kazi ya Bwana kwakuwa mavuno ni mengi ila watenda kazi ni wachache,” amesema Askofu Mkude.
Hata hivyo kiongozi huyo wa kiroho amesema kuwa si vibaya kuwa na mali na utajiri katika dunia, bali mali na utajiri zitumike kwa unyenyekevu ili iwe njia pekee ya kuwasaidia wahitaji mbalimbali ambao Mwenyezi Mungu anawatizama kwa jicho la huruma.
Mbali na hayo Askofu Mkude ametoa pongezi kwa mashirika mbalimbali ya kitawa jimboni humo, kutokana na mchango wao katika huduma za kiroho kwa waamini, ambazo zinaendelea kuwa kivutio katika jimbo katoliki Morogoro


Shirika la Mtakatifu Vicenti wa Msalaba mpaka sasa lina miaka zaidi ya 300 tangu kuanzishwa kwake, likiwa na mwendelezo wa huduma za kiroho katika sehemu mbalimbali za dunia zinazotolewa na mapadri na masista katika kulitegemeza Kanisa la Mungu.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU