Sababu za maelfu kuukimbilia ushirikina

SWALI: Padri, kuna viongozi wengi nchini, wakiwamo wa dini, wanaojilinda kwa ulozi. Wewe unasemaje juu ya jambo hili? Hii si aibu kwetu? Swali hili limeulizwa na vijana katika akaunti yangu ya Facebook.

Jibu: Ninayo habari na maneno ya namna hiyo ya kwamba viongozi mbalimbali, wakiwamo wa kidini, wanaojilinda kwa ulozi. Ninyi vijana mnaniuliza juu ya maoni yangu, lakini kwa kweli mimi sijui niseme nini kuhusu tuhuma hizo. Inabidi ufanyike utafiti ili watu wanaojilinda kwa ulozi wahesabiwe.

Husikika kwamba watu hutafuta uongozi kwa kuwaendea waganga wa kienyeji wanaowapa dawa za kunywa au kujipaka pamoja na hirizi za kuvaa. Husemwa wengine huagizwa wawaue albino au wawatoe kafara watu wa karibu nao. Kishapo husemwa viongozi wengine wakishapata madaraka na vyeo walivyowania hujilinda kwa hirizi na kinga mbalimbali.

Sasa, kwa kuwa haujafanyika utafiti wowote, tuhuma hizo zinabaki kuwa tuhuma tu. Lakini kutokana na utafiti wa mwaka 2009 wa PEW Research Center ya Washington, DC, ulioonesha kwamba Tanzania ni nchi ya kwanza barani Afrika kwa kuamini uchawi (kwa vile uligundua kwamba 93% ya Watanzania wanaamini katika ushirikina).

Kusema kwamba viongozi mbalimbali, wakiwamo wa kidini wanajilinda kwa ulozi kunaweza kufanana na ukweli. Hakika mtu anayeamini katika mambo ya kishirikina, lazima atashindwa kujiamini kuishi pasipo kuyategemea mambo anayoyaamini.

Lakini hiyo ni bahati mbaya sana. Wakristo tulipaswa kumwamini Mungu na kumwacha yeye atulinde. Wala haiingii akili, mtu anayemwamini Mungu mwenyezi aamini kupata ulinzi kutoka kwenye kipande cha mti au mzizi ulioshonewa hirizi. Mti mzima hauwezi kumlinda mtu, sembuse gome au kipande chake cha mzizi uliokufa!

Wala haiingii akili, mtu anayemwamini Mungu mwenyezi aamini kupata ulinzi kutoka kwenye jino la nguruwe au kutoka kwenye kipande cha mkia wa kenge aliyekufa. Nguruwe mzima au kenge mzima hawawezi kumlinda mtu, sembuse meno yao au mikia yao iliyokaushwa! Tena ni kinyume kabisa cha matazamio ya Mungu. Mungu alituamuru tukavitawale viumbe vyote, kumbe badala yake tunatawaliwa navyo! Ndivyo tunavyosoma kwenye Biblia.

Sikiliza imeandikwa, “Kisha Mungu akasema, ‘Tumfanye mtu kwa kwa mfano wetu, kwa sura yetu; atawale samaki wa baharini, ndege wa angani, wanyama wa kufugwa , dunia yote na viumbe vyote vitambaavyo.’

Basi, Mungu akamuumba mtu kwa mfano wake; naam, kwa mfano wake Mungu alimuumba, alimuumba mwanamume na mwanamke. Mungu akawabariki na kuwaambia, ‘Zaeni muongezeke, mkaijaze nchi na kuimiliki, muwatawale samaki wa baharini, ndege wa angani, na kila kiumbe hai kitembeacho duniani’” (Mwa 1:26-28).

Sasa inakuwaje binadamu kushuka hata kuhangaishwa na ndege kama bundi, sisimizi, panya, mende na kadhalika na si kukomea hapo bali kwenda mbali zaidi na kuamini kwamba viumbe hivyo, mifupa yao au ngozi zao zinaweza kuwapa ulinzi kumpita Mungu? 
Hapo ndipo inapoingia aibu kwa shughuli zima za kutafuta bahati na ulinzi wa kishirikina au ulozi Hilo la kujilinda kwa vitu vya ziada vya kishirikina wenyewe wanaita siku hizi “ulinzi shirikishi”. “Ulinzi shirikishi” si sawa na ni kazi bure kwa maana Mungu ndiye mlinzi halisi na chochote tunachofanya kilitakiwa kiwe chini ya usimamizi na baraka zake.

Si kwamba tusema wanadamu tukae na kusubiri kulishwa kama kuku zizini, la hasha. Kuna upande wetu na kuna upande wa Mungu katika utendaji wetu. Kwa upande wetu tulitakiwa kujiamini na majaliwa aliyotupatia yatusaidie maishani, yaani vipaji vya akili na utashi na karama au talanta zetu mbalimbali (1Kor 12-14).

Ndivyo inavyopasa kutendeka, sisi tutumie akili na utashi na neema tunazopata kutoka kwa Mungu na yeye abariki nia na kazi zetu. Nasisitiza kusema ndivyo ilivyopasa kufanyika kwani tumeandikiwa ifuatavyo: “Mwenyezi Mungu asipoijenga nyumba, waijengao wanajisumbua bure. Mwenyezi Mungu asipoulinda mji, waulindao wanakesha bure. Mnajisumbua bure kuamka mapema asubuhi na kuchelewa kwenda kumpumzika jioni, mjipatie chakula kwa jasho lenu. Mungu huwazuruku walio wake hata walalapo” (Zab 127:1-2).

Kumbe, kweli tunajiaibisha mbele ya Mungu na mbele ya wenzetu, kwa kuamini kwetu mambo ya ushirikina na ulozi. Mungu anatushangaa na bila shaka atatuadhibu kwa kupindua alichotupangia kiwe. Anapika dawa yetu, ikiiva atatunywesha. Tutakiona cha mtema kuni kilichomtoa khanga manyoya huko mwishoni mwa maisha haya. Basi, ole wetu. Tuache kuyategemea mambo hayo na kwa kweli aliyakataza.

Tusisahau tulivyopigiwa marufuku kujihusisha na mambo ya kishirikina katika Kum 18:9-13.
Tumeandikiwa, “Mtakapofika katika ile nchi niwapayo Mwenyezi Mungu, Mungu wenu msifuate zile tabia za kuchukiza za mataifa ya huko. Asiwepo mtu yeyote miongoni mwenu atakayemchoma mtoto au mwanawe wa kiume au wa kike kuwa tambiko, wala mtu apigaye ramli, wala mwaguzi, wala mpiga bao, wala “mcheza mazingaombwe” ya kudhuru, wala mlozi, wala mwenye kutaka kauli kwa mizimu na pepo au kutoka kwa wafu, maana yeyote atendaye mambo haya.

Mambo haya ni chukizo kwa Mwenyezi Mungu na kwa ajili ya mambo haya ya kuchukiza Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, anawafukuza watu wa namna hiyo mbele yenu. Muwe wakamilifu mbele ya Mwenyezi Mungu, Mungu wenu”.

Watu wa mataifa mengine wanatuonea huruma Waafrika wote kwa sababu hatutaki kubandukana na mambo ya imani ya kishirikina. Wenzetu wengi walishabandukana nayo na wala hawajala hasara yoyote. kwa upande wetu hatutaki kubandukana nayo na wala hatupati faida yoyote. Kwa nini tusivae ushujaa wakuachana na kitu ambacho hakituletei faida wala hasara tuliachana nacho?
 
Baba Mtakatifu Benedikto XVI akituonea huruma alituusia kwa maneno haya: “Uchawi, ambao msingi wake ni dini za jadi, kwa hivi karibuni hutiwa tena nguvu. Woga wa zamani unaibuka tena na unatengeneza pingu poozeshi za kutojiamni. Wasiwasi kuhusu afya, ustawi, watoto, hali ya hewa, na kujikinga na pepo wabaya mara nyingine husababisha watu kukimbilia kwenye mazoezi fulani ya dini za jadi za Kiafrika ambayo hayapatani na mafundisho ya Kikristo.
Tatizo la ‘kujisajili kuwili’ – kwenye Ukristo na kwenye dini za jadi za Kiafrika – linabaki ni changamoto. Kwa njia ya katekesi na utamadunisho wa kina, Kanisa huko Afrika linahitaji kuwasaidia watu kugundua ukamilifu wa tunu za Injili. Ni muhimu kuweka wazi maana ya kina ya mazoezi haya ya ushirikina kwa kuainisha mambo mengi ya kiteolojia, kijamii na kiuchungaji yanayohusu janga hili” (Africae Munus na. 93).

Lakini ajabu ni kwamba Waafrika wengi hatuyajui mausia haya na wala hatujali. Eti huko mbele ya safari Waafrika tutakapotupwa motoni kwa kuamini na kuendesha maisha kwa imani za kishirikina tutashangaa!


Imetangazwa kabisa tutaadhibiwa na hatutaonja ufalme wa Mungu tukibaki katika uongo wa kishirikina bado hatutilii maanani  jambo hilo (rej. Gal 5:19-21). Sisi bwana! Kwa herini kwa sasa!

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU