UTUME WA KATEKESI KATIKA KANISA
SEHEMU YA KWANZA
                          


ASILI NA MAANA YA NENO KATEKESI
Neno Katekesi kadiri ya mazoea ya wengi lina maana ya maarifa ya kufundisha katekisimu,  pia ni maarifa ya namna ya kufundisha dini.  Dini maana yake ni uhusiano baina ya Mungu na mwanadamu. Katekesi kama namna ya kufundisha dini, ina maana ya kumwelekeza mtu atambue uwepo wa Mungu, Uwezo na Nafasi yake katika maisha ya mwanadamu.
Kwa asili neno Katekesi linalotokana na neno la lugha ya kiyunani Katechein au katechizen likiwa na maana ya kufundisha kwa mdomo.
Katika Agani Jipya tunaona mkazo wa namna hiyo ya kufundisha kwa mdomo katika nukuu mbalimbali kwa mfano:-
‘... enendeni mkawafanye kuwa wanafunzi wangu... na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi’ (Mt 28:19-20).  ‘...mtu huyo alifundishwa njia za Bwana, na kwa kuwa roho yake ilikuwa ikiwaka alianza kunena na kufundisha kwa usahihi habari za Yesu...’ (Mdo 18:25); ‘...nipate kunena maneno...nipate kuwafundisha wengine’ (1Kor 14:19);  ‘....mwanfunzi amshirikishe mkufunzi wake katika mema yote’ (Gal 6:6); ‘...mmekwisha kulisikia neno neno la kweli, habari njema ya wokovu wenu...’ (Efe 1:13). Pamoja na kufundisha kwa mdomo, bado katika Injili neno katekesi linajionesha hasa katika maana ya kazi ya kuhubiri ambayo hufanyika zaidi kwa njia ya mdomo kama tunavyosoma katika habari za Yesu, alikuwa akihubiri na kufundisha kwa mdomo mfano  ‘hata baada ya Yohana kutiwa gerezani Yesu akaenda Galilaya akihubiri habari njema ya Mungu (Mk. 1:14,). Naye alikuwa akizunguka katika Galilaya yote akifundisha na kuhubiri habari njema katika masinagogi yao’ (Mt. 4:23).
Ni katika Injili ilivyosimuliwa na Luka tunasikia Yesu akisisitiza kuwa utume wake awali ya yote ni kuhubiri ni lazima autimize na kuukamilisha kadiri ya mpango wa Mungu Baba ninamnukuu ‘Roho wa Bwana yu juu yangu kwa maana amenitia mafuta ili niwahubiri maskini Habari Njema’ (Lk 4:18). Tena alikazia kuwa ‘imenipasa kuhubiri habari njema ya ufalme wa Mungu katika miji mingine pia’ (Lk.4:43), mwisho Luka anatuonesha jinsi Yesu alivyotekeleza utume huo kwa kuwaendea watu waliohitaji kusikia Habari Njema ‘…ikawa baada ya hayo alikuwa akizungukazunguka katika miji na vijiji akihubiri na kutangaza habari njema...’ (Lk. 8:1).
Pia Injili inaonesha kuwa Yesu alikutana na watu aliowafundisha katika mahali pao pa sala ‘ikawa siku moja alipokuwa akifundisha watu hekaluni na kuhubiri watu habari njema (Lk.20:1).
Kutokana na mifano hiyo, tunahitimisha kuwa waandishi wa Injili wanasema wazi kuwa Katekesi ni kufundisha, kuhubiri, kutangaza, kushirikisha na kufahamisha.
Katika Kitabu cha Matendo ya Mitume tunasikia habari za Mitume waliokuwa wakifundisha kwa mdomo. Mfano, katika tukio la Pentekoste ya kwanza Petro kwa ujasiri alisimama na kutangaza wazi Fumbo la Ufufuko wa Bwana tunasoma ‘…Petro akasimama… akapaza sauti yake akawaambia…’ (Mdo 2:14- 36).
Pamoja na mitume kuna wengine waliojitokeza pia kushirikiana nao katika kuitangaza Habari hiyo Njema ya wokovu mmoja wapo ni yule Apolo myahudi wa Iskanderia aliyeishi kule Efeso kama tunavyosoma ‘…huyo alikuwa amefundishwa njia ya Bwana; na kwa kuwa roho yake ilikuwa ikiwaka alianza kunena na kufundisha kwa usahihi habari za Yesu, naye alijua ubatizo wa Yohani tu (Mdo 18:25).   
Pia Paulo mwenye anathibitisha kuwa alishiriki utume wa mkatekista katika Kanisa la mwanzo kama anavyosema ‘sikujiepusha katika kuwatangazia neno lolote liwezalo kuwafaa, bali niliwafundisha waziwazi nyumba kwa nyumba (Mdo 20:20). Na katika katika nyaraka zake, Mtume Paulo anasema wazi, ‘basi sisi tunamhubiri Kristo aliye sulubiwa’ (1Kor.1:23). Na anaongeza kusema kuwa aliitenda kazi hiyo kwa ushirikiano na wengine ‘...maana Mwana wa Mungu Kristo Yesu aliyehubiriwa katikati yenu na sisi yaani mimi na Silwano na Timotheo... katika Yeye ni ndiyo. (2Kor.1:19).
Pamoja na mtazamo huo wa kibiblia, bado kuna wataaalamu mbalimbali wamejaribu na wanendelea kujitahidi kulielezea neno Katekesi kadiri ya mitazamo yao. Katika ujumla wao wengi waliiona katekesi kuwa ni tendo, kazi au shughuli zote zinazofanywa na Kanisa ili kufanikisha ufahamu wa binadamu katika kujua ufunuo wa kimungu. Wanaowakilisha mtazamo huu wa katekesi wanasema yafuatayo.
Katekesi ni kila tendo linalofanywa ndani ya Kanisa ambalo linamshirikisha binadamu Neno la Mungu kikamilifu katika mazingira ya maisha yake (Van Caster). Shughuli inafanywa na Kanisa ili kumwingiza binadamu aone kazi ya Mungu ya ukombozi. Katekesi ni shughuli inayomshuhudia Kristo ikitangaza Neno lake na Utume wake wa wokovu wa mwanadamu.  Katekesi ni tangazo la ujumbe wa maisha ya Kristo, na ni elimu ihusuyo imani hai, tena ni mwanzo wa kuingia katika maisha ya Kanisa. Katekesi ni kazi ya kufunua mwito wa Mungu kwa binadamu aweze kutambua mwito wa upeo na mwitikio kwa njia ya imani iliyo Imara (Audinet 1974).
Maisha ya kushirikishana kiimani na waamini wapya katika Kanisa (Jean Danelou); Mafundisho juu ya Imani ya kikristo (J.A. Jungman). Katekesi katika mwelekeo wa kimystagojia inamaana ya kuelekeza kwa kina mafundisho ya dini baada ya ubatizo (A. Liege). Katekesi pia humaanisha maelezo na tafsiri juu ya Tangazo la awali la Habari njema (Kerygma) anayopewa mtu ili kuendeleza ujuzi wake hata elimu ya dini (J. Colombo).
Nia ya katekesi ni kuamsha na kuchochea imani mioyoni mwa watu pia ni kusisimua binadamu ili aishi maisha yaliyonyooka kiimani (Nijmegen School).

Kwa nyakati zetu tafsiri sahihi na ya kina ya neno katekesi ni ile iliyotolewa na Mamlaka ya Ufundishaji ya Kanisa (Magistero) katika Katekisimu ya Kanisa Katoliki.  Katekisimu hii inaeleza kuwa katekesi ni jumla ya jitihada zote za makusudi na njia zote za Kanisa Katoliki za kuwatafuta, kuwaunda, kuwaingiza na kuwakomaza waamini wake (wapya na wale waliotayari waamini  tangu zamani) katika kuwasaidia kuamini kweli kuwa Kristo ni Mwana wa Mungu na kwa imani hiyo wapate uzima wa milele kwa njia ya Yesu Kristo.
Hii ina maana kuwa Katekesi ni jitihada na njia zote za kimpangilio za kuwatafuta, kuwafundisha na kuwaelimisha watu katika Imani ya kikristo na za kuujenga mwili wa fumbo wa Kristo yaani Kanisa ambalo ndilo Sakramenti ya wokovu katika maisha ya hapa duniani.
Na hii inatufanya sisi kuelewa kuwa Katekesi ni shule na elimu katika imani kwa watu wote na wa nyanja zote kuanzia watoto na vijana wote na pia kwa watu wazima ndani na nje ya familia.

Kwa kuwa katekesi ni elimu basi ni lazima itolewe kwa mpangilio na utaratibu wa hatua kwa hatua mpaka mwisho ili kuwaingiza wamini katika ukamilifu wa maisha ya kikristo, kwa kufuata kwa makini na uaminifu muhtasari wote wa mafundisho ya Imani ya Kanisa ulio kwenye kitabu/kijitabu tukiitacho Katekesimu -hasa ile maarufu kama (KKK  4-6).

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU