TEC wapigwa msasa juu ya sheria ya ajira

WATUMISHI wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) wamepewa mafunzo maalum juu ya sheria ya kazi ili kuleta ufanisi katika utendaji kazi ikiwa ni sehemu ya  tekeleza sheria, timiza wajibu, na  imarisha mahusiano chanya katika  sehemu za kazi.

Mafunzo hayo ya siku moja yamefanyika katika Makao Makuu ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) Kurasini jijini Dar es Salaam na kuongozwa na wataalamu kutoka Wizara ya Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu wilaya ya Temeke.

Katibu Mkuu wa  Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) Padri Raymond Saba ameeleza kuwa, TEC imeamua kuwaalika wataalamu kutoka Wizara ya Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu ili kutoa ufahamu wa sheria ya kazi na mahusiano kazini kwa lengo la kuendesha taasisi katika utaratibu unaoleta ufanisi kwa kujenga mahusiano mazuri yenye tija baina ya mwajiri na mwajiriwa.

“Lengo ni kuwasikiliza wataalamu wetu, tuwaelewe, tuzifahamu na kuielewa sheria ya ajira ili kuweka mfumo wa utatuzi wa migogoro ya kazi kwa njia ya usuluhishi, na uamuzi sahihi, kujenga mahusiano chanya na kupata mwongozo wa kisheria kuhusu mahusiano mazuri mahala pa kazi na viwango vya kazi,” amesema Padri Saba.

Akitoa ufafanuzi kuhusu sheria hiyo, Afisa Kazi mwandamizi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Wizara ya Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu wilaya ya Temeke Bi Vedastus Kapongo ameeleza kuwa, kila mwajiriwa na mwajiri wana haki ya kuzijua sheria ya kazi na mahusiano kazini Na.6/2004 ili kuwa na mfumo sahihi wa kuendesha taasisi yoyote ile.

“Licha ya kuwa taasisi binafsi zina mamlaka ya kutunga taratibu zake za kazi, taratibu hizo lazima zifuate mwongozo wa Sheria Mama ya Ajira na mahusiano Kazini ya mwaka 2004 kwani hakuna aliye juu ya sheria, taratibu na miongozo ya kazi katika sekta binafsi na zile za serikalini lazima zisipingane na sheria hii kwani sheria hii ndiyo mwongozo wa nchi katika ajira,” amesisitiza Bi. Kapongo.

Akifafanua juu ya matumizi ya sheria hiyo, Bi. Kapongo ameeleza kuwa, Sheria hiyo inawahusu waajiri na wafanyakazi wote waliopo katika sekta binafsi na umma Tanzania Bara lakini haiwahusu wafanyakazi walioajiriwa katika utumishi wa Jeshi la wananchi wa Tanzania, Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza na Jeshi la kujenga Taifa.

Kati ya vifungu vya sheria alivyovifafanua ni pamoja na Ubaguzi katika ajira unaokatazwa chini ya kifungu cha saba (7)
Ubaguzi hauruhusiwi katika mambo yafuatayo: Taratibu za ajira, Upandishwaji vyeo, Uhamisho, Mafunzo, Mishahara, Mgawanyo wa majukumu, Kushusha cheo na Kuachisha kazi na hatua za nidhamu.

Kwamba sheria inasema si ubaguzi mwajiri kutoa ajira kulingana na Sifa au mahitaji halisi ya kazi, Kulingana na Sheria ya Huduma za Ajira ya mwaka 1999, Kwa upendeleo katika kukuza fursa sawa na kuondoa ubaguzi mhala pa kazi (Affirmative action)”
Sheria ya mkataba
Amezungumzia pia sheria ya mkataba akisema kuwa, Mkataba ni makubaliano ya pande mbili ikiwa na lengo la kutekeleza shughuli fulani ambapo amebainisha kuwa mkataba huo lazima uwe wa hiari, umesainiwa na pande mbili zenye akili timamu, lazima uwe na thamani,uwe wa maandishi wenye masharti yanayoendana na Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Na.6/2004
Amezitaja aina za mikataba ya Ajira kulingana na sheria hiyo akisema kuwa,
Saa za Kazi
Ameelezea pia sheria ya saa kazi akisema kuwa, Sheria inaruhusu mfanyakazi afanye kazi Siku 6 kwa wiki, Saa 45 kwa wiki na Saa 9 kwa siku.

Kwa mujibu wa kifungu cha 23 cha Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Na. 6/2004 Mwajiri anawajibika kumpa angalau saa moja ya kupumzika mfanyakazi aliyefanya kazi kwa masaa matano mfululizo kwa siku.

Mwajiri hatakiwi kumfanyisha kazi mwajiriwa saa za ziada bila kuwepo na makubaliano. Endapo mfanyakazi atakubaliana na mwajiri kufanya kazi za ziada, saa za ziada hazitazidi masaa matatu kwa siku na masaa 50 kwa wiki nne.

Malipo ya saa za ziada
Kwa mujibu wa kifungu cha 19 (5) saa za ziada zitalipwa kwa kiwango cha 1.5 ya mshahara wa saa kwa kila saa aliyofanya kazi mwajiriwa kwa siku za kawaida.

Siku za mapumziko/sikukuu
Mfanyakazi anastahili kupumzika siku moja katika kila wiki pamoja na siku zote za sikukuu. Pale ambapo kwa maridhiano na mwajiri, atafanya kazi kwa siku za mapumziko atastahili kulipwa mara mbili ya mshahara wake kwa kila saa atakayofanya kazi.
Kwa mujibu wa kifungu cha 21 cha sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini, kwa makubaliano ya maandishi, mfanyakazi anaweza akafanya kazi kwa masaa 12 kwa siku ikiwa ni pamoja na muda wa chakula cha mchana pasipo kupata malipo ya ziada. Kwa mkataba huo mfanyakazi hatatakiwa kufanya kazi zaidi ya Siku 5 kwa wiki, Saa 45 kwa wiki na Saa 10 kwa saa za ziada katika wiki.


Kwa ufafanuzi zaidi  fuatilia gazeti la kiongozi katika matoleo yajayo ambapo sheria hii itachapishwa mfululizo ili kuleta uelewa wa kina.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU