Wazazi waaswa kusaidia Utoto Mtakatifu kuinjilisha

     
WAZAZI na walezi kote nchini wametakiwa kujitoa kwa kila hali na mali kuwasaidia watoto kushiriki matamasha ya kiroho, kongamano na hija  za Utoto Mtakatifu, ikiwa ni sehemu ya malezi kwa mtoto.
      Akitoa homilia katika Misa Takatifu kigango cha Mbutu Parokia ya Kimbiji Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam Paroko Msaidizi wa Parokia hiyo Padri Justus Lugayimkam amewakumbusha na kuwataka wazazi na walezi wote kutambua kuwa, jukumu  la kulea Watoto wa Utoto Mtakatifu, lipo mikononi mwao na mtoto anapokua katika malezi ya dini humfanya awe mwenye heshima na mchamungu.
          Amesema wapo walezi ambao jukumu la Utoto Mtakatifu wamewaachia walimu jambo linaloleta ugumu kwa walimu  pindi  inapotokea watoto wanahitaji kushiriki katika matamasha mbalimbali .
“Watoto wanahitaji mchango wa kifedha ili waweze kushiriki matamasha na watoto wenzao kutoka katika maparokia mbalimbali. Amesema michango hiyo ya fedha ni kwaajili ya nauli na chakula hivyo kila mtoto anapaswa kuchangiwa na mzazi wake ama mlezi si mwalimu,” amesisitiza.
Amewataka wazazi kutambua kuwa Yesu Kristo anawapenda watoto waende kwake kama alivyosema  “waacheni watoto waje kwangu kwa maana ufalme wa mbingu ni wao,” kwa hiyo ni vema wazazi wakawa bega kwa bega na walimu wa utoto mtakatifu  ili kuwawezesha watoto kuwa wamisionari wa kuinjilisha katika maeneo mbalimbali ndani ya nchi.
Hata hivyo kilio cha  Watoto wa Utoto Mtakatifu kwa wazazi wao kutowachangia pale wanapohitajika kwenda kuhiji, kuinjilisha ama kukutana na watoto wenzao kijimbo na kitaifa kimekuwa ni cha muda mrefu na kipo katika majimbo karibu yote Tanzania.
Hivyo wazazi wanasisitizwa kuweka kipaumbele cha kuwawezesha watoto wao kukutana katika kutafakari neno la Mungu, kufanya matendo ya huruma kwa wengine na kuinjilishana kwani hayo ndiyo malezi chanya kwa watoto hususani katika nyakati hizi.

Kipaumbele cha wazazi kiwe katika kuinjilisha watoto wao wawe askari shujaa wa imani yao huku wakiandaa kizazi chenye imani thabiti, chenye maadili na utu wema katika jamii.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU