‘Ukame siyo mpango wa Mungu, tumejitakia’ Ask. Amani

ASKOFU wa Jimbo Katoliki Moshi Mhashamu Isaac Amani amesema kuwa athari za mabadiliko ya tabia nchi, kama ukame na mlipuko wa magonjwa, ni matokeo ya uzembe wa mwanadamu katika kuhifadhi mazingira.
Ameeleza hayo hivi karibuni alipokuwa anafungua Mkutano wa Kitaifa wa Wakurugenzi wa Idara na Vitengo vilivyopo chini ya Kurugenzi ya Uchungaji, uliofanyika katika Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania na kuhudhuriwa na wakurugenzi kutoka majimbo mbalimbali katoliki nchini.
“Kutunza mazingira na usafi ni amri ya Mungu. Tumepewa jukumu la kuhifadhi uhai kwa kuyatunza mazingira, tukizembea jukumu hilo tunaonja athari za mabadiliko ya tabianchi. Athari hizi tunatengeneza sisi, siyo mpango wa Mungu” ameeleza Askofu Amani.
Wakati huo huo Askofu Amani amesema kuwa, katika kusherehekea Jubilei ya miaka 150 ya uinjilishaji na miaka 100 ya Upadri Tanzania, ni lazima kuweka mkazo wa kuinjilisha katika familia za kikristo.
Amesema kuwa nafasi ya familia na jumuiya katika uchungaji ni kubwa na kwamba nafsi ya mtu hujengeka na kuponywa katika familia.
“Kanisa linaadhimisha zawadi ya umri wa miaka 150 ya imani Katoliki Tanzania. Neno la Mungu lijenge tamaduni mpya katika familia, kwani familia yenye nguvu na mshikamano hustawisha taifa” ameeleza.

Pia ametoa wito kwa waamini nchini kutumia maadhimisho ya miaka 150 ya uinjilishaji na miaka 100 ya upadri Tanzania kwa kufanya hija katika maeneo ya kihistoria. Amesema kuwa kufanya hija kunawaunganisha waamini pamoja na matukio ya zamani yanayowaimarisha kiimani.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU