Wimbi la kuuawa kwa walinzi geita lamsononesha Askofu Kassala

WIMBI la kuuawa mara kwa mara kwa walinzi katika maeneo mbalimbali ya Halmashauri ya mji wa Geita yamemsononesha na kumtia simanzi Askofu Flavian Kassala wa Jimbo Katoliki la Geita.

Akizungumzia hali hiyo katika maadhimisho ya Misa maalum ya kutoa kutoa Sakramenti ya Kipaimara katika Kanisa Kuu la Jimbo la Bikira Maria Malkia wa Amani ,alisema anasikitishwa kuona walinzi wakiendelea kuuawa kila wakati.

Alisema hali ya namna hiyo inaleta simanzi kubwa na pia ni mshangao kwani pamoja na kuuawa kwa walinzi hao wauaji hakuna kitu wanachochukua hali inayofanya watu watu kuyahusisha matukio hayo na imani za kishirikina.

"Hali hii ya kuuawa kila siku kwa walinzi katika mji wetu wa Geita si ishara nzuri hata kidogo na inashangaza hawa wanaohusika na mauaji hayo hawachukui kitu chochote baada ya mauaji inatia shaka kuona imani za kishirikina zikiendelea kushamiri kwa kiwango hiki" alisema Askofu Kassala.

Hadi sasa jumla ya walinzi 20 wa makampuni mbalimbali za ulinzi na walinzi binafsi wameuawa katika maeneo mbalimbali ya mji wa Geita huku jeshi la Polisi likishindwa kutoa majibu sahihi juu ya vifo hali inayowafanya wananchi kubaki katika hali ya wasiwasi juu ya vitendo hivyo.

Askofu Kassala aliwahimiza waaamini hao na watu wengine kuacha kudhani watapata nyota kwa kukatisha maisha ya wenzao akihimiza kutokubalika kwa matendo hayo.

"Ndugu zangu wapendwa hivi kuhangaika kutafuta nyota kwa wale ambao hawajaiona nyota? maana nyoya za waganga ni za muda na mtu ukihangaika na kimwanga kidogo kinachokwisha muda mfupi giza litakapokuja utaongozwa na nini?" alisema

Aliwahimiza waamini hao kuendelea kuwa na sifa za kuwa wafuasi wa Kristo kwa matendo na mwenendo mwema huku akiwahiza sana kuwa daima na huruma kwa wengine na kusameheana wanapokoseana.

Katika hatua nyingine Askofu Kassala aliwahimiza waamini kujitahidi kufunga ndoa na kuacha visingizio vya kuchelewa kufunga ndoa kwa kisingizio cha sherehe na kuendelea kujifungia masakramenti hali aliyosema kiroho siyo jema.

Aidha alitoa wito kwa waamini na watu mbalimbali wa ndani na nje ya Jimbo kujitokeza kukisaidia kituo cha kulea watoto yatima cha Moyo wa huruma kwani alisema gharama za kuwasomesha watoto hao zimekuwa kubwa na kulielemea Jimbo.


Aliipongeza Parokia ya Bikira Maria wa Fatima kwa mchango wake katika kituo hicho wakati wa Krismasi ambapo waamini wa Parokia hiy walichangia jumla ya shilingi milioni saba za papo kwa papo ,huku akiihimiza na Parokia hiyo ya Kanisa kuu kuweka mipango ya kusaidia kituo hicho.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU