Maridhiano baina ya walezi huleta ufanisi katika malezi

KUMEKUWA na hulka tofauti tofauti za walezi kuhusu matokeo ya malezi wanayowapatia watoto wao. Mtoto anapokuwa na mafanikio huwa ni mali ya Baba ila anapokuwa hajafanya vizuri anakuwa ni mali ya Mama.
Kwa mfano, utamsikia Baba akitoa kauli  unaona huyu mtoto wako alivyo mkorofi! ila akiwa ni afisa fulani kwa maana ya mafanikio bora baba atajigamba kila kona mnamwona mtoto wangu, pale nimetoa jembe bwana!
Ni katika maana hii nadiriki kusema kuwa malezi ni suala mfungamano, yaani ni maridhiano ya mama na baba kuhusu namna ya kutoa malezi ili matokeo yawe ni mali ya wazazi wote wawili.
Kulea: Ni kazi ya wote wawili. Hakuna mwenye majukumu hayo alafu mwingine afurahie au achukie matokeo yake. Mara nyingi malezi ya watoto kwa maana ya kugombeza, kufundisha kazi, na hata kuhangaikia elimu limekuwa ni jukumu la mama kwa walio wengi.
Ni lazima kutambua kuwa kazi ya kulea ni ya wote wawili iwe ni wakati wa kufaa au la, yaani isiwe baba yuko kimya anayeadhibu ni mama peke yake, hapo ni rahisi kwa mtoto kuelewa kuwa ni mama ndiye aliyenilea kwa hiyo baba si mlezi wangu.
Kuwapatia watoto majina: Hili nalo pia ni suala muhimu katika malezi. Ni taratibu katika mila nyingi kuwapa watoto majina ya wazazi wao. Kwa mfano kama baba yako aliitwa Samweli ukizaa mtoto utamwita Samweli. Ni maridhiano katika kutoa majina haya kutakapoleta tija katika malezi kwani kumekuwa na mvutano kwa walio wengi kuita majina mengi ya upande mmoja bila kufikiria mwingine.
Hii inachangia malezi hafifu kwani upande mmoja utaona haukuthaminiwa hivyo mwenye watoto alee mwenyewe watoto wake.Ni suala la kukubaliana kwa haki kabisa kugawana wazao kwa maana ya kuwapa majina ya pande zote mbili kwa makubaliano maalumu la sivyo mmoja ataona hana haki  ya kulea.
Dini kwa watoto ni makubaliano: Watoto wanaelekezwa dini fulani  waifuate na wazazi wao. Suala hili ni muhimu katika malezi kwani kumekuwa na kasumba ya upande mmoja kuvutia watoto upande wake bila kukaa na kukubaliana watoto wawe katika msingi gani wa imani ili kuwa rahisi kuwafuatilia.
Ni mshangao kuona familia moja kuwa na dini zaidi ya nne au madhehebu zaidi ya manne. Je mtawaleaje watoto hawa? humo ndani si itakuwa ni mafarakano ya kidini tu ? ”wasabato hawali kambale, waislamu hawali nguruwe ,wahindu hawali ngombe..je wakatoliki ndani ya nyumba hiyo wataishije” alisema rafiki yangu mmoja Aloisi nilipomhoji ]
Je itakuwaje humo ndani?Ni vyema kukubaliana kuwa watoto wakue katika maadili Fulani ya kidini ili wote muweze kuelekeza nguvu katika imani hiyo mnayotaka watoto wenu wawe nayo.
Kutembelea familia ya upande mwingine: Kuna utaratibu mzuri katika jamii nyingi kutembeleana. Utaratibu huu unashirikishwa pia kwa watoto pale wanaporuhusiwa kulala kwa bibi au babu. La kushangaza ni pale watoto wanaporuhusiwa kutembelea upande mmoja tu na kukatazwa upande mwingine.
Hii haifai kwa malezi kwani lengo la kuwaruhusu kutembeleana ni ili wafahamu ndugu wa pande zote mbili. Unapowakataza upande mmoja basi wanaanza kukua na chuki kuwa upande wa mama kwa mfano ndugu zake ni wabaya na haturuhusiwi kuwatembelea na kukaa nao. Walezi jitahidini kuwa na mfumo mmoja, kama ni kuwakataza wakatazeni pande zote mbili kama ni ruhusa toeni kwa pande zote mkizingatia kiasi na uhuru wenye mipaka.
Malezi ni suala la pamoja baina ya pande mbili,ni vyema kujenga mfumo wa pamoja ili kuwafanya watoto wasiegemee upande mmoja na kudharau mwingine. Hili linawajengea walelewa uwezo wa kutambua kuwa katika maisha zipo pande mbili yaani malezi toka kwa mama na Baba ambayo kamwe hayatengani, hivyo si rahisi kwa watoto kupinga malezi wakiona wanayoelekezwa yanatoka kwa wote wawili [baba na mama]
Mwandishi ni Paroko wa Parokia ya Ndungu

Jimbo Katoliki la Same.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU