Elimu ndogo ya katekesi chanzo cha uchanga wa imani kwa waamini

IMEELEZWA kuwa katekesi ndogo na isiyotosha ya sakramenti na maadhimisho ya liturujia ni chanzo cha uchanga wa imani kwa waamini na hata kupelekea kuhama makanisa.
Hayo yamebainishwa na Padri Titus Amigu wa Jimbo Katoliki Lindi wakati akitoa mada katika mkutano wa siku tatu wa Mapadri wanaounda Umoja wa Mapadri Tanzania (UMAWATA), uliofanyika katika Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC).
Padri Amigu amewataka mapadri kufundisha katekesi ya kina ili kuwasaidia waamini waelewe vyema badala ya kuwaachia makatekista pekee. Amekumbusha kuwa katekesi ni muhimu kwa waamini hasa kujifunza kuhusiana na sakramenti na maadhimisho ya liturujia kwa jumla.
“Sisi wenyewe tunasomea vyema huko Seminari Kuu na bado hatufanyi vizuri, je, kwa ndugu wasioelewa? Watu wetu huambulia katekesi ndogo kwa ajili ya ubatizo, kipaimara na komunio ya kwanza na kidogo tu kabla ya kufunga ndoa. Zaidi ya hapo katekesi yenyewe hufanywa kwa uzimamoto na pengine kwa kuachiwa katekista tu. Mkasa huu unabakiza watu wetu katika utoto wa imani na hivyo kuwa wahanga wa mafundisho ya kigeni na kuhamahama makanisa kwa vile hawaoni tofauti yoyote kati ya makanisa” ameeleza Padri Amigu.
Ametaja madhara ya waamini kukosa elimu ya katekesi kuwa ni pamoja na kudharaulika kwa sakramenti hususan Ubatizo, Ekaristi Takatifu, Kitubio, Mpako wa Wagonjwa, Ndoa na Upadri.
“Lakini siku hizi, pengine kwa sababu ya sisi kutoeleza na kufanya katekesi ya sakramenti, sakramenti kadhaa zinadharaulika. Hazijulikani faida yake wala umuhimu wake. Ukichanganya na teolojia ya Martin Luther, sakramenti saba zinashambuliwa kwa kejeli nyingi. Matokeo yake ni kudharaulika. Ubatizo unaonekana hauna uzito mbele ya “ubatizo katika Roho”. Mahali pengine watu hawaithamini Ekaristi Takatifu  wakati ndiyo kiini cha maisha ya padre na maisha ya Mkatoliki yeyote” amesema.
Aidha Padri Amigu ametoa wito kwa mapadri kutoogopa kuonya kwa kuwa Nabii hapaswi kuwa mwoga kwa sababu anasimamia ukweli. Amesema kuwa kama mlinzi wa kundi la wafuasi wa Kristo na mtu anayewajibika kuwafikisha sala mbinguni kondoo wake, padri anapaswa kutimiza ofisi yake ya unabii pasipo kuogopa.
Lakini siyo uongo mapadri mara kadhaa tunarudi nyuma katika unabii kwa  kuchelea kuharibu uhusiano wetu na watu. Tunafumbwa vinywa na kutengenezwa mabubu na matokeo yake tunakuwa viwete mbele ya yote yanayohatarisha mustakabali wa kiimani katika parokia au taasisi tulizopewa dhamana” ameeleza.

Pia amewaomba mapadri kuwekeza katika watoto na vijana akisema kuwa hiyo ni busara ya kutaka kuvuna mavuno mazuri na makubwa siku za usoni. Amesema kuwa kushindwa au kudharau kuwekeza katika watoto na vijana, kwa kujua au kwa kutokujua, ni kufanya kosa kubwa.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU