KIONGOZI MBIO ZA MWENGE ALIPONGEZA KANISA KATOLIKI
Kiongozi wa mbio za Mwenge
kitaifa mwaka 2017 Bw. Amour Ahmad Amour amelipongeza Jimbo Katoliki Ifakara
kwa kuendeleza mradi wa Ujenzi wa Hospitali ya Good Samaritan kwa ajili ya
matibabu ya wagonjwa wa Kansa iliyopo katika Halmashauri ya mji wa Ifakara.
Bw. Amour amesema hayo
hivi karibuni kwenye Msafara wa Mwenge wa Uhuru ulipofika katika eneo la ujenzi
wa mradi huo na kuweka jiwe la msingi ambapo ujenzi huo unatarajiwa kukamilika
kabla ya mwezi Desemba mwaka huu.
Aidha Kiongozi huyo wa
mbio za Mwenge Kitaifa kwa mwaka huu amesema kuwa kukamilika kwa Hospitali hiyo
kutasaidia watu wengi kupata huduma kwa urahisi kwani huduma zitakuwa zikitolewa
bila malipo ambapo wananchi wengi wenye
matatizo ya Kansa kutoka maeneo yote nchini watahudumiwa bure wakiwa hospitalini
hapo.
“Nawapongeza sana na
nawaomba msichoke kufanya vitu vizuri kama hivi, kwani kukamilika hapa
kutasaidia wananchi wa Ifakara, Kilombero, Morogoro na Tanzania nzima tena kuna
watu wengine watatoka kwetu Zanzibar kuja hapa na tunawaomba muwapokee,” amesema
Amour.
Pia Amour amewataka
wananchi wote wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara na Wilaya ya Kilombero kwa
ujumla kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Kanisa Katoliki kwa kuwezesha
huduma mbalimbali hususani za afya kwa jamii.
Katika Risala iliyosomwa
na Padri Jerish Geory kwa niaba ya Jimbo Katoliki Ifakara, amesema kuwa mradi huo ulianza mwaka 2015 na unatarajiwa
kukamilika mwishoni mwa mwaka huu.
Aidha ameeleza lengo la
mradi huo kuwa ni kutoa matibabu kwa wananchi wa hali ya chini ambao hawana
uwezo wa kwenda kupata matibabu katika hospitali mbalimbali zilizopo mikoa ya
mbali.
Risala hiyo pia
ilibainisha utekelezaji wa mradi kuwa mradi huo kuwa mpaka kukamilika kwake
unatarajiwa kuwa na majengo 11 ikiwa ni pamoja na wodi 4, jengo la utawala,
jengo la mapokezi, jengo la mikutano, chumba cha upasuaji pamoja na miundombinu
mingine ya msingi, ambapo mpaka sasa
zaidi ya Majengo 9 yapo katika hatua za umaliziaji.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Ulanga aliyemwakilisha Mkuu
wa Wilaya ya Kilombero Bwana Jacob Kasema
amesema kuwa anathamini uwepo wa Jimbo Katoliki na kuomba makanisa mengine
kuunga mkono jitihada mbalimbali ili kusaidia kupunguza changamoto za
afya, elimu na maji kwa jamii.
Comments
Post a Comment