TUMUUNGE MKONO RAIS SUALA LA MIMBA SHULENI-ASKOFU KASSALA
Askofu wa Jimbo Katoliki Geita Mhashamu Flavian Kassala amewataka
mapadri kutoogopa kusema ukweli ili kuiepusha jamii ya Tanzania kuanguka
kimaadili, hasa kwa baadhi ya watu kuilazimisha jamii kufanya mambo haramu kwa
kisingizio cha haki za binadamu.
Aidha Askofu Kassala ameshangazwa na baadhi ya wazazi wanaopingana na hatua ya Serikali ya kuwanusuru mabinti walio shuleni dhidi ya mimba za shuleni na magonjwa. Askofu Kassala amewaomba wananchi kumuunga mkono na si kumbeza Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mhe. John Magufuli kwa ujasiri wake kukemea mambo yanayosababisha kumomonyoka kwa maadili nchini.
Akizungumza katika Misa Takatifu ya kuadhimisha miaka 25 ya Upadri kwa mapadri wawili wa Jimbo Geita, Revocatus Makonge na Deusdedit Kaigoma jumapili iliyopita, Askofu Kassala amemsifu Rais wa Tanzania kwa kusimamia ukweli kuhusu ongezeko la vitendo vya watoto wa shule kubeba mimba na utoaji mimba.
"Ni kitendo cha aibu kwa watanzania, wazazi na baadhi ya
wanasiasa kusimama kidete na kupinga jitihada za makusudi za kuwanusuru mabinti
zetu wasipate ujauzito wakiwa masomoni, je tunapoiomba Serikali kuwarejesha
masomoni watoto waliopata mimba hii si sawa na kusema tunataka mabinti wengi
zaidi kupata ujauzito?” Amehoji.
Akiwapongeza mapadri Makonge na Kaigoma kwa utumishi uliojaa
uvumilivu kwa miaka 25 katika Daraja Takatifu ya Upadri, amewataka kumuiga
Mtakatifu Paulo kutambua hazina kubwa waliyonayo ya utumishi japo katika vyombo
vya udongo na hivyo kutoogopa kuvumilia masumbufu, magumu mengi na hata
kutengwa ili kuifikisha Injili ya Kristo.
Aidha Mhashamu Kassala ametoa wito kwa watanzania wote kuwa karibu
na Jeshi la Polisi na kulipa ushirikiano mkubwa ili kulisaidia kutekeleza
wajibu wake. Amesema maaskari polisi kwa sasa wanatekeleza huduma yao kwa woga
kufuatia vitendo vya baadhi ya watu kuwashambulia na kuwaletea majeraha
makubwa.
Amesema jamii yote ikishirikiana hakika watu hao wachache
wanaotaka kuvuruga amani ya Taifa letu watabainika na kuchukuliwa hatua.
Katika Misa hiyo waamini wengi walifurika kuwapongeza Mapadre Revocatus Makonge, ambaye aliwahi kuwa Mkuu wa Idara ya Mawasiliano Jamii ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) kati ya 2004 hadi 2010, na Padri Deusdedit Kaigoma ambaye alihudumu Parokia za Geita Seminari, Kalebejo na Bukoli na kisha akaenda Marekani hadi hivi sasa. Katika pongezi zilizotolewa, wajubilanti walipata jumla ya zawadi zenye thamani ya zaidi ya milioni 13 za kitanzania, ambapo Mhashamu Baba Askofu aliwakumbusha kuwa ziwasaidie kuamsha utume wao, wawe na moyo kama siku ya kwanza ya Upadrisho.
Wakati huo huo
Askofu Flavian Kassala amemteua padri Yohane Mabula kuwa Katibu wa Jimbo
(Chancellor) na Katibu wa Askofu na kisha akampa kiapo cha utii na usiri ambapo
atasaidiana na Askofu katika utendaji wa Jimbo.
Naye padri Mabula akitoa kiapo hicho mbele ya waamini wengi
waliohudhuria sherehe hizi za Jubilei katika Kanisa Kuu la Jimbo, ameahidi kuwa
mtiifu, msiri na mshauri mzuri wa Baba Askofu katika kuwezesha ufame wa Mungu
kukua zaidi na zaidi.
Comments
Post a Comment