MIAKA 50 YA UCHUNGAJI: PADRI SHAO AMSHUKURU MWENYEZI MUNGU
Padri Pius Shao anayefanya utume katika Jimbo Kuu Katoliki
Arusha, ameadhimisha miaka hamsini (50) ya Upadri, adhimisho ambalo limekwenda
sambamba na Misa Takatifu kumshukuru Mungu kwa yote aliyomjalia katika kipindi
chote hicho.
Akimwakilisha Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Arusha, Wakili wa Jimbo hilo (Vicar General) Padri Simon Tenges katika
mahubiri yake, amemfananisha padri Shao na mmoja kati ya wagonjwa kumi wa ukoma
walioponyeshwa na Yesu na kurudi kumpa
Yesu Kristo shukrani.
Padri Pius amefanya mengi katika Jimbo Kuu Arusha,
hasa wakati akiwa Mkuu wa Idara ya Uinjilishaji ambapo ametembelea parokia na
vigango mbalimbali katika Jimbo lenye ukubwa wa Kilometa za mraba 64,340 akiinjilisha
kwa kina. Amechangia kufunguliwa parokia mpya ya Enduimet na vigango vyake wakati
huo huo akiimarisha parokia nyingine mpya ya Kamwanga na vigango vyake.
Pia Padri Simon Tenges amemfananisha na askari
hodari aliye vitani anayetetea watu wake bila kuangalia kabila lao, dini, mila au desturi huku akisaidia pia ujenzi wa
Hospitali yenye hadhi, shule ya chekechea na kuboresha mazingira ya asili ya
maeneo ya wakaaji wake.
Hata hivyo padri Pius Shao amekumbana na vizingiti
vingi vya mazingira, mila na tamaduni hasa zile potovu, na ameweza kukabiliana
navyo kikamilifu, hii ni pamoja na kuweka watu wa matabaka, hulka na tabia
tofauti katika kundi moja linalopendana na kusaidiana.
Kwenye Misa hiyo ya kumshukuru Mungu, wamehudhuria
mapadri kadhaa wa Jimbo Kuu Arusha na wana jubilee wenzake wawili kutoka Jimbo
Katoliki Moshi, padri Caetan Kazi na Everist.
Comments
Post a Comment