Askofu amwomba IGP Sirro Kanda Maalumu Ngara
ASKOFU wa Jimbo Katoliki Rulenge-Ngara,
Mhashamu Severine Niwe-Mugizi, amesema ana imani na uongozi wa Mkuu mpya wa
Jeshi la Polisi nchini (IGP), Simon Sirro na amemuomba kuunda kanda au mkoa
maalumu wa kipolisi katika Jimbo hilo ili kukabili matukio ya kihalifu yakiwamo
ya uingizaji silaha haramu nchini.
Maeneo mbalimbali ya mipakani mwa nchi
hususani katika mikoa ya Kagera na Kigoma yamekuwa na matukio mengi ya kihalifu
yanayodaiwa kuchangiwa pia na wahamiaji haramu au wakimbizi toka nchi jirani za
Rwanda, Burundi na hata Uganda.
Hivi karibuni, Rais John Magufuli
amemteua aliyekuwa Kamanda wa Polisi Kanda Malumu ya Dar es Salaam, Kamishna
Simon Sirro, kuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania akichukua nafasi ya Ernest
Mangu ambaye taarifa ya Ikulu ilisema, atapangiwa kazi nyingine.
Wakati watu mbalimbali wakimhimiza
kutupia macho na kusafisha maeneo mbalimbali yanayolalamikiwa yakiwamo mauaji
yanayofanywa na watu wasiojulikana huko Kibiti na maeneo mengine mkoani Pwani,
malalamiko ya raia kubambikwa kesi, ujambazi wa kutumia silaha na uhusiano
mbaya na baadhi ya vyama vya siasa na jeshi lake, yeye mwenyewe amesema
amejipanga kupambana na matukio ya kihalifu hata kama ni kwa ubaya.
Akizungumza kwa simu na KIONGOZI toka
Rulenge, Mhashamu Niwe-Mugizi amesema katikati ya juma kuwa, ingawa mara nyingi
amekuwa akitoa ombi hili lakini halitekelezwi, hataacha kutimiza wajibu wake wa
kusema na kukumbusha yale anayoona yanafaa kwa ustawi wa jamii.
“Hiki kilio changu sasa kimekuwa kama
machozi ya samaki hata yakitoka, hakuna anayeyaona maana yote yanaishia majini
tu. Nimesema mpaka sasa nimechoka, lakini hakuna anayejali sijui tunasubiri
lipi litokee,”amesema.
Mhashamu Niwe-Mugizi amesema Jimbo
Katoliki Rulenge-Ngara ambalo kikanisa linahusisha wilaya za Ngara, Chato na
Biharamulo, ni eneo lenye changamoto nyingi za kiusalama kwa kuwa lipo jirani
na nchi ambazo mara nyingi zina migogoro na hivyo, kuingilika kirahisi na
wahamiaji haramu au wakimbizi ambao baadhi yao huwa na silaha haramu
zinazotumika kufanya uhalifu nchini.
“Ngara ni eneo hatarishi kutokana na
kuwa jirani na nchi za Rwanda, Burundi na Uganda na kutokana na mwingiliano wa
watu, ni vigumu kuwadhibiti na hivyo usalama unakuwa kidogo. Wakimbizi wengi
wanapita hapa kwenda kwenye makambi. Huu mwingiliano rahisi, unatuweka sisi
watu wa maeneo haya katika hatari,” amefafanua.
“Namuomba sana huyu IGP mpya, atusikie
ili tusisubiri mpaka jambo lifumuke na mambo yaharibike, eti ndipo tuanze
kukimbia kama zimamoto. Ndiyo maana ninaliomba Jeshi la Polisi na Serikali kwa
jumla, waliangalie eneo hili kwa jicho makini kabisa na kulifanya kuwa Kanda au
mkoa maalumu wa kipolisi. Hii itaimarisha usalama eneo hili.”
Amesema kutokana na mwingiliano uliopo
na nchi jirani, anaamini kuwa silaha nyingi zinazotumika katika maeneo
mbalimbali nchini kwa mambo ya kihalifu, zinapita maeneo hayo na hivyo, lazima
kushtuka mapema badala ya kusubiri madhara zaidi kutokea.
Comments
Post a Comment