ASKOFU MINDE AWAASA WAZAZI KUCHOCHEA MAADILI
Wazazi wamehimizwa kuchochea maadili
kwa watoto katika kipindi hiki ili waweze kuishi maisha yanayompendeza Mungu na
jamii kwa ujumla kwani bila hivyo kuutafuta ufalme wa mbingu haitawezekana.
Maneno hayo yamesemwa na Askofu wa
Jimbo Katoliki Kahama Mhashamu Ludovick Minde katika adhimisho la ibada ya misa
ya kupaa kwa Bwana katika parokia ya Ekaristi Takatifu Kabuhima.
Askofu Minde amesema hata katika
uumbaji, Mwenyezi Mungu alimuumba Eva kutoka ubavu wa kuume wa Adam hivyo hata
katika maadhimisho ya siku ya kupaa kwaYesu Kristo jamii inakumbushwa kuwa anakwenda
kukaa kuume kwa Mungu Baba.
“Baada ya kupaa mbinguni Bwana wetu
Yesu Kristo, wafuasi wake walishikamana pamoja nao wanawake na Mariamu mama
yake Yesu na ndugu zake, hawa wote walidumu kwa moyo mmoja katika kusali.
Hata sisi inatupasa kusali na kufanya kazi.”
Naye Dekano wa dekania ya Ushirombo
ambaye pia ni Paroko wa parokia ya Ekaristi Takatifu Kabuhima padri Salvatore
Guerrera, amemshukuru Mhashamu Askofu kwa moyo wa upendo kwa wanaparokia ya
Ekaristi Takatifu kwani amekuwa akiwatembelea mara kwa mara na hii
inadhihirisha kuwa huwa anawakumbuka katika maombi na sala.
Amemshukuru pia Sista Mkuu Mama Theresia
wa shirika la wamisionari Wabenediktini kutoka Ndanda Mtwara pamoja na watawa
wenzake ambao wapo parokiani hapo kwa ajili ya kusalimia na kusali pamoja na
wanafamilia wa Mungu.
Na, Shokolo Hosea, Kabuhima Kahama
Comments
Post a Comment