Askofu Ruzoka akikabidhi kituo cha afya Kaliua majengo yenye thamani ya shilingi 700,000,000
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Tabora Mhashamu Paulo
Ruzoka hivi karibuni amekabidhi majengo mapya katika kituo cha afya Kaliua
yenye thamani ya shilingi milioni mia saba (700,000,000) ikiwa ni juhudi ya
kumkomboa mwanadamu dhidi ya adui maradhi.
Akikabidhi majengo hayo mapya Askofu Mkuu Ruzoka amesema Kanisa
Katoliki linashirikiana na Serikali ya Tanzania katika juhudi za kumkomboa mwanadamu
dhidi ya maradhi ili aweze kujipatia maendeleo kwa wakati, na kwa mantiki hiyo
Jimbo Kuu Katoliki Tabora limeendelea kukuza maendeleo kwa kutoa huduma za
afya, elimu, maji safi na salama na nyanja zingine za kijamii.
Askofu Mkuu Ruzoka amewaagiza waganga na wauguzi wa kituo
hicho cha afya kutunza miundo mbinu yote ya kituo na kutoa huduma yao kwa
weledi ili huduma iende sambamba na miundo mbinu mipya iliyokabidhiwa.
Pia Askofu Mkuu Ruzoka aliwataka waganga na wauguzi kulenga
zaidi watu wa kipato cha chini katika kuwapa huduma bora akinukuu maneno toka
mwinjili Matayo kuwa chochote mlichomtendea mmoja wa hao wadogo mlinitendea
mimi.(Mt.25:31-46)
Baadhi ya majengo mapya aliyoyabariki na kukabidhi ni jengo
la wagonjwa wa nje yaani (OPD) , wodi ya wakina mama, wodi ya wanaume, wodi ya
watoto, wodi ya wakina mama wajawazito na chumba cha kuhifadhia maiti (mortuary),
vyote vikiwa na thamani ya shilingi milioni 700 za kitanzania.
Akitoa mahubiri yake katika Misa Takatifu ya kukabidhi
majengo hayo, Askofu Mkuu Paulo Ruzoka ameiomba Serikali kuhakikisha inatoa
ulinzi wa watanzania na mali zao ili Kanisa lipate mazingira rafiki ya kumletea
maendeleo mtanzania, kwani pasipo na amani hakuna maendeleo yoyote yanayoweza
kufanyika.
Aidha Askofu Mkuu Ruzoka ametoa wito kwa waamini wote
kutumia kituo hicho cha afya ili kuboresha afya zao na kupuuza baadhi ya watu
wanaowagiribu watu wasitumie huduma za afya kwa kisingizio cha Mungu peke yake
kuwaponya bila msaada wa huduma za kitabibu.
Naye Katibu wa afya Jimbo Kuu Tabora padri Alex Nduwayo
akitoa taarifa yake amesema kuwa kituo bado kina changamoto kama vile uchakavu
wa baadhi ya majengo kama vile chumba cha upasuaji, vifaa tiba nakadhalika.
Mganga Mkuu wa mkoa wa Tabora aliyetoa salamu kwa niaba ya
Serikali amepongeza juhudi zilizofanyika kuboresha miundo mbinu hiyo na kuahidi
kuongeza wahudumu katika kituo cha afya na kuwapa changamoto ya kuangalia upya
huduma za kituo hicho hasa upande wa mama na mtoto ili kupunguza rufaa za
hospitali jirani ya wilaya ya Urambo.
Kituo cha afya Kaliua kilianzishwa kama zahanati tarehe
2.7.1962 na aliyekuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Tabora Hayati Marko Mihayo chini
ya usimamizi wa masista wa Grail. Mwaka 1971 kituo kilichukuliwa na Serikali na
watumishi wote kulipwa mishahara na serikali, ambapo tarehe 15.8.1997 Serikali ilikabidhi kituo kwa Jimbo Kuu
Tabora chini ya uongozi wa Hayati Askofu Mkuu Mario A. Mgulunde na shirika la
masista wa Mabinti wa Maria walianza kutoa huduma mpaka leo hii.
Jimbo Kuu Katoliki Tabora limetekeleza
mradi huu kwa ushirikiano na Baraza la Maaskofu Katoliki Italia (CEI). Hafla
hiyo ilihudhuriwa pia na Mbunge wa Kaliua Mh.Magdalena Sakaya , mwakilishi wa Mkuu
wa wilaya ya Kaliua, na mwakilishi wa Mkurugenzi wa Kaliua.
Kituo hicho cha afya kinatarajiwa kupanda
hadhi na kuwa Hospitali hivi karibuni.
Comments
Post a Comment