MAFRATERI WAWE NA MALENGO ENDELEVU
Mafrateri wa seminari Kuu ya Mtakatifu Paulo Mtume
Kipalapala wameaswa kuwa na malengo endelevu katika maisha yao ya kila siku ili
kuweza kuhimili changamoto za maisha yao hapo baadaye.
Rai hiyo imetolewa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki
Tabora Mhashamu Paulo Ruzoka hivi karibuni katika Adhimisho la Misa Takatifu
aliyoiadhimisha seminarini hapo.
Askofu Mkuu Ruzoka amesema kila mwanadamu anapaswa kuishi
mwenyewe katika maisha yake ya kila siku na si kuishi maisha ya mtu mwingine au
maisha tegemezi ambayo si rahisi kumfanya mtu huyo kujiletea mafanikio.
Aidha Askofu Mkuu Ruzoka amewaomba mafrateri kuishi maisha
adilifu yatakayowasaidia kufikia lengo kuu yaani uzima wa milele na hasa
wajihoji daima nipo wapi? naenda wapi? aina hii ya maswali ni muhimu katika
safari yao ya kuelekea maisha ya upadri, bila hivyo wataishia kutapatapa.
Askofu Mkuu Ruzoka pia ametoa wito kwa wabatizwa wote wajibu
wa kusaidiana na kuelekezana yale yanayotupeleka katika uzima wa milele.
Katika mahubiri yake Askofu Mkuu amewasisitiza mapadri,
mafrateri, watawa na wahudumu wa seminari daima kuchangamkia sakramenti za Kanisa
bila kusahau sakramenti za upatanisho na Ekaristi Takatifu zinazotupatia uwepo
wa Kristo Yesu katika maisha yetu ya kila siku.
Akilinganisha wito wa Ibrahim, Askofu Mkuu ametoa wito kwa
kila mkristo kujitahidi kudumu katika Imani na Utii kwa Mungu hasa wakati wa
changamoto tunazokutana nazo katika maisha na daima tuyapokee mapenzi ya Mungu
bila kukata tama, kwani yote kwa Mungu yanawezekana.
Aidha mafrateri wameelezwa umuhimu wa kujiwekea utaratibu
mzuri katika maisha yao ili waweze kutumia muda wao vizuri ili kuhimili
changamoto za ulimwengu wa leo.
Wakati huohuo, Askofu Mkuu Ruzoka ametoa wito kwa kila mkristo
kuiombea nchi yetu amani na utulivu kwani pasipo na amani hakuna maendeleo.
Mwaka huu 2017 mafrateri 24 toka majimbo
mbalimbali Tanzania wamehitimu malezi yao seminarini hapo. Mahafali hayo
yamehudhuriwa na mapadri, watawa, mafrateri na wahudumu wa seminari.
Comments
Post a Comment