Kahama wamkumbuka Mtakatifu Karoli Lwanga
Padri Peter Kadundu wa Jimbo
Katoliki Kahama amewataka waamini kuwa mashuhuda wa imani kiroho na
kimwili kwa kuishi maisha ya matendo mema ya sala ya kumpendeza Mwenyezi
Mungu na kuwa na upendo kwa watu wote.
Padri Kadundu ambaye ni makamu wa Askofu
amesema hayo alipokuwa akihubiri kwenye adhimisho la misa takatifu ya
kumkumbuka Mtakatifu Karoli Lwanga iliyofanyika katika Kanisa kuu la Mtakatifu
Karoli Lwanga, parokia ya Kahama mjini.
Katika homilia yake, padri Kadundu
amesema katika maisha wakristo wanapaswa kuyajua na kuyatambua mambo matakatifu
kisha kuyatangaza na kumuomba Roho Mtakatifu awajalie kuwa wamoja wenye moyo
uliojaa furaha na undugu.
Amesema wakristo wamefundishwa Katekisimu
na kuipokea, wanapaswa kuishika
kwa kutambua kuwa kuna Mungu, Yesu Kristo na Roho Mtakatifu na ndiyo
maana Mtakatifu Karoli Lwanga na wenzake walikubali kufa kifo cha mateso makali
ya kuchomwa moto na kuungua kwa kukiri imani hiyo.
Kwa upande wake akizungumza na waamini
baada ya misa hiyo takatifu, paroko wa parokia ya Mtakatifu Karoli
Lwanga Kahama Mjini, Padri Robart Lujula amewataka waamini kuishi maisha
matakatifu ya kiroho na kimwili kwa kutenda mema katika jamii.
Parokia ya Mtakatifu Karoli Lwanga
iliyopo Kahama mjini ilianzishwa mwaka 1965 wakati huo ikiwa chini ya Jimbo Kuu
Tabora hadi mwaka 1990 ilipomegwa na kuwa chini ya Jimbo Katoliki Kahama
chini Askofu wa kwanza mwasisi hayati Askofu Mateo Shija.
Comments
Post a Comment