Miaka 100 ya Upadri/ 150 ya Uinjilishaji: Waamini watakiwa kuvienzi vituo vya ukuaji wa Imani
Wakristo nchini wametakiwa kujali na
kuthamini vitovu na vyanzo vya ukuaji wa imani katika majimbo mbalimbali
nchini ili kuimarisha uinjilishaji.
Wito huo umetolewa na Padri Cosmas
Makasi parokiani Kate katika Kanisa la Jiweni Kamba wakati wa maadhimisho wa
mwaka wa mapadri kijimbo na Hija iliyohusisha mapadri wote wa Jimbo Katoliki Sumbawanga
iliyofanyika hivi karibuni.
Padri Makasi amesema kuwa katika
kuadhimisha Jubilei ya miaka 150 ya ukristo na miaka 100 ya upadri ni vyema wakristo
hasa waamini wakatoliki kuheshimu misingi na vitovu vya imani vilivyoanzishwa
na mapadri weupe (White Fathers) na kuviendeleza.
“Ni wajibu wetu wakristo wakatoliki
nchini kote tunapoadhimisha jubilei ya miaka 150 ya imani yetu na miaka 100 ya
mapadri kutunza na kuendeleza maeneo, miradi, makanisa na huduma mbalimbali walizoziasisi
watangulizi wetu ambao walitufanya kuitambua imani na kwa kufanya hivyo tutakua
tunatunza kumbukumbu ya imani yetu kwa vizazi vijavyo katika historia ya Kanisa,"
amesema padri Makasi.
Maadhimisho ya miaka 100 ya upadri
jimboni Sumbawanga yamefanyika katika Kanisa la kwanza kujengwa jimboni
Sumbawanga ambalo limependekezwa kuwa Kanisa la Hija lililopo maeneo ya Jiweni
Kamba mwambao mwa ziwa Tanganyika lililopo katika parokia ya Kirando jimboni
Sumbawanga.
Akihitimisha Kongamano hilo la
mapadri lililojumuisha mapadri wa Jimbo Sumbawanga, Mwenyekiti wa mapadri
jimboni humo padri Joachim Sangu amesema kuwa katika kila mwaka
kupitia Dominika ya Moyo Mtakatifu wa Yesu jimboni Sumbawanga ni siku ya
mapadri kijimbo ambapo hufanya Hija, mafungo na mikutano ya ndani vyote vikiwa na
lengo la kutakatifuza mapadri ili waweze kujitakasa na kwenda kuwatakasa
waamini na kuendeleza huduma za kichungaji Jimboni.
"Tumeamua kufanya Kongamano
hili katika maeneo haya ya Jiweni Kamba mahali ambapo ndipo kiini cha ukristo
jimboni Sumbawanga kwa kuwa na Kanisa la kwanza, nyumba za watawa na mapadri,
kwa ufupi tumekuja huku kufanya Hija yetu na mafungo kwa sababu Kanisa
linaadhimisha miaka 150 ya ukristo na 100 ya upadri, hivyo tukijua kuwa chanzo
cha upadri Jimboni Sumbawanga ni maeneo haya na mapadri weupe wengi wamelala
hapa, hivyo kwa neema sala na maombezi ya mama Bikira Maria msimamizi wa Jimbo
letu atujalie mastahili katika utume wetu kwa Kanisa," Amesema Padri
Sangu.
Jimboni Sumbawanga, Jiweni Kamba ni
sehemu ambapo Kanisa la kwanza lilijengwa baada ya kusimikwa kwa mbegu ya imani
zamani ikijulikana kama Jimbo la Kalema kabla ya kugawanywa kwa Jimbo Sumbawanga
na Jimbo Katoliki Mpanda.
Sehemu hii yenye historia nyingi
katika ukuaji wa mkoa wa Rukwa na Kanisa la Sumbawanga imependekezwa kuwa
sehemu ya Hija kijimbo ili kukumbuka na kuendeleza mbegu ya imani iliyopandwa
na mapadri weupe nchini Tanzania na hasa kwa Jimbo.
Comments
Post a Comment