ASKOFU MSONGANZILA AWAKUMBUSHA WAZAZI WAJIBU WAO
Askofu wa Jimbo Katoliki Musoma Mhashamu
Michael Msonganzila amewakumbusha wazazi/walezi kuhakikisha siku haipiti bila
kupandikiza kitu kipya cha hekima kwa watoto wao,ili kuwaandaa wawe wazazi
wazuri kwa baadae na kuaondokana na masuala ya ukatili kwa watoto.
Askofu huyo ameyasema hayo kwenye
mahojiano maalum na gazeti hili, alipokuwa akizungumzia umuhimu wa kuadhimisha
siku ya mtoto wa Afrika ambayo hufanyika kila mwaka Juni 16, kwa ajili ya
kuwakumbuka watoto waliouawa kikatili huko Soweto nchini Afrika Kusini na
makaburu,wakidai haki yao, ambapo aliwafafanisha makaburu hao na maherode
waliotaka kumuua Yesu kwa sababu ya uchu wa madaraka.
Askofu Msonganzila alisema kuwa
kitendo cha kuwaua watoto hao kinafafanishwa na Herode alivyotaka watoto wote
wa chini ya miaka miwili kuuawa huko Misri, baada ya Yesu kuzaliwa na
akashindwa namna ya kumuua na kuamuru watoto wote wa kiume wauawe akijua kuwa
hata huyo Yesu aliyekuwa amezaliwa angeweza kuwa miongoni mwa watoto hao wa
chini ya miaka miwili.
Anasema kuwa kwa upande wa Kanisa Katoliki
kila inapofika Desemba 28 ya kila mwaka huwa wanaadhimisha sikukuu ya
mashahidi wa Yehova ili kuwajenga na kupata mawazo mbalimbali kutoka kwao
kwa kuwa nao wanahaki ya kusikilizwa mawazo yao kuheshimiwa na kulindwa .
“Kero hizi dhidi ya watoto
zinatakiwa zisiwepo kabisa, kutowalinda watoto ili waondoke katika
manyanyaso mbalimbali, ukatili wa kijinsia, mila na desturi kandamizi ni
sawa na uuaji na uherode, jamii inatakiwa itusaidie tuwe na dira nzuri
juu ya mambo haya, ili kuwepo na nguvu ya kupambana na masuala yote ya ukatili
wa watoto,” alisema Askofu huyo.
Aliongeza kuwa Taifa lililo na
watoto wasioendelezwa ni sawa na Taifa Gumba, kwani watoto ndio wanaotegemewa
wachukue nafasi za viongozi waliopo madarakani,na pia ndio viongozi wa familia,
Jumuiya na Taifa kwa ujumla, hivyo malezi ya watoto yasibakie kwa taasisi, bali
familia kwa maana ya wazazi wajipange kulea watoto wao na wasizilazimishe
taasisi kuwalelea watoto wao, na ndio maana Kanisa lina mradi wa Gracal Machel
Trust ambao unawasaidia watoto walioko nje ya mfumo wa shule kurudi shuleni ili
waweze kutimiza ndoto zao.
Meneja wa Mradi wa Gracal Machel
Trust (GMT) wa watoto walioko nje ya mfumo wa shule Godfrey Wawa alisema
ujio wa mradi huo utasaidia watoto 20,000 kuanzia miaka 7-17 waliokosa
elimu kwa sababu mbalimbali ikiwemo vitendo vya ukatili walivyokuwa wanafanyiwa
majumbani, kuweza kurudi shuleni na kupata elimu hiyo pia kupata haki yao
waliyoikosa na hatimaye kutimiza ndoto zao.
Wawa alisema katika kutekeleza mradi
huo watahakikisha kila mtumishi atakayefanya kazi kwenye mradi huo, anasaini
mkataba wa kuhakikisha haki za mtoto zinalindwa kuanzia kumtambua, kumuandikisha
na kumlinda mtoto aendelee kubaki shuleni hadi atakapomaliza elimu yake, kwa
kuwa ni haki yake ya msingi kupata elimu hata kama aliikosa hapo nyuma kwa
sababu mbalimbali za kifamilia na kijamii.
Alisema kuwa pia kwa sasa
wamejipanga kuanza kutoa elimu kwa kamati za shule zote, kwa walimu wakuu
na waratibu elimu kata, ili kumlinda mtoto asikimbie shule,na pia ili wajue
njia bora za mkumlinda mtoto awapo shuleni, ukizingatia kuwa hata
Serikali ilishatoa michango mbalimbali mashuleni ambayo ilikuwa ni moja ya
changamoto iliyomfanya mtoto huyo ashindwe kuendelea na masomo yake kutokana na
hali duni ya kipato cha familia.
Akibainisha changamoto wanazokumbana
nazo katika utekelzaji wa mradi huo, alisema mila na desturi ni
changamoto sana hasa ya ukeketaji, ambayo inamfanya mtoto kujiona mkubwa
baada ya kufanyiwa ukeketaji na kuwa tayari kuolewa katika umri mdogo,watoto
wengine kufichwa kwa ajili ya kutumikishwa kazi za nyumbani hasa zaidi kwa
mtoto wa kike, ambapo aliwaomba wadau mbalimbali kushirikiana kwa pamoja na
kuweka mikakati ya kumlinda na kumtunza mtoto wa Afrika.
Alitoa wito kwa jamii kutambua kuwa
mtoto ni binadamu na ni taifa la leo na kesho na jamii inatakiwa kuwekeza
kwake, kupiga vita dhidi ya mila potofu zinazomkandamiza mtoto na umasikini,
pia lazima alelewe vizuri ili aendeleze utaifa na utamaduni wa kiafrika
sambamba na uzalendo kwa nchi yake.
Akizungumza na gazeti hili
Ofisini kwake Katibu wa Mara Alliance ambao ndio watekelezaji wa
Mradi wa Mama Gracal Machel Trust na Mkurugenzi wa kituo cha sheria
na kijamii The Legal na social Assistance Centre (LSAC) Ostack Mligo
ambaye pia ni wakili alisema kuwa hali ya ukatili kwa watoto inaonekana
kupungua kwa baadhi ya maeneo kutokana na mashirika kuendelea kutoa elimu,
lakini wilaya ya Tarime ni moja kati ya wilaya inayoongoza kwa matukio ya
vitendo vya ukatili kwa watoto, ambapo kwa wiki moja zaidi ya simu
3-4 zinapigwa na wananchi mbalimbali wakieleza kutokea kwa kitendo cha ukatili
ndani ya kata au eneo fulani katika wilaya hiyo huku wilaya ya Serengeti
ikiwa na matukio machache ya ukatili na hii inawezekana ni kutokana na uwepo wa
mashirika mengi ya kutetea haki za watoto katika wilaya hiyo.
Mkurugenzi huyo alisema kuwa
kinachochangia kwa asilimia kubwa vitendo vya ukatili kwa watoto ni migogoro
ndani ya ndoa pamoja na jamii kutowajibika ipaswavyo katika kutoa taarifa au
kukemea hali ya vitendo vya ukatili inapotokea harafu mambo hayo
yanabakia kama ya kawaida ndani ya jamii na kuonekana kama ni hali ya
kawaida.
Mratibu wa shirika lililoanzishwa na
masisita wa Maryknolly Sisters linalofanya kazi katika Wilaya ya Butiama, Manispaa
ya Musoma na Musoma vijijini katika Mkoa wa Mara la Watoto Wapinge Ukimwi (WWU)
Peter Nyarufunjo alisema kuwa hali ya vitendo vya ukatili katika Mkoa wa Mara
bado ni kubwa na hali hiyo inachangiwa sana na watoto kukosa malezi ya wazazi
kwani wazazi wanahangaika na suala la kukuza uchumi au kipato ndani ya familia
na kusahau umuhimu wa malezi bora kwa watoto wao.
“Wazazi wanaondoka asubuhi kwenda
kutafuta riziki hadi jioni ndio wanarudi ,hawapati muda wa kukaa na
watoto ili wapate kujua mwenendo mzima wa makuzi ya watoto wao au kupata habari
sahihi za watoto hao, hii ndio imekuwa changamoto kubwa sana,lakini sisi
tumeanza kutoa elimu mashuleni kwa kushirikiana na dawati la jinsia ili
kupanua wigo mkubwa wa uelewa juu ya madhara ya vitendo vya ukatili kwa
watoto,”alisema Nyarufunjo.
Comments
Post a Comment