"HOFU YA MAISHA, CHANZO CHA WASOMI KUFELI"
KATIBU Mkuu wa Jimbo Katoliki
Morogoro Padri Luitfrid Makseyo amewaasa wanafunzi wa vyuo vikuu nchini
kuondokana na hofu na mashaka ya maisha katika nafsi zao ili waweze kufanya
vizuri katika mitihani yao hatimaye waje kulitumikia vyema taifa.
Padri Makseyo amesema hayo katika
mahafali ya kuwaaga wana jumuiya ya Wanafunzi Wakatoliki Tanzania [TMCS]
iliyofanyika katika Kampasi ya Mazimbu jimboni humo, ikiambatana na utoaji wa
sakramenti ya kipaimara kwa vijana 29 chuoni hapo.
Amesema moja ya sababu zinazowafanya
wanafunzi wengi nchini kutokufaulu vizuri masomo ni hofu, mashaka na woga
miongoni mwao hali inayosababisha kushindwa kujiandaa vyema katika mitihani yao
huku akisema kuwa katika maisha ya kawaida hakuna mwanadamu ambaye hajawahi
kujenga hofu moyoni mwake japo kwa wanafunzi ndio zaidi hasa wanapokabiliwa na
mitihani.
Hata hivyo Katibu huyo amesema kuwa
kutokana na hofu hiyo inayotawala miongoni mwa wanafunzi katika masomo yao,
inafika wakati wengine kujihusisha na imani za kishirikina kwa waganga wa
kienyeji pamoja na matumizi ya hirizi jambo ambalo huongeza hofu nyingine kwa
jamii inayowazunguka.
“Ukidhani kwamba Yesu hafai kwa
lolote na kwenda kwa waganga wa kienyeji nenda kajaribu uone matokeo yake,
watakwambia uchukue hirizi wakati wa kusoma ikuongoze kuelewa, kwanza kuibeba
tu unajenga mashaka mengine kwa kujiuliza pengine wenzangu wanaweza
wakaiona ikidondoka, ukifikia hatua hiyo ujitambue wazi akili zako hazipo sawasawa
badala ya kuondoa mashaka unaongeza mashaka mengine,” Amesisitiza
Sambamba na hayo Padri Makseyo
amesema kuwa njia pekee ya kuepukana na hofu ni kumwamini Mwenyezi Mungu pekee,
kwa kuwa hakuna jambo gumu linaloshindakana kwake badala ya kushiriki katika
imani za kishirikina.
Wakati huo huo Padri Makseyo ametoa
rai kwa wahitimu hao kuwa na utayari wa kulitumikia taifa, wakiamini kwamba
watanzania wanahitaji mchango wao katika upatikanaji wa huduma zinazoendana na
taaluma zao.
Mbali na hayo amewataka wahitimu
hao kujenga uvumilivu katika changamoto watakazokabiliana nazo katika
uwajibikaji wao katika taifa huku wakikubali kukosolewa na kushauriwa na
wataalamu wengine badala ya kutumia taaluma zao pekee.
“Nyie mmetekeleza jukumu lenu kwa
ajili ya kulitumikia taifa, huko mnapoenda mtakutana na makundi ya kila aina,
wajinga wanawahitaji,wasomi wanawahitaji, na jamii inawahitaji pia, jambo pekee
la kujua ni kuzitendea haki taaluma zenu bila kujiingiza katika vitendo vya
rushwa, ufisadi, na dawa za kulevya, mkiepukana na hayo mtaleta manufaa kwa
taifa.”
Comments
Post a Comment