“MAKATEKISTA WATHAMINIWE” ASKOFU KYARUZI
Askofu wa Jimbo Katoliki Sumbawanga Mhashamu Damian Kyaruzi
amewataka wakristo nchini kujali na kuthamini utume unaofanywa na makatekista
nchini kwani una mchango mkubwa katika kukuza na kutetea imani ndani ya Kanisa.
Ameyasema hayo juma hili wakati wa maadhimisho ya misa ya
kuwatuma makatekista watatu waliohitimu masomo yao kutoka katika majimbo ya
Mpanda na Sumbawanga katika kituo cha malezi cha Mt. Augustino kilichopo Matai
jimboni Sumbawanga.
“Makatekista ni muhimu na wanahitajika katika Kanisa ukilinganisha
na uhaba wa mapadri tulionao, na ukatekista ni wito na wito lazima upaliliwe,
mapadri na walei tuwathamini hawa watu ili waweze kututumikia katika mahitaji
yetu ya kiroho”. Amesema Askofu Kyaruzi.
Askofu Kyaruzi amewataka makatekista kutumika kikamilifu kwa
ajili ya Kristo na Kanisa lake kwa kuimarisha imani za wakristo kwa kukumbuka
viapo na kutenda kazi ya bwana wakisaidiana, kutiana nguvu na wenza wao ili
kutekeleza wajibu huo kwa kutambua kuwa ukatekista si kazi ambayo inatumikiwa
kipindi cha miaka kadhaa tu bali kwa hali yake ukatekista ni maisha, wito
unaopaswa kujaliwa na kuthaminiwa kwa
thamani kubwa.
Akiwapongeza makatekista hao wahitimu mkuu wa Chuo hicho cha
makatekista padri Fabian Mwiga amewaasa makatekista kuwajibika katika maeneo
yao na wasibweteke na kuonekana ni
mahohehahe katika vijiji bali wafanye kazi za kimaendeleo na zaidi walei na
viongozi wa vigango wawasaidie katika kufanikisha miradi itakayowezesha kutunza
familia zao kwani muda mwingi wanatumika katika Kanisa.
Wakitoa shukrani zao kwa uongozi na walimu wa Chuo cha Matai,
makatekista wahitimu ambao ni katekista Jastini Bilia parokia ya Mamba Jimbo
Katoliki Sumbawanga, katekista Cosmas Shirinde wa parokia ya Mamba Jimbo
Katoliki Mpanda na katekista Daudi Magazini
wa parokia ya Mt. Fransisko wa Asizi Jimbo Katoliki Sumbawanga, wameahidi
kuwa mfano bora kwa waamini watakaowatumikia ili kukuza imani na kuzidi
kumtangaza Kristo kwa watu wote.
Comments
Post a Comment